1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamke wa kwanza kuteuliwa askofu wa Kianglikana Kenya

Musa Naviye13 Septemba 2021

Kanisa la Kianglikana nchini Kenya limeandika historia kwa kumteua mwanamke wa kwanza kuwa Askofu anaesimamia dayosisi, uteuzi ambao umeibua hisia mseto hasaa miongoni mwa viongozi mbali mbali wa kike. 

https://p.dw.com/p/40FZB
Kenia All Saints Cathedral in Nairobi
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Akionekana mkakamavu, Rose Okeno mwenye umri wa miaka 52 alisimama na bibilia kwenye mkono wake wa kulia kula kiapo cha uteuzi wa kuwa askofu wa kwanza wa kike wa kanisa la Kianglikana nchini Kenya kwenye sherehe iliyoandaliwa katika kanisa la Kiangalikana la Butere - jimboni Kakamega.

Moja kwa moja katika hotuba yake, askofu Okeno amesema atatumia nafasi yake kuangazia maslahi ya watoto wa kike, wanawake na wasiojiweza katika jamii.

"Tutaangazia maswala ya haki za watoto wa kike...," amesema Rose Okeno.

Uteuzi wa Okeno umeibua hisia mseto miongoni mwa waumini wa dini ya Kikristo wengi wakipongeza hatua ya kanisa hilo kumteua mwanamke ila wapo waliokuwa na kauli tofauti licha ya kuuunga mkono uteuzi huo hili likichangiwa na msimamo wa dini katika swala la uongozi wa wanawake kwenye kanisa.

"Ningependa kutoa pongezi zangu kwa uteuzi wa askofu ..., " amesema mmoja wa waumini.

Uteuzi wake Okeno umeonekana kupiga msasa nafasi ya mwanamke katika maswala ya uongozi nchini, viongozi mbali mbali hasaa wa kisiasa wakijitokeza kutia msisitizo kuwa, kuna haja ya mtoto wa kike kuendelea kuwezeshwa zaidi ili kufikia malengo ya juu maishani.

Okeno ambaye ni mama ya watoto wanne amekuwa akihudumu katika kanisa la Kianglikana kwa kipindi cha miaka 20 katika nafasi mbalimbali kabla ya uteuzi wake.