Myanmar yawasilsha ripoti yake ya Rohingya katika mahakama ya ICJ | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.05.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Myanmar yawasilsha ripoti yake ya Rohingya katika mahakama ya ICJ

Mahakama ya haki ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa Myanmar imewasilisha ripoti yake ya kwanza katika mahakama hiyo kuhusu hatua ilizozichukua kuzuia mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa jamii ya wachache ya Rohingya .

 

Mahakama hiyo ya kimataifa ICJ, ilitoa agizo la muda mwezi Januari kwamba taifa la Myanmar lenye jamii kubwa ya waumini wa madhehebu ya budhaa lazima lichukuwe hatua zote zilizo ndani ya uwezo wake kukomesha mauaji ya kimbari ya jamii hiyo ya wachache na kwamba lazima iwasilishe ripoti katika mahakama hiyo kila baada ya miezi sita hadi wakati uamuzi wa mwisho utakapotolewa.

Taifa la Gambia lilifungua kesi hiyo dhidi ya Myanmar na ilihusiha kikao mwezi Desemba ambapo kiongozi wa zamani wa kiraia na kinara wa demokrasia Aung San Suu Kyi aliwakilisha Myanmar kwenye kesi hiyo. Gambia iliishtumu Myanmar kwa kukiuka makubaliano ya mwaka 1948 ya mauaji ya kimbari.

Jopo la majaji 17 liliunga mkono kwa kauli moja agizo hilo la muda dhidi ya Myanmar ili kulinda ushahidi wowote wa uhalifu na kuzuia matukio ya ghasia.

Niederlande Den Haag Aung San Suu Kyi vor dem Internationalen Gerichtshof

Aung San Suu Kyi- kiongozi wa kiraia wa Myanmar

Watu milioni moja wa jamii ya Rohingya wanateseka kambini katika nchi jirani ya Bangladesh baada ya ukandamizaji mkubwa uliofanywa na jeshi la Myanmar mwaka 2017 huku jamaa wengine laki sita wa jamii hiyo wakibakia katika jimbo la Rakhine Kusini Magharibi mwa Myanmar. Hata hivyo maafisa wakuu wa mahakama hiyo wameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba yaliyomo kwenye ripoti hiyo ya Myanmar ambapo nakala inapaswa kupelekwa nchini Gambia yatasalia kuwa siri hadi wakati majaji wake watakapoamua kuyatoa hadharani.

Makundi ya wanaharakati wa kutetea jamii hiyo ya Rohingya hata hivyo yamesema kuwa Myanmar haijachukuwa ''hatua zozote za maana'' kuimarisha hali katika jimbo la Rakhine tangu uamuzi wa mahakama hiyo ya kimataifa ya haki ya Umoja wa Mataifa wa mwezi Januari. Kwa mujibu wa rais wa jumuiya ya Warohingya wa Myanmar yenye makao yake nchini Uingereza Tun Khin, mauaji ya kimbari bado yanaendelea bila kupingwa nchini Myanmar na kwamba wanawake na watoto wanaendelea kuteseka katika jimbo la Rakhine.

Tun Khin aliiihimiza mahakama hiyo kutoa ripoti hiyo hadharani haraka iwezekanavyo na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa ''kuimarisha shinikizo dhidi ya Myanmar'' kuzingatia hatua hizo za muda za mahakama hiyo. Katika uamuzi usiokuwa wa kawaida mapema mwaka huu, mahakama hiyo ilikataa hoja za mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Suu Kyi kwamba ukubwa wa uhalifu dhidi ya jamii ya Rohingya huenda ulitiwa chumvi  na kwamba yalikuwa ni masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Mahakama hiyo iliruhusu ombi la Gambia la hatua za dharura ikisubiriwa kuanzishwa kwa kesi kamili ambayo huenda ikachukuwa miaka na kusema kwamba jamii ya Rohingya nchini Myanmar ''insalia kuwa katika hatari kubwa.''