1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzee Yusuf na muziki wa Taarabu

Christopher Buke2 Septemba 2007

Alianza akiwa mwimbaji wa kawaida sasa hivi anamiliki Jahazi.

https://p.dw.com/p/CHjT
Penzi likiwepo mambo hujionyesha
Penzi likiwepo mambo hujionyeshaPicha: AP

Mziki wa Taarabu kwa hakika una ushawishi mkubwa katika maeneo ya upwa wa Afrika Mashariki na kiasi fulani Afrika ya kati. Muulize mtu anayetokea maeneo ya Mombassa, maeneo ya uswahilini mjini Bujumbura nk atakwambia.

Mwenyewe katika pita pita yangu pembezoni mwa jiji la Dar es salaam, mintarafu mkoa wa Pwani, huo ndio mziki wa watu. Mtu anapokuwa na sherehe wenyewe lakini wakiita shughuli, bila mziki wa taarabu au rusha roho kama wanavyoliita wao mtu utamwambia nini?

Basi likipigwa lile wamama waliojinakshi kwa mavazi ya hishima, wanazunguka mduara vidole viwili vya mkono mmoja wikinyaunyua kidogo tu gauni alilovalia mwana mama, huku kidole kimoja cha mkono mwingine kikinyanyuliwa juu. Ukiona hivyo jua shughuli inafanyika. Pangine ndio maana wenyewe wakiyaita mambo ya vidole juu.

Basi nkwambie na mimi hupita siku moja moja nkaangalia mambo haya. nilikuja gundua wimbo mmoja ukipigwa sana katika rusha roho nyimgi. Wimbo huu ni ule uliopigwa na Mzee Yusuf, uitwao Najiamini napendwa.

Kusema kweli ukisikia tungo za msanii huyo ama utakubali kuwa amekubuu na ni mkongwe katika utunzi. Na ilivyokuwa anaitwa Mzee Yusuf unaweza udhani ni mzee kweli, kumbe sio. Mzee kwake ni jina na wala sio sifa.

Nilikutana naye katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania Dar es salaam, na mazungumzo yetu yakawa kama ifuatavyo.

SWALI: Sisi tumezoea kwa jina la Mzee Yusuf kama jina la usanii, jina lako kamili unaitwa nani?

JIBU: Ndilo jina langu kamili, Mzee Yusuf. Sasa hivi wananiita Mfalme.

SWALI: Kwa nini sasa wanakuita mfalme badala ya Mzee Yusuf?

JIBU: Hiyo n’kama AKA. Katika ile kupamba-pamba nakshi-nakshi yani. Ndiyo naitwa mfalme sasa, nilikuwa naitwa profesa nkatawazwa rasmi sasa namiliki jahazi sa n’nayo hadhi ya kuitwa mfalme.

SWALI: Sasa turudi upande wa historia yako, labda tueleze ulizaliwa lini ukakulia wapi, maisha yako kwa ujumla.

JIBU: Nimezaliwa miaka 30 iliyopita na nimezaliwa Zanzibar. Nimelelewa kulekule nimekulia kulekule na kazi zangu nilianza kule kule za usanii, na nimemaliza darasa la 10 Zanzibar katika shule ya Aile Seasie.

Sikuwa nataka tena kuendelea na shule sababu niliona hali ngumu, si unajua maisha? nkaona hata! Hii ndio itanipeleka hii, sa niache huku. Niache moja nikamate moja.

Kwa hiyo niliacha shule, sikuendelea darasa la kumi na moja. Nikaanza mziki. Nilikuwa nafanya mziki nafanya maigizo, niko na shule, sa ilifika pahali sa nikachukuliwa na bendi ya melody.

Sa nkaona kidogo hapa kuna maslahi japo nilikuwa ‘napigwa buku kwa siku’ (nalipwa shilingi elfu moja kwa siku), lakini nilikuwa nashukuru sababu nilikuwa siipati ile buku,

SWALI: Sasa umeingia katika mziki wa taarabu. Ni muziki ambao kwa kweli unapendwa. Wengi wakisema mziki wa mwambao, wengine hivi, alimradi kila mtu na lugha yake anavyouita mziki huu. Ulipata ushawishi gani mpaka ukaingia katika ulimwengu huu wa mziki wa taarabu?

JIBU: Kwa kweli labda unajua kwa nilipokuwepo taarabu ndio ilikuwa inapendwa na nilikuwa na uwezo wa kuimba taarabu si vingine.

Na sikutegemea kama mtakuwa labda nami naweza kutunga nini mm’kh! Nilikuwa nahisi naweza kuimba. Sababu hata tulikuwa tunakaa nyumbani, tulikuwa tunamsikiliza mother (mama) anaimba, anaimba taarabu, tunakaa naye anatufahamisha hii inaimbwa hivi, hii ndio hivi, hii ndio hivi.

Sa ikafika mahali yani ile muziki ukawa unanijaa. Unanijaa sana kiasi ikafika mahala kwenye mazoezi ya mpira nawaambia wenzangu mimi ntakuwa naimba taarabu.

Basi kwa sababu nilikuwa napenda, halafu ni kwamba uwezo nilikuwa nao. Pale ndo nilipokuwa na ilo nivutia, lakini sio kuwa nilifikiria labda kumuona mtu mmmhkh! Sababu nilikuwa naweza.

Halafu mama yangu mzazi mwimbaji wa taarabu.

SWALI: Anaitwa nani?

JIBU: Anaitwa Mwanajuma Mzee.

SWALI: Ye anaimbia kikundi gani?

JIBU: Alikuwa anaimbia Culture. Ye ameacha sasa. Ametuachia sisi.

SWALI: Mpaka sasa hivi una nyimbo ngapi ambazo umetunga?

JIBU: Aah! yani naweza kusema kwa kukisia tu nyimbo zinafika hata 30. nilizotunga mwenyewe mashairi na music kila kitu nilotunga mwenyewe na kuimba zinafika 6, au 7.

Na Zote nashukuru nyingi zimekamata chati kama Ntadumu naye, Nikipendacho roho, Lawachoma, Najiamini, hizo nimekamata vizuri na Najua kupenda, kuna wimbo unaitwa Wanitazama, Nimekupokea,

SWALI: Sasa ukirejea katika zote zile wimbo gani ambao binafsi ukiwa umekaa pembeni hivi ukausikiliza hata wewe mwenyewe unajihisi kunyanyuka kidogo kwenye kiti?

JIBU: Unajua kwa mimi kila siku nikikaa nafikiria kwamba nitoe bora zaidi ya ile. Sasa nikisema ni ipi, sasa hivi najiamini ndio naona iko juu, na nimetengeneza nyingine inaitwa two in one.

Na vile vile nimetengeneza nyimbo nyinginne ya mapenzi lakini sijaingia studio. Sasa hii naihisi inachukua chati, kwa sababu naipiga tu katika kumbi, naipiga watu wanaipokea vizuri.

Na ile najiamini ile! Ile yani ile nyimbo ile najiamini! Imenipa power (uwezo) sana, na kiasi kwamba yani nahisi hasa najiamini napenndwa. Napendwa vipi? nimezungumza najiamini. Na kitu gani? maana nimezungumza najiamini.

Najiamini labda na uwezo, niliopewa na MUNGU. najiamini nikipenda mtu namridhia labda awe mpuuzi, najiamini niliyekuwa naye vile vile ananipenda, sasa katulia. Hanirushi roho. Sasa vitu vingi nazungumza katika najiamini. Sana lakini nimegusia katika mapenzi sana.

SWALI: Sasa unajua kwa mfano katika au upande wa muziki wao wana sababu na hekaya zao kwa nini hutunga nyimbo. Sijui sana upande wa taarabu, lakini hebu labda wewe umetunga, umeimba. Wimbo huu kama ulivyosema unagusa hisia za wengi. Kitu gani hasa kilikutuma kutunga wimbo huu?

JIBU: Unajua mimi sijapata matatizo au pia naweza kusema nimepata matatizo. Matatizo niliyoyapata ndiyo yamenifanya niimbe hivi kama mwanaume.

Mwanaume unatakiwa nini? Kujiamini. Nitunge nyimbo najiamini.

SWALI: Matatizo ya kimapenzi matatizo ya nini?

JIBU: Matatizo ya kimapenzi unajua mtu ukichukuliwa mpenzi wako halafu mwenyewe uko unajua sasa ni vitu matatizo.

Sasa nikafikiria kwamba huyu hanifai kwa sababu yeye si mwaminifu kwangu, kwa hiyo huyu nilokuwa naye sasa, nahisi yeye ni mwaminifu kwa hiyo vipi nita fanya hivi, huyu najiamini kwamba kweli ananipenda.

SWALI: Manake imefika kwamba sasa anakupangusa hata yale machozi uliyokuwa nayo?

JIBU: Eeh! yani nimezungumza mle, kwamba yote niliyotendwa nishayasahau, yote nshayasahau. Kwa hiyo nimetulia kabisa. Kwamba najiamini kwamba napendwa. Na MUNGU atatulindia hilo penzi letu.

SWALI: Na halafu kuna neno umegusa pale, manake kuna maneno mengine katika utunzi yanakuwa si dhahiri, sana unasema anakula nyama ya kasa tafsiri yake ni nini ? au nini maana ya nyama ya kasa?

JIBU: Kasa ni mnyama. Ni samaki sijui niseme? Yuko baharini na alikuwa analiwa. Sisi kwetu tunakula nyama ya kasa. Na walifika pahali wazungu wakawapiga sindano wale, ili walikuwa wanaliwa sana wale, sasa na yule kasa anatabia kwamba akitaka kucheza ngoma, anacheza ndani kwa ndani. Huwezi kujua anajitikisa mle ndani. Kwa hiyo ndio nikasema nakula nyama ya kasa.

Ndani kwa ndani ajitikisia. Yani inatikisika kwa ndani. Huwezi kuona we nje. Ni tofauti huna, yani ujanja yani kusema utamuona kasa anacheza ngoma. Kwa hiyo nikasema ninakula nyama ya kasa. Nyama ya kasa kuiona tabu. Haiuzwi kwenye mabucha, kwa hiyo nakula nyama ya kasa ya siri kabisa ya ndani.

SWALI: Manake unakula kitu cha peke yako ambacho a ghali watu wengine si rahisi kukipata?

JIBU: Si ndio maana nkasema najiamini, kwa sababu kasa gamba lake utamuua atakufa, kwa hiyo hata umtoe kasa ndani mle tabu, kwa hiyo wangu ni kasa yule.

Kwa hiyo nakula nyama ya kasa ambayo ni ghali. Ikipatikana bei yake ni kubwa. mpaka imetiwa sumu ili wasile watu. Vitongoji Pemba wengi walikufa wengi sana watu miaka fulani, kwa sababu walikula nyama ya kasa.

SWALI: Ndio sasa turejee upande wa utunzi. mtunzi wa muziki wa taarabu, kwa mfano kama hao wanaoinukia, labda wewe kama unamshauri, ni vitu gani azingatie hasa anapokuwa anakusudia kuwa anaenda kutunga mziki wa taarabu?

JIBU: Mziki wa taarabu unajua mpana sana. Halafu sasa huu tunaotunga sasa uko wazi. Zamani kidogo unafumba eeh!

Utasema bunduki isiyorisasi sijui itapigaje? nini huwezi kuelewa. Lakini kwa sasa hivi ukitaka kutunga lazima utunge kitu kinakwenda moja kwa moja kwa mtu “ langu jicho sinyanyui mdomo wangu” si lazima umtukane tu mwenzio “ we uso wako uko hivi” akha.

Mi nyimbo zangu napenda kutunga nyimbo ambazo zinagusa jamii. Nimetunga wimbo, undugu hazina yetu mi na mdogo wangu.

Kwamba kuwaambia ndugu, watu waliogombana, kugombania mali sijui hawaelewani nimezungumza. Kwa hiyo ili kutunga taarabu unatakiwa ile subject kama mfano, unataka kusema “chuki nichukie roho yangu niachie” sasa uizungumze sasa anakuchukia kwa vipi?

Hizo chuki zake zikoje? namna hii namna hii. Na je chuki ni dawa ya husda? Dawa ya kuziba rizki? Sio dawa ya kuziba rizki! Kwa hiyo namwambia chuki sio ngao ya kuzibia rizki.

Na kunifanyia mwao, haitanipata mihilaki hazitanipata mihilaki. MUNGU kaweka mgao, wa maelfu na malaki. Huwapa awapao, hiyo ndiyo kazi yake Maliki. Bure yani, chuma hugeuzi mbao, shuka haiwi kaniki.

Umeona eeh? Kwa hiyo ukitizama, shuka wewe unaweza ukaifanya iwe kaniki? Sasa huwezi! Mbao chuma utakigeuza kiwe mbao? Hayo ndio mambo MUNGU kesha weka hivi. Hiki chuma hiki chuma hii mbao hii mbao.

Kwa hiyo nasema, ukuu-kuu wa chuma, sio upya wa boriti. Chuma hata kiwe cha zamani sio, na boriti uiweke mpya, itakufa lakini chuma kipo pale pale.

SWALI: Na hapa unanirejesha kwa wazo la.... kumekuwa na mawazo tofauti, kuna hiki kinaitwa taarabu za mipasho, na kuna ile nyingine wengine wanasema asilia, lakini baadhi wanakosoa kwamba hizi nyingine zinakuwa na matusi sana lakini nyingine zinakuwa hazina matusi sana, labda sijui wewe hilo unalitizamana kwa mtizamo gani?

JIBU: Mimi kwanza sina nyimbo niliyotunga labda mumeo hivi mke wako hivi sina. Nyimbo yangu mapenzi maisha MUNGU basi.

SWALI: Kwa hiyo na wewe huungi mkono haya mambo ya kutukanana katika taarabu nini wanaita mipasho?

JIBU: Mimi siungi mkono kwa sababu gani? nimetunga ‘mkuki kwa nguruwe’ kumwambia mtu kwamba shida, dhiki, mitihani, humfika kila mtu aliyeumbwa duniani, kukwepa hatothubutu. Huna njia ya kumkwepa MUNGU. Huna.

Kwa hiyo ile nyimbo haijasema chochote na iko kwenye chati. Nimetunga nyimbo ‘two in one’, ya kumzungumza mtu mwema na mnafiki. Kwa sababu gani? Anagombanisha huyu, anajidai kumpatanisha huyu, akitaka kufanya hivi ataharibu hapa atatengenza huku, atajidai kufanya njia hii, atageuzia huku, atafanya hivi. Umeona? Nimemzungumza hiyo wanaipenda.

Kuna nyimbo inaitwa ‘maneno ya mkosaji’ maana kuna mtu kamuacha mpenzi wake halafu anasema sema ovyo, yule hivi

Namwambia maneno ya mkosaji hayanikoseshi raha ya kunywa maji. Kama wewe ulisusa, mwenzio anakula, sasa kitu gani? sasa unataka kusema sema maneno? kwa hiyo, hiyo na watu wanaipenda. Haina mipasho haina nini.

Kuna wimbo nimetunga vile vile unaitwa ‘hayanifiki’. Nazungumza kwamba hayanifiki mambo mnayotaka nyinyi watu yanifike mimi. Hayanifiki kwa sababu gani? kwa nguvu za MUNGU. Kama nyinyi ni MUNGU, basi yatanifika.

Lakini najua namtegemea MUNGU, na watu wanaipenda. Sina nyimbo hata moja, iliyosema “mume wako hivi mke wako hivi, nimemchukua humpati tena” na labda nikazungumza matusi mazito.

Ukizungumza hivi ni vitu vya kawaida, sa ukisema moja kwa moja tusi, “uso wako kama futi uso wako kama mbwa” hakuna anayeweza kumuumba mwenziwe na pia anayeweza kumuumbua.

Anaweza kumuumbua labda akampiga kisu lakini hawezi labda akamrudisha hali yake. Kwa hiyo anayeweza ni MUNGU tu.

Sa vitu hivyo mimi bado na vinakubalika na ndivyo vilivyonipa hili jina hili leo. Mi sijatunga nyimbo ya mpasho. Sijatunga! Natunga nyimbo zangu ‘sichagui sibagui atayenizika simjui’.

‘Sina kinyongo na mtu’ ‘langu jicho sinyanyui mdomo wangu’, ‘nia njema ni tabibu nia mbaya huharibu’. Nimetunga vitu ambavyo kila mtu akisikia tu kinamgusa.

SWALI: Sasa zamani ukiimba na zanzibar taarabu kwa nini ukatoka kule?

JIBU: Unajua kuna maradhi unatamani yaishe katika mwili. Unajua maradhi mabaya we unaweza ukayafikiria ni yapi? Manake yanaweza kukuua haraka haraka?

Sasa mimi naweza kusema pumu maradhi mabaya sana, lakini ni maradhi ambayo simple (rahisi kupona). sababu ukiwa na dawa yake yaani uki meza umepona tofauti na malaria.

Malaria hata anywe dawa leo mpaka wikiiiii! Ndo dozi yake inamalizika

Sasa ile ilikuwa kama pumu na dawa yake ni kutoka. Niondoke Zanzibars stars nitafute changu. Kwa sababu kwanza walikuwa wananitegemea. Wananifanyisha kazi. Nimekuwa punda! nafanya kazi lakini hawanilishi vizuri, kama mtu. Halafu kwa nini tulikuwa hatuelewani?

Mimi nataka hivi jamani mwendo huu huu nahisi huu unakuwa mzuri, kwa nini tusiende huu? wenzangu wanaona wao ni huu. Kwanza walikuwa wananiita mtoto.

Hili neno lilikuwa linaniuma sana. “ huyu mtoto Bwana mambo ya kitoto, mzee mropokaji” lakini basi lile neno linaniuma sana. Kwa nini aniambie mimi mtoto? Wakati mimi nina watoto wengine watatu? Watoto wangu mimi halafu mimi niitwe mtoto?.

Mtoto kwa baba yangu na mama yangu, si kwa kijana mwenzangu! Hii roho ilikuwa inaniuma sana. Lakini yote ilikuwa kwamba nafikiria kwamba je ntatokaje? Nami ntakuwa na kitu changu? Na hayo mawazo pia nilikuwa nayo.

Kwa hiyo nikafikiria kwamba sasa nguvu ninazo wacha nifanye. Si kwa namna nyingine yoyote lakini nimehisi hii ndio sasa itanisaidia. Ya kutokuitwa mtoto.

SWALI: Na ndipo sasa ukaanzisha jahazi?

JIBU: Jahazi modern taarabu! Na sasa hivi linaelea vizuri tu. Kwa nakshi nakshi.

SWALI: Sasa kwa hapa ulipofika hebu nitajie matatizo unayokabiliana nayo, manake unakuta katika ulimwengu kuna matatizo, kuna raha kuna nini kwa upande labda wa matatizo, ni kitu gani ambacho unadhani kwamba labda kinakusumbua?

JIBU: Kinachonisumbua labda ni fitina. Kufanyiwa fitna. Mtu unafikia unaachishwa ukumbi, mtu unafanyiwa vituko ndani ya ukumbi, kwa hiyo zote hizo ni fitna. Sasa zile ndizo zinazonisumbua mimi.

Lakini kwa upande mwingine bado sijakutana na matatizo sababu mimi si mtu ambaye labda najisikia. Napenda watu. Sasa yale matatizo mengine ni ya kawaida.

Lakini haya ya fitina haya, haya yananitia wasi wasi. Yananitia wasiwasi sana.

Mwisho.