1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi 18 ya waasi yanatarajiwa kushiriki mazungumzo hayo

Mjahida31 Agosti 2016

Mazungumzo ya amani kati ya serikali mpya ya Myanmar na makundi mengi ya waasi nchini humo, yanatarajiwa kuanza wiki hii yakiwa na lengo la kumaliza mapigano ya muda mrefu ya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/1JtD8
Waziri wa nchi za nje Myanmar Aung San Suu Kyi
Waziri wa nchi za nje Myanmar Aung San Suu KyiPicha: Reuters/S.Z. Tun

Serikali mpya ya Myanmar inayoongozwa na Aung San Suu Kyi, wiki hii inatarajiwa kukaa chini na waasi katika mkutano mkubwa wa amani, miezi kadhaa baada ya kuchukua madaraka kufuatia uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo baada ya miongo kadhaa.

"Hata kama hakuna kikubwa kinachotarajiwa kutoka katika mkutano huo, ni mazungumzo ya amani ya kihistoria katika nchi yetu," Naing Hantha, Naibu mwenyekiti wa baraza la shirikisho la Umoja wa Kitaifa (UNFC), linalobeba makundi mengine 11 ya kikabila nchini humo.

Mazungumzo hayo yanaashiria mwanzo mzuri wa kujaribu kumaliza moja ya mapigano marefu ya wenyewe kwa wenyewe duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anatarajiwa kufungua rasmi mkutano huo wa siku nne utakaoanza siku ya Jumatano wiki ijayo katika mji mkuu Naypyitaw.

Jenerali wa jeshi la Myanmar Aung Hlaing
Jenerali wa jeshi la Myanmar Aung HlaingPicha: Getty Images/AFP/R. Gacad

Mkutano huo utahudhuriwa na makundi ya waasi 18 kati ya 21 yanayopigania uhuru zaidi wa kujitawala. Suu Kyi ameyafanya masuala ya amani na maridhiano kuwa kipa umbele katika serikali yake iliyochukua madaraka mwezi Machi kufuatia uchaguzi uliyofanyika mwezi Novemba.

Suu Kyi aomba msaada wa China katika mazungumzo hayo

Licha ya China kuunga mkono utawala wa kijeshi iliyomshikilia au kumuweka katika kizuizi cha nyumbani kwa miaka 15, Suu Kyi pia amomba uungwaji mkono kutoka Beijing katika mazungumzo hayo ya amani . Kyi aliomba msaada huo alipokuwa katika ziara muhimu ya kidiplomasia mjini humo mapema mwezi huu. Awali China iliwahi kufadhili baadhi ya makundi ya kikabila ya waasi nchini Myanmmar.

Hata hivyo mkutano huu unafanyika baada ya kuwepo mkutano mdogo wa amani Mwezi Januari na makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliyotiwa saini mwezi Oktoba kati ya serikali na makundi yapatao nane ya waasi. Makubaliano hayo yalipewa jina la "Panglong ya Karne ya 21" baada ya mpango wa mwaka 1947 kati ya Uingereza na kiongozi wa Burma jenerali Aung San, ambaye ni babaake Suu Kyi.

Suu Kyi akitoa hotuba katika mkutano wa amani
Suu Kyi akitoa hotuba katika mkutano wa amaniPicha: Getty Images/AFP/R. Gacad

Mpango huo wa Panglong ulinuwia kutoa uhuru zaidi wa kujitawala kwa makundi makuu ya kikabila katika maeneo ya Shan, Kachin na Chin uchini ya serikali ya shirikisho kutoka kwama 1948 wakati nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza.

Lakini baada ya kuuwawa kwa jenerali Aung Sang muda mfupi kabla ya Uhuru, nchi hiyo haraka ikaingia katika mgogoro wa kisiasa na jeshi likachukua madaraka mwaka 1962. Hata hivyo serikali awali ilikuwa imesema kwamba makundi yote ya waasi pamoja na makundi ambayo yalikataa kutia saini makubaliano ya kusitisha mapigano ya Oktoba wataalikwa kuhudhuria mazungumzo ya sasa.

Lakini Hla Maung Shwe mpatanishi katika shirika linalofungamana na serikali la amani na mshikamano wa kitaifa ameliambia shirika la habari la dpa kuwa makundi matatu ambayo bado yapo katika mapigano hayatahudhuria mazungumzo hayo kwasababu za kukataa kuweka chini silaha zao.

Taarifa iliyotolewa Agosti 18 kutoka kwa jeshi la kitaifa la ukombozi la Ta'ang, jeshi la Arakan na Jeshi la Myanmar ilisema kwamba wana nia ya kumaliza mgogoro uliyopo.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters

Mhariri:Iddi Ssessanga