1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa fedha

Hamidou, Oumilkher7 Oktoba 2008

Heka heka katika masoko ya hisa barani Ulaya na Asia pia katika wakati ambapo Umoja wa Ulaya waahidi kuzinusuru taasisi za fedha za nchi wanachama

https://p.dw.com/p/FVQI
Mwenyekiti wa nchi za zoni ya yuro Jean Claude JunckerPicha: AP




Masoko ya hisa barani Asia yanagubikwa upya na misuko suko katika wakati ambapo yale ya Ulaya yalitulia kidogo yalipofunguliwa leo asubuhi,kufuatia juhudi za nchi za umoja wa ulaya za kunusuru akiba za watu binafsi na kuhifadhi mfumo wao wa fedha .


Mawaziri wa fedha Umoja wa ulaya wanaokutana mjini Luxembourg wamethibitisha hii leo wanatathmini mkakati wa pamoja wa umoja wa ulaya kuweza kukabiliana na kishindo kinachotokana na mzozo wa fedha ili ,miongoni mwa mengineyo papatikane hakikisho la kudhaminiwa akiba za wateja wa kibinafsi,kuanzia yuro 20 elfu hadi kufikia yuro laki moja pindi benki zikifilisika.


Nchi za zoni ya Yuro zitahakikisha hakuna taasisi yoyote kubwa ya fedha itakayojikuta katika hali ya kufilisika-amesema hapo jana mwenyekiti wa jumuia ya nchi zinazotumia sarafu ya Yuro,Jean-Claude Juncker na kusisitiza:



Kila la kufanya litafanywa,ili mradi taasisi za fedha zisifilisike.Mataifa yanajibebesha dhamana ya kuzuwia hali hiyo isitokee."


Kwa upande wake mwenyekiti wa benki kuu ya Ulaya Jean Claude Trichet ameahidi taasisi hiyo ya fedha ya Umoja wa ulaya itaendelea kumimina fedha taslim katika mfumo wa fedha kwa wakati wote utakaohitajika.


Kutokana na hofu zilizosababishwa na misuko suko ya fedha,nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya zikiwemo Ujerumani,Ufaransa,Ureno,Hispania,Ireland na Island zimetangaza hatua za kutuliza hofu za wateja.


Masoko ya hisa ya ulaya yalitulia kidogo na hisa kupanda kidogo yalipofunguliwa leo asubuhi,lakini muda si muda hisa hizo zikaanza tena kuporomoka.Soko la Dax mjini Frankfurt lilipanda kwa moja nukta 18 asili mia kabla ya kuporomoka kwa moja nukta 48 asili mia.Benki ya biashara Kommerzbank imepoteza asili mia 9 huku Deutsch Bank ikipoteza asili mia 13 ya hisa katika soko hilo loa Dax mjini Frankfurt.Hali sawa na hiyo imeshuhudiwa pia mjini London .

Mjini Moscow masoko mawili ya hisa RTS na Micex yalisitisha shughuli zake hata kabla ya kufunguliwa.

Barani Asia,masoko ya hisa yalianza kwa vurugu kabla ya hali kutulia baadae.


Faharasa ya Nikkei mjini Tokyo iliporomoka chini ya pointi elfu kumi,kwa asili mia 5.32-  mara ya kwanza baada ya kupita zaidi ya miaka mitano,kabla ya kupunguza hasara kwa asili mia 3.03 soko la hisa la mjini Tokyo lilipofungwa.


Wataalam wanahisi kuporomoka thamani ya Dollar ikilinganishwa na Yen ndio sababu ya wasi wasi katika masoko ya hisa ya Japan.


Kusambaa mzozo wa fedha barani Ulaya kunazidi kuidhoofisha pia sarafu ya Yuro iliyoporomoka na kufikia kiwango cha chini kabisa tangu kupita zaidi ya miezi 14 hapo jana ikilinganishwa na dola ya Marekani.Yuro imebadilishwa kwa dala moja na senti 3441.