Mwaka mmoja tangu kukamatwa kwa Gbagbo | Matukio ya Afrika | DW | 11.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mwaka mmoja tangu kukamatwa kwa Gbagbo

Laurent Gbagbo alikamatwa baada ya kipindi kirefu cha mapigano yaliyozuka baada ya kiongozi huyo kukataa kumwachia madaraka Alassane Ouattara aliyeshinda duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka 2010.

Laurent Gbagbo aliyekuwa rais wa Cote D'Ivoire

Laurent Gbagbo aliyekuwa rais wa Cote D'Ivoire

Leo umetimia mwaka mmoja tangu kukamatwa kwa aliyekuwa rais wa Cote D'Ivoire, Laurent Gbagbo. Kukamatwa kwake kulifanyika baada ya kipindi kirefu cha mapigano yaliyozuka baada ya Gbagbo kukataa kumwachia madaraka Allasane Ouattara aliyetambulika kimataifa kama mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka juzi.

Kwa miaka kadhaa sasa, Cote D'Ivoire inaonekana na nchi za Magharibi kama nchi ambayo ni hatari kwa safari za utalii. Hili lilithibitishwa mwaka jana baada ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais kumwingiza madarakani Alasane Ouattara na hivyo kumaliza utawala wa Laurent Gbagbo. Lakini Gbagbo alikataa kung'atuka madarakani na hivyo kwa kipindi fulani, Cote D'Ivoire ilikuwa na marais wawili: Gbagbo na Alasane Outtara aliyetambulika kimataifa kama mshindi wa uchaguzi.

Rais Alassane Ouattara wa Cote D'Ivoire

Rais Alassane Ouattara wa Cote D'Ivoire

Huu ndio ulikuwa mwanzo wa mgogoro uliodumu kwa miezi kadhaa. Mgogoro huo ulisemekana kumalizika rasmi tarehe 11 Aprili mwaka jana, pale ambapo vikosi vitiifu kwa Ouattara, vikisaidiwa na wanajeshi kutoka nje, vilipolivamia handaki la Gbagbo na kumkamata mwanasiasa huyo. Gbagbo alitolewa nje akiwa hajavaa hata shati, bali vesti nyeupe tu.

Zaidi ya watu 3,000 waliuwawa

Mapigano baina ya wafuasi wa Gbagbo na vikosi vya Ouattara yalisababisha vifo vya mamia ya watu na kuwalazimisha maelfu kukimbia makaazi yao. Wakimbizi wapatao 30,000 walitafuta hifadhi katika kituo cha misheni cha kikatoliki kilichopo mjini Duékoué. Mji huo ulioko Magharibi mwa Cote D'Ivoire ulifahamika kwa kuwa na wafuasi wengi wa Gbagbo. Cyprien Ahouré, ambaye ni Padre katika kituo hiki anakumbukia mapigano yaliyofanyika mjini humo: "Lilikuwa jambo la kuogopesha kabisa. Hali ilikuwa mbaya kabisa siku hiyo ya tarehe 29 mwezi Machi. Lakini hali hii ilianza tayari tarehe 28. Tutalazimika kuishi na kumbukumbu hizi milele."

Wakimbizi mjini Duékoué, Cote D'Ivoire

Wakimbizi mjini Duékoué, Cote D'Ivoire

Siku chache baada ya mapigano makali anayoyakumbuka Padre huyu, makaburi makubwa yaliyokuwa na mamia ya maiti yaligunduliwa. Mashirika yanayotoa msaada wa kibinadamu yaliwasili mjini Duékoué na kutoa misaada kwa watu walionusurika.

Inakadiriwa kwamba jumla ya watu 3,000 waliuwawa katika kipindi kizima cha mapigano huku wengine 50,000 wakiyakimbia makaazi yao. Baada ya kuingia madarakani, Alassane Ouattara aliunda kamisheni ya maridhiano akifuata mfano wa nchi ya Afrika Kusini. Lakini kazi ya kamisheni hiyo haikuonekana. Hata shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelaumu kwamba hakuna upepelezi unaoendelea juu ya mauaji yaliyofanywa baada ya kipindi cha uchaguzi.

Mwandishi: Katrin Gänsler
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman