1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa Uturuki na Ulaya wazidi kupamba moto

Sylvia Mwehozi
13 Machi 2017

Mvutano baina ya Uturuki na nchi za Ulaya umezidi makali baada ya Uturuki kumwita balozi wa Uholanzi nchini humo kulalamika juu ya vitendo vilivyofanywa na polisi wa Rotterdam dhidi ya waandamanaji wa Kituruki.

https://p.dw.com/p/2Z5Lz
Türkei Niederländisches Konsulat in Istanbul - Protest
Picha: Reuters/O. Orsal

Katika taarifa ya kidiplomasia iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Uturuki, imesema uingiliaji wa polisi haukuwa sahihi na kutaka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya polisi hao.

Polisi wa Uholanzi walitumia mbwa na maji ya kuwasha hapo siku ya Jumapili (12.03.2017) kuwatimua mamia ya waandamanaji ambao walikuwa wakipeperusha bendera za Uturuki nje ya ubalozi mjini Rortterdam. Baadhi ya waandamanaji walirusha chupa na mawe huku baadhi yao wakipigwa na polisi kwa mujibu wa mashuhuda.

Denmark nayo imeungana na nchi nyingine kupinga juhudi za Uturuki kufanya kampeni kwenye nchi za Ulaya. Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Lokke Rasmussen amependekeza kuwa ziara ya waziri mkuu wa Uturuki, Binali Yildrim iliyokuwa ifanyike baadae mwezi huu ihairishwe kutokana na mvutano uliopo baina ya nchi hiyo na Uholanzi.

Polisi wa Uturuki wakiwa wamezuia lango kuu la Ubalozi wa Uholanzi mjini Istanbul
Polisi wa Uturuki wakiwa wamezuia lango kuu la Ubalozi wa Uholanzi mjini IstanbulPicha: Getty Images/AFP/Y. Akgul

Ujerumani yenyewe imesema ingawa haijazuia wanasiasa wa Uturuki kufanya kampeni, hiyo haimaanishi kuwa watakuwa huru kufanya watakavyo katika siku za usoni. Manispaa kadhaa za Ujerumani zilisitisha mikutano kadhaa ambayo mawaziri wa Uturuki walipaswa kuhutubia ili kutafuta uungaji mkono kura ya maoni itakayompatia mamlaka zaidi rais Erdogan.

Waziri katika ofisi ya Kansela Merkel Peter Altmaier amesema hii leo kuwa kwa hadi kufikia sasa katika kipindi cha miaka 60 Ujerumani imekuwa ikirudia marufuku kwa nchi kama hiyo, akitolea mfano muungano wa kisovieti, China na nchi nyingine ambazo zilikuwa katika vita baridi.

Mzozo na mataifa ya Ulaya

Uturuki inazozana na nchi kadhaa za Ulaya kutokana na jaribio lake la kutaka kuendesha mikutano ya hadhara ili kufanya kampeni kwa Waturuki walioko nje ya nchi kwa ajili ya kupiga kura ya 'Ndiyo' katika kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Aprili 16.

Rais Erdogan amekuwa akilenga idadi kubwa ya Waturuki wanaoishi Ulaya hususan Ujerumani na Uholanzi kuweza kumsaidia kupata ushindi mwezi ujao katika kura hiyo ya maoni. "Tukio lililotokea Uholanzi ilikuwa ni ukiukwaji wa demokrasia, sheria za kimataifa, kanuni na heshima. Kuna mwanga utachomoza kutoka Ulaya? Hapana. kwanini? Kwasababu hawataweza kuumana wenyewe. Wote ni walewale. Uholanzi imefanya mambo mambo yasiyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya ambao wanaongozwa na utawala wa sheria, bali kama nchi isiyokuwa na utawala," alisema rais Erdogan. 

Türkei Präsident Erdogan Rede in Istanbul
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan Picha: picture-alliance/Ap Photo/Y. Bulbul

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, alifanikiwa kufanya mkutano wa hadhara katika mji wa Metz nchini Ufaransa licha ya kupigwa marufuku nchini Ujerumani na Uholanzi.

Cavusoglu amesema mbele ya umati wa Waturuki wapatao 800 kuwa Uholanzi ijitayarishe na athari za kuizuia ndege aliyokuwamo ndani yake, kutuwa nchini humo akilenga kufanya mkutano katika mji wa Rotterdam siku ya Jumamosi.

Mataifa mengi ya barani Ulaya yamepinga kufanyika mikutano katika miji yao kwa kutaja sababu za usalama, jambo lilowakasirisha viongozi wa Uturuki.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga