1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Mwanamapinduzi Thomas Sankara

Bruce Amani
25 Julai 2018

Kiongozi wa mapinduzi nchini Burkina Faso Thomas Sankara anazingatiwa kuwa mmoja wa vigogo wa kisiasa barani Afrika wa karne ya 20, pamoja na Patrice Lumumba na Nelson Mandela

https://p.dw.com/p/2sgsh

Thomas Sankara - mwanamapinduzi mashuhuri

Kiongozi wa mapinduzi Thomas Sankara anazingatiwa kuwa mmoja wa vigogo wa kisiasa barani Afrika wa karne ya 20, pamoja na Patrice Lumumba na Nelson Mandela. “Che Guevara wa Afrika”, aliyetambuliwa na wafuasi wake kuwa kiongozi mwenye maono, aliongoza mapinduzi ya Agosti 4, 1983 katika iliyokuwa Upper Volta. Ushawishi wa mawazo ya Sankara bado unadumu mpaka sasa, licha ya kwamba aliuliwa mnamo Oktoba 15, 1987.

Maisha ya Thomas Sankara

Kapteni Thomas Sankara, aliezaliwa mwaka 1949, alichukua madaraka wakati wa mapinduzi ya Agosti 4 1983. Akiwa na mshirika wake jeshini, akaipa Upper Volta, kama ilivyoitwa na mkoloni wake Ufaransa, jina la Jamhuri ya Kidemokrasia na Maarufu ya Burkina Faso, ambalo lina maana “nchi ya watu waaminifu”. Akatolewa madarakani na mmoja wa marafiki zake, Blaise Compaoré, kisha akauliwa mnamo October 15, 1987 pamoja na wenzake 12.

DW Videostill Projekt African Roots | Thomas Sankara, Burkina Faso
Picha: Comic Republic

Nini ambacho Thomas Sankara anajulikana kwa kukifanya? 

Kwa kujaribu kuibadilisha nchi yake ya Afrika Magharibi kuwa maabara ya kilimo ili kuwa na uwezo mkubwa wa kujitosheleza kwa chakula. Wakati wa enzi yake, alipigia debe bidhaa zilizotengenezwa nchini Burkina na akajaribu kuimarisha uzalishaji na utumiaji bidhaa za ndani ya nchi. Rais huyo wa Burkina alitaka kuimarisha mfumo wa afya na elimu katika nchi ambayo ilikuwa moja ya maskini zaidi duniani. Alikuwa na maisha ya wastani yeye mwenyewe. Uhuru wa wanawake pia ulikuwa mojawapo ya mambo aliyoyapata kipaumbele

Nini ambacho Thomas Sankara anakosolewa kwa kukifanya? 

Mahusiano yake na kanali Gaddafi wa Libya, lakini pia kwa kuvuruga utaratibu uliowekwa. Katika mwaka wa 1985, mgogoro ulizuka hata na Mali kuhusu mpaka kati ya nchi hizo mbili.

Nini kilikuwa chanzo cha msukumo: katika hotuba ya kihistoria iliyotolewa Julai 1987 katika Umoja wa nchi huru za Afrika – OAU mjini Addis Abeba, rais huyo wa Burkina Faso alizikemea taasisi za Bretton Woods, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, ambazo kulingana naye zilirithiwa kutokana na ukoloni.

Karibu miongo mitatu baada ya mauaji yake, kapteni huyo bado alionekana kuwa shujaa na watu ambao waliuangusha utawala wa Blaise Compaoré mnamo Oktoba 2014. Watu wengi wanamtambuwa kuwa shujaa wa vijana wa Afrika. Mradi wa kuweka kumbukumbu yake unaendelea mjini Ouagadougou.

Asili ya Afrika: Thomas Sankara

Nini baadhi ya dondoo za Thomas Sankara? 

“Asili ya Madeni hutoka kwa asili ya ukoloni”. Wale wanaotukopesha fedha ni wale waliotutawala hapo kabla. Ni wale ambao walikuwa wakisimamia uchumi wetu. Wakoloni ni wale walioifanya Afrika kuwa na madeni kupitia ndugu zao ambao ndio walikuwa wakopeshaji. Hatukuwa na mahusiano na madeni hayo. Hivyo hatuwezi kuyalipa”.

“Mimi sio masihi wala nabii. Mimi sina ukweli. Ndoto yangu pekee ni matarajio mawili: kwanza kuweza kuzungumza katika lugha rahisi, yenye maneno yanayosikika na ya wazi, kwa niaba ya watu wangu, watu wa Burkina Faso; pili kuweza pia kuwa sauti ya watu wasio na sauti ulimwenguni, wale ambao wanaoishi tu ulimwenguni na kukwama katika Ulimwengu wa Tatu. Na kusema, ijapokuwa huenda nisifaulu katika kuwafanya waeleweke, sababu za uasi yetu. 

“tungependa kuwa warithi wa mapinduzi yote ya ulimwengu, wa mapambano yote ya uhuru wa watu wa nchi za Ulimwengu wa Tatu”

Utata juu ya kifo chake: Ukweli kamili haujabainika kuhusu mazingira na wale waliohusika kwa kifo chake wakati wa mapinduzi ya mwaka wa 1987. Mjane wake Mariam Sankara bado anatafuta haki. Vipimo vya vinasaba – DNA vilifanywa kwa mabaki yanayodaiwa kuwa ya kiongozi huyo wa Burkina, lakini havikuwa kamilifu. Waranti wa kimataifa wa kukakamatwa umetolewa dhidi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Blaise Compaoré, anayeishi sasa uhamishoni. Kuna miito mingi kwa Ufaransa kutoa ruhusa ya kuchunguzwa nyaraka zake za zamani kuona kama koloni hilo la zamani lilihusika na kifo cha “Che Guevara wa Afrika”.

 

Claire-Marie Kostmann, Richard Tiéné, Gwendolin Hilse na Philipp Sandner  wamechangia katika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.