1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanaharakati aachiwa China

8 Machi 2008
https://p.dw.com/p/DL9Q

BEIJING

Wakili mashuhuri wa haki za binaadamu nchini China Teng Biao ameachiliwa huru leo hii baada ya polisi wasiojulikana kumteka nyara siku mbili zilizopita nje ya nyumba yake mjini Beijing.

Teng ameserma alichukuliwa hapo Alhamisi wakati wa usiku na kutumbukizwa ndani ya gari ambapo alifunikwa uso kwa mfuko na watu ambao hawakumuonyeaha vitambulisho vyoyote vile ila kumwambia kwamba walikuwa wakitoka Ofisi ya Usalama wa Wananchi mjini Beijing.

Wanaharakati wa China na makundi ya kutetea haki za binaadamu ya kimataifa leo hii walilaani kutekwa nyara kwa Teng kuwa ni jambo la kufadhaisha wakati hofu ikiongezeka ya kukandamizwa kwa wapinzani kabla ya kufanyika kwa Michezo ya Olympiki nchini humo.

Polisi walimwambia kwamba alikamatwa kutokana na makala alizoandika kuhusu kulinda haki za raia ikiwa ni pamoja na baruwa ya wazi kwa serikali aliyoandika pamoja na mwanaharakati mwenzake Hu Jia ambaye hivi sasa anasubiri kushtakiwa kwa uchochezi.