Mwaka mmoja watimia tangu kuzama kwa Mv Spice Islander Zanzibar | Matukio ya Afrika | DW | 10.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mwaka mmoja watimia tangu kuzama kwa Mv Spice Islander Zanzibar

Siku kama ya leo, mwaka mmoja uliopita, ilikuwa ni ya msiba mkubwa visiwani Zanzibar baada ya meli ya Spice Islander kuzama mkondoni Nungwi ikitokea Unguja kwenda Pemba na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000.

Juhudi za uokozi zilpokuwa zikiendelea baada ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander. tarehe 9 Septemba 2011.

Juhudi za uokozi zilpokuwa zikiendelea baada ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander. tarehe 9 Septemba 2011.

Kwa mujibu wa taarifa ya ripioti ya Tume ya Kuzama kwa Meli hiyo iliyotolewa mwezi wa Februari, idadi ya maiti zilizopatikana na kuzikwa ni 243, huku watu 941 wakiokolewa wakiwa hai.

Idadi kubwa zaidi hata hivyo, inaaminika ni ya wale waliokuwa hawakupatikana. Mali nyingi pia ilipotea na hadi sasa bado haijawahi kujuilikana hasa thamani kamili ya mali hiyo wala idadi kamili ya wahanga wa Spice Islander, ingawa watu waliotajwa kufa na kupotea hadi sasa ni 1,370.

Msiba huu unatajwa kuwa mkubwa kabisa kwa historia iliyo kwenye rikodi za visiwa hivyo, kwa watu wengi namna hiyo kufa katika mkasa wa baharini.

Mtoto akiwa amejikunyata, mmoja wa manusura wa mkasa wa Mv Spice Islander.

Mtoto akiwa amejikunyata, mmoja wa manusura wa mkasa wa Mv Spice Islander.

Sabri Juma ni miongoni mwa watu waliopoteza watu wao kupitia ajali hiyo. Yeye alimpoteza mke wake, ambaye ndio kwanza walikuwa wamekaa kwa kipindi cha mwaka mmoja tu. Anasema nyumba yake inamzomea kila akiingia ndani, kwani kumbukumbu za mke wake bado zingali naye.

Kufuatia ajali hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuunda Tume ya Uchunguzi wa ajali hiyo, ikiongozwa na Jaji Abdulhakim Ameir Issa.

Pamoja na mengine, Tume hiyo iligundua kwamba upakiaji uliopindukia ndio uliosababisha ajali hiyo, ambao nao ulitokana na kukiukwa kwa kanuni na taratibu kadhaa za usafiri baharini, ikiwemo pia uwekwaji vibaya wa mizigo, matatizo ya kiufundi yaliofanya kiwango cha upakizi kisijulikane, na hata na uzembe wa nahodha.

Waokoaji wakibeba muili wa mmoja wa wahanga wa ajali ya Mv Spice Islander.

Waokoaji wakibeba muili wa mmoja wa wahanga wa ajali ya Mv Spice Islander.

Tume ilisema kuwa licha ya meli kuwa na uwezo wa kupakia abiria 620, usiku wa siku kama leo mwaka jana ilikuwa imepakia abiria 2,470, yaani karibu kidogo ya mara nne zaidi ya uwezo wake.

Katika mapendekezo yake, tume hiyo ilitaka hatua za kisheria na kinidhamu kuchukuliwa kwa baadhi ya waliohusika na pia msaada kwa waliopoteza ndugu, jamaa na mali zao.

Mwaka mmoja baadaye, waziri wa sasa wa miundombinu na mawasiliano wa Zanzibar, Rashid Seif, anasema serikali imejipanga hayo hayatokei tena, ingawa hata miezi miwili haijatimia tangu meli nyengine ya Mv Skagit kuzama ikitokea Dar es Salaam kwenda Unguja na kuua watu zaidi ya 100.

Kwa hakika, hakuna jicho lenye huruma lilijizuia kutoka machozi kwa msiba huu mkubwa kwa Zanzibar. Karibu dunia nzima iliunganika na Wazanzibari katika kipindi kile kigumu. Na katika kuukumbuka huu mwaka mmoja, Deutsche Welle, bado inaungana na ndugu, jamaa na familia zilizokumbwa na msiba huu mzito.

Hapana shaka, Mungu alitoa, na Mungu alitwaa na kwake ndiko kwenye marejeo ya viumbe wote. Lakini pia, kama anavyosema Sabri Juma na kama ilivyogundua tume ya uchunguzi wa ajali hiyo, uzembe wa mkururo wa wahusika hauwezi kutengwa kando kwenye maafa haya makubwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdulrahman

Sauti na Vidio Kuhusu Mada