Mwenendo upya wa ugaidi? | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 12.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mwenendo upya wa ugaidi?

Baada ya mashambulio ya mabomu mjini Algiers, Algerien, viongozi wa kutoka duniani kote wameyalaani mashambulio haya. Jana usiku kunda la kigaidi la Al Qaida katika eneo la Kiislamu la Maghreb, yaani Afrika ya Kaskazini, limechukua dhamana ya mashambulio ambayo yamewaua watu 24 na kuwajeruhi wengine wasiopungua 222.

Mlipuko wa bomu mjini Algiers

Mlipuko wa bomu mjini Algiers

Yalikuwa mashambulio mabaya zaidi kutokea nchini Algeria tangu miaka kadhaa iliyopita. Watu wawili waliojitolea muhanga walitumia mabomu yaliyowekwa ndani ya magari. Mmoja alililipua bomu akiwa mbele ya jengo la serikali mjini Algiers ambapo iko ofisi ya waziri mkuu Abdelaziz Belkhadem na vilevile wizara ya mambo ya ndani ya Algeria. Dakika chache tu baada ya hapo, bomu la pili lililipuliwa Magharibi katika mji wa Algiers karibu na kituo cha polisi.

Ripoti nyingine ambazo hazijathibitishwa na idara za serikali zinasema mabomu mengine mawili yaligunduliwa ambayo lakini hayakulipuka, moja likiwa katika mtaa ziliko balozi nyingi za kigeni, na la pili karibu na idara ya usalama wa taifa.

Katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya Al-Arabiya, waziri mkuu Abdelaziz Belkhadem alisema lengo la mashambulio hayo ni kuchokoza muda mfupi kabla ya uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 17 Mei. Belkhadem aliongeza kuwa uchaguzi utaendelea kama ulivyopangwa.

Kundi lililochukua dhamana ya mashambulio hayo ni lile la Al-Qaida katika eneo la kiislamu la Maghreb wakati lilipozungumza kwa njia ya simu na televisheni ya Al-Jazeera. Kundi hilo ni muugano wa makundi kadhaa ya kigaidi katika eneo la Afrika Kaskazini. Mwanzoni mwa wiki hii, watu watano waliuawa katika mashambulio ya watu waliojitoa muhanga mjini Casablanca katika nchi jirani ya Marokko.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya ugaidi, kundi la Al-Qaida linajaribu kujitanua katika eneo la Maghreb, kama anavyosema Mfaransa Benjamin Stora: “Kuna aina mpya ya upinzani wa kisiasa na kijamii katika tabaka na vizazi vipya katika eneo la Maghreb, hasa katika miji mikubwa ya Marokko na Algeria. Lakini tusisahau Tunesia ambao mwishoni mwa mwaka 2006 kulitokea mashambulio kadhaa ya kigaidi karibu na Tunis na jeshi la Tunesia kuhusishwa katika mapigano katika mitaa ya Tunis.”

Wadadisi wa mambo wanasema huenda huo ni mwanzo tu wa mwenendo upya wa ugaidi katika eneo hilo.

Viongozi wa mataifa mengi duniani pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, walilaani mashambulio hayo ya kigaidi. Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bi Marie Okabe, katibu mkuu Ban anaamini tukio hili ambalo linafuatia mashambulio mengine katika enea la Maghreb linaonyesha haja ya kuchukua hatua za pomoja dhidi ya ugaidi. Serikali za Marekani, nchi za Umoja wa Ulaya, Urusi, Canada na nyingine zilieleza masikitiko na shutuma zao.

Katika eneo la Mashariki ya Kati, katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu, Amr Mussa, alilaani mashambulio hayo. Msemaji wa wizara ya nchi za nje ya Iran pia alilaumu mashambulio haya ya Algeria akisema hayaendi sambamba na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Mfalme wa Jordan, Abdullah II, alisema ni mashambulio ya woga ambayo hayana uhusiano wowote na Uislamu.

 • Tarehe 12.04.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4m
 • Tarehe 12.04.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4m
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com