1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanaharakati wa Belarus apatikana amekufa Ukraine

Josephat Charo
4 Agosti 2021

Mwanaharakati wa Belarus Vitaly Shishov amepatikana akiwa ananing'inia kwenye mti kwenye bustani iliyo karibu na eneo alikokuwa akiishi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/3yVaX
Belarus | Aktivist | Vitaly Shishov
Picha: instagram.com/vvshishov

Shishov, aliyekuwa na umri wa miaka 26, aliiongoza asasi isiyo ya kiserikali ya Belarussian House -Nyumba ya Belarus - nchini Ukraine, inayojihusisha na kazi ya kuwasaidia Wabelarus wanaokimbia ukandamizaji kupata makazi Ukraine na kuandaa maandamano ya kuupinga utawala wa mjini Minsk.

Shishov alitoka nyumbani kufanya mazoezi ya kukimbia siku ya Jumatatu asubuhi lakini hakurejea na hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi. Polisi ya Ukraine imethibitisha katika taarifa kuhusu kupatikana kwa Shishov akiwa amekufa.

Polisi imesema inachunguza uwezekano wa Shishov kujinyonga au kama aliuliwa lakini wauaji wakamtundika mtini ionekane kana kwamba alijinyonga. Mkuu wa jeshi la polisi nchini Ukraine Ihor Klymenko amewaambia waandishi habari mjini Kiev kwamba Shishov alipatikana amechubuka kwenye pua na goti lake lakini ni mapema kubaini ikiwa alishambuliwa.

"Tumeanzisha uchunguzi wa uhalifu kama inavyoelekezwa katika ibara ya 115 sehemu ya kwanza ya sheria ya uhalifu ya Ukraine kuhusu mauaji. Kwa sasa tunafanya uchunguzi mbalimbali kubaini taarifa zote za kifo cha muhanga. Wachunguzi wanachunguza uwezekano wa kujinyonga au ikiwa aliuliwa, na wauaji wanataka ionekane alijiua mwenyewe."

Mpenzi wa Shishov, raia wa Belarus, Bazhena Zholudz, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba haamini Shishov angeweza kujiua mwenyewe.

Asasi aliyokuwa akiifanyia kazi Shishov House of Ukraine, pia imesema alikuwa akifuatiliwa na watu wasiofahamika katika siku chache zilizopita. Mkuu wa shirika hilo mjini Warsaw nchini Poland, Ales Zarembiuk, ameliambia shirika la habari la Ufaransa ana uhakika asilimia 100 kuwa Shishov aliuliwa katika jitihada ya kuwatisha Wabelarus wanaoishi nje ya nchi, ambao mashirika yao yanaunga mkono maandamano ya mwaka uliopita.

Sviatlana Tsikhanouskaya ahofia maisha yake

Kiongozi wa upinzani wa Belarus Sviatlana Tsikhanouskaya, amesema angependelea kusubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi kwa sababu anaelewa mazingira ya kifo cha Shishov. Tsikhanouskaya amesema inauma sana wakati watu wasio na hatia wanapotekwa nyara au kuuliwa na mawakala wa utawala.

"Naweza kutoweka wakati wowote. Naelewa hili, lakini nitafanya ninachikifanya. Siwezi kuwacha kwa sababu nahisi nina jukumu hili kwa mustakhbali wa nchi yangu, sawa na wale wanaopigana sasa hivi wanavyohisi jukumu lao. Nafahamu hata nikitoweka siku moja, vuguvugu hili litaendelea bila mimi."

London Treffen Svetlana Tichanowskaja mit  Premierminister Boris Johnson
Sviatlana Tsikhanouskaya, kiongozi wa upinzani wa Belarus akiwa LondonPicha: Peter Nicholls/REUTERS

Akizungumza baada ya kukutana na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson jijini London jana Jumanne, Tsikhanouskaya ametaka kila mtu aliye Belarus na wote wanaoishi nje ya nchi wawe waagalifu kwa sababu utawala wa Belarus hautasita kufanya chochote kuwafikia ukitaka kufanya jambo fulani.

Umoja wa Mataifa na Marekani wametaka maafisa wa Ukraine wafanye uchunguzi wa kina. Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia haki za binadamu, Marta Hurtado, amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba ni wazi hali nchini Belarus inaendelea kuzorota.

Ubalozi wa Mareakni mjini Kiev umesema kifo cha Shishov kimetokea wakati kukiwa na ukandamizaji usiokubalika wa mashirika ya kijamii na umeitaka Ukraine kufanya uchunguzi kamili na wa kina.

Mjini Washington msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Ned Price amerudia tena wito wa kukomesha ukandamizaji Belarus na kuachiwa huru mara moja kwa wafungwa wa kisiasa na kufanyike uchaguzi huru.

Raia takriban 300 wa Belarus wanaoishi nchini Ukraine wameandamana nje ya ubalozi wa Belarus mjini Kiev, wengi wakibeba picha za Vitaly Shishov wakitaka uchunguzi ufanyike kuhusu kifo chake.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anafuatilia kwa karibu kesi hiyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Serhiy Nykyforov. Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ameahidi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba Ukraine itafanya kila linalowezekana kuchunguza kikamilifu kifo cha Shishov.

(afpe, ap)