1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka 2014 ulikuwa mgumu kwa waandishi wa kimataifa

Josephat Nyiro Charo23 Desemba 2014

Kamati ya kimataifa ya kuwalinda waandishi wa habari, CPJ, imesema leo (23.12.2014) waandishi kiasi 60 waliuwawa kazini 2014 au kwa sababu ya kazi yao. Asilimia 44 ya waandishi walilengwa katika mauaji.

https://p.dw.com/p/1E9Do
Symbolbild Pressefreiheit / Tag der Pressefreiheit
Picha: picture-alliance/dpa

Kamati ya CPJ yenye makao yake makuu mjini New York nchini Marekani, imesema katika ripoti yake mpya iliyochapishwa leo kwamba idadi kubwa isiyo ya kawaida au takriban asilimia 20 ya waandishi waliouwawa walikuwa ni wa kimataifa, ingawa idadi kubwa ya waliotishwa iliendelea kuwajumuisha waandishi katika nchi zao za asili.

Miongoni mwa waandishi waliouwawa mwaka huu ni Anja Niedringhaus, mpiga picha wa shirika la habari la Associated Press aliyepigwa risasi alipokuwa akiripoti kuhusu uchaguzi wa Afghanistan.

Ripoti ya Kamati ya CPJ imesema idadi ya waandishi wa habari waliouwawa mwaka huu ilipungua kutoka 70 mwaka uliopita, lakini miaka mitatu iliyopita imekuwa mibaya zaidi tangu shirika hilo lilipoanza kuorodhesha matukio ya aina hiyo mnamo mwaka 1992.

Kriegsfotografin Anja Niedringhaus Archivbild 2005 Rom
Anja NiedringhausPicha: picture-alliance/AP Photo

Mzozo unaoendelea nchini Syria ambao sasa umeingia mwaka wa nne, umechangia kwa kiwango kikubwa. Ripoti hiyo imesema waandishi wapatao 17 waliuwawa mwaka huu, huku wengine wapatao 79 wakiwa wameuwawa tangu mapigano yalipoanza mwaka 2011.

Waandishi wa kigeni walilengwa

Syria imehusishwa na visa viwili vya kutisha vya mauaji ya waandishi wa habari mwaka huu, kuchinjwa kwa waandishi huria wa kimarekani James Foley na Steven Sotloff na kundi linalojiita Dola la Kiislamu. Wote wawili walikuwa wamepotea wakati wakiripoti kuhusu mzozo huo wa Syria.

Mzozo nchini Ukraine kati ya serikali mpya na wanamgambo wanaoungwa mkono na Urusi ulisababisha waandishi watano na wafanyakazi wawili wa vyombo vya habari kuuwawa wakati mahusiano kati ya Urusi na mataifa ya magharibi yalipoporomoka na kufikia kiwango cha chini kabisa tangu kumalizika kwa vita baridi. Mauaji hayo yalikuwa ya kwanza kurekodiwa na kamati ya CPJ nchini Ukraine tangu mwaka 2001.

Siku 50 za vita katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na Wapalestina wakati wa msimu wa kiangazi zilisababisha waandishi wapatao wanne na wafanyakazi wengine watatu wa vyombo vya habari kuuliwa, akiwemo mpiga picha wa shirika la habari la Associated Press, AP, Simone Camili na mkalimani Ali Shehda Abu Afash, waliouwawa na mlipuko wa mabaki ya bomu.

James Foley Journalist Reporter
James FoleyPicha: picture-alliance/dpa

Takwimu kuhusu vifo

Nchini Iraq, waandishi wasiopungua watano waliuwawa, watatu kati yao walipokuwa wakiripoti mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu, wakati lilipokuwa likiyateka maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Ripoti ya CPJ inazungumzia mauaji ya kwanza ya waandishi wa habari katika kipindi cha miaka kadhaa katika baadhi ya nchi, zikiwemo Paraguay, ambako vifo vitatu viliripotiwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2007 na Myanmar, ambako kuuliwa kwa mwandishi wa habari aliyekuwa akizuiliwa, ni kifo cha kwanza tangu mwaka 2007.

Kamati ya CPJ pia imeripoti mauaji ya kwanza ya mwandishi wa habari katika Jamhrui ya Afrika ya Kati, ambayo imegawanyika kutokana na machafuko kati ya Wakristo na Waislamu. Na hata kuripoti mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola kumesababisha vifo vya waandishi huku maiti za mwandishi na wafanya kazi wawili wa vyombo vya habari ikipatikana katika kijiji kimoja nchini Guinea, ambako walikuwa wamekwenda kuripoti kuhusu kampeni ya uhamasishaji wa umma.

Kamati ya Kimataifa ya kuwalinda waandishi wa habari CPJ, inasema inachunguza vifo vya waandishi wapatao 18 mwaka huu. Shirika hilo halihesabu vifo vinavyotokana na magonjwa au ajali ya magari au kuanguka kwa ndege mpaka ajali hizo ziwe zilisababishwa na hatua za uchokozi.

Mwandishi: Josephat Charo/APE

Mhariri:Gakuba Daniel