1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka 2008 ulikuwa ni mwaka wenye joto sana tangu mwaka 1850

Kabogo Grace Patricia18 Desemba 2008

Utafiti mpya juu ya mabadiliko ya hali ya hewa uliyofanywa na Umoja wa Mataifa umeonyesha mwaka 2008 ulikuwa ni mwaka wa joto sana tangu mwaka 1850, wakati wanasayansi walipoanza kuhifadhi kumbukumbu za hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/GJCE
Moja ya eneo lenye ukame duniani, mengi yakiwa yamesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.Picha: picture-alliance / chromorange

Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), matokeo mabaya ya hali ya hewa ikiwemo mafuriko, ukame, dhoruba ya theluji na mawimbi ya joto yalihifadhiwa kwenye nchi nyingi duniani.

Utafiti wa shirika hilo unaonyesha kuwa mwaka huu wastani wa halijoto ya nchi kavu na bahari ulikuwa nyuzijoto 0.31 sentigredi, hivyo kuwa ya juu kuliko viwango vilivyoandikwa kati ya mwaka 1961 na 1990. Taarifa za mwanzo kwa mwaka 2008 zimeegemea data za mabadiliko ya hali ya hewa kutoka mitandao ya nchi kavu ya vituo vya hali ya hewa, meli na maboya pamoja na satellites.

Carine Richard-Van Maele wa shirika hilo la WMO, amesema pia mwaka 2008 ulikuwa mwaka wenye wastani wa juu wa halijoto kwa Ulaya, zikiwemo nchi za Scandnavia na Siberia. Katika maeneo mengi ya Ulaya mwezi Januari na Februari, kwa mwaka huu ilikuwa siyo ya baridi sana huku wastani wa halijoto ukiongezeka kwa nyuzijoto 7 sentigredi katika nchi za Scandnavia. Kwa nchi hizo za Scandnavia ulikuwa ni msimu wa baridi uliokuwa na joto hiyo ikiwa hali ambayo haijatokea kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Data hizo zinaonyesha kuwa mwezi Februari, mwaka huu ulikuwa mwezi wa baridi katika maeneo mengi ya Marekani. Watafiti hao wa WMO wamegundua kuwa katikati ya majira ya joto, baadhi ya sehemu ya Amerika ya Kati yalikumbwa na mawimbi ya baridi huku halijoto ikishuka chini ya nyuzijoto 6 sentigredi.

Kwa mujibu wa data za shirika hilo, mabadiliko ya hali ya hewa kwa mwaka huu yamesababisha ukame mkubwa, mafuriko na dhoruba katika maeneo mengi ya dunia. Aidha, watafiti wa shirika hilo wamesema wamegundua mwaka huu shimo la ozoni ya Antaktiki lilikuwa kubwa kuliko mwaka uliopita wa 2007. Hali kama hiyo pia imeonyesha barafu ya bahari ya Atik ilidondoka kwa kiwango cha chini mara mbili tangu vipimo vya satellite vilipoanza mwaka 1979.

Katika kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa na matokeo yake kwa uchumi na mazingira ya dunia, Umoja wa Mataifa Jumanne iliyopita ulitangaza mwongozo mpya kwa ajili ya kuzisaidia nchi mbalimbali duniani kukusanya taarifa muhimu ili kukabiliana na majanga ya asili. Mwongozo huo ni pamoja na kuwa na mifumo inayofaa ya kugundua mahitaji, kusimamia data na kusaidia kupunguza makadirio ya matokeo, ili kufanya majanga asili kutokuwa majanga yanayosababishwa na mwanadamu.