Mvutano wa kimamlaka waibuka Gabon | Matukio ya Afrika | DW | 19.11.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mvutano wa kimamlaka waibuka Gabon

Rais wa Gabon Ali Bongo amelazwa hospitalini kwa zaidi ya wiki tatu. Na sasa nguvu za makamu wake zimeongezwa kuhakikisha kile serikali ya Gabon imekiita kuendeleza shughuli za dola uamuzi ambao upinzani umeupinga. 

Rais wa Gabon amekuwa akitibiwa katika hospitali ya King Faisal mjini Riyadh nchini Saudi Arabia tangu Oktoba 24. Kuna uvumi kuwa alipatwa na kiharusi lakini hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa kuthibitisha.

Hadi sasa hakuna tarehe rasmi iliyotangazwa ya Rais Bongo kurejea nchini Gabon msemaji wake Ike Ngouoni alikairiwa na duru za habari akisema Rais Bongo amekuwa akisumbuliwa na kizunguzungu kikali lakini sasa afya yake inaimarika.

Siku ya jumatano mahakama ya katiba nchini Gabon chini ya Rais wake Marie-Madeleine Mborantsuo ilitangaza marekebisho madogo ya katiba katika ibara inayozungumzia hatua za kuchukua iwapo mkuu wa nchi hatoweza kwa muda fulani kutekeleza majukumu yake.

Uamuzi huo wa mahakam ulitokana na hatua za makamu wa rais Pierre-Claver Maganga Moussavou ambaye aliitaka mahakama ya kikatiba kuingilia kati ili kuondoa ombwe la uongozi nchini humo kwa kutumia ibara za 13 na 16 za katiba ya Gabon.

Gabun Stade d'Oyem Eröffnung Präsident Ondimba

Rais Bongo akiwa katika moja ya shughuli za kijamii nchini mwake.

Moussavou aliita mahakama kuamua ni nani kwa mujibu wa katiba anayepaswa kuongoza vikao vya baraza la mawaziri ili chombo hicho kiwezo kushughulikia masuala muhimu ya taifa katika kipindi ambacho rais hatokuwepo mamlakani kwa muda.

Kipengele kipya kilichoongezwa kwenye katiba katika marekebisho yaliyotangazwa na mahakama kimetoa nafasi ya baadhi ya majukumu kutekelezwa na makamu wa rais au waziri mkuu na makamu wa rais amepewa nguvu ya kuitisha na kuongoza vikao vya baraza la mawaziri.

Mahakama ya katiba imetetea uamuzi wake kwa kusema unalenga kuhakikisha shughuli za uendeshaji nchi hazikwami na huduma za umma zinaendelea bila kutatizwa.

Gabun Präsident Bongo Poltischer Dialog

Rais Ali Bongo akiwa na mkewe Sylvia kwenye makazi ya rais mwaka 2017.

Hata hivyo upinzani umeikosoa hatua hiyo kama jaribio la kuimarisha madaraka ya ukoo wa rais Bongo.  Mtaalamu wa masuala ya siasa nchini Gabon Andre Adjo amesema uamuzi wa mahakama umeunda masharti mepya amabyo hapo kabla hayakuwepo kwa mujibu wa katiba. Kulingana na Adjo katiba ya Gabon kabla ya marekebisho hayo tayari ilikuwa imeweka masharti ya kuitishwa uchaguzi ndani ya siku 45 ikiwa rais atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa kujiuzulu, kifo au sababu za kiafya.

Kwa namna hiyo uamuzi binafsi wa mahakama wa kupitisha kipengele kipya hauweki ukomo wa ni muda gani rais aliyeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa sabbau za kiafya inafaa awachie madaraka na uchaguzi mpya kuitishwa.

Kuhusu wasiwasi wa kutokea mapinduzi ya kijeshi katika kipindi ambacho rais bongo hayupo nchini humo mtaalamu mwengine wa masuala ya siasa Wilson-Ande Ndombet amesema uwezekano wa suala hilo ni mdogo ikizingatiwa kuwa kikosi cha ulinzi wa rais kinaongozwa na binamu wa rais Bongo na Gabon haijashughudia mapinduzi ya kijeshi tangu mnamo 1960.

Ikiwa Rais Bongo hatopona huo unaweza kuwa mwisho wa zama za utawala wa miongo mitano wa familia yake na utajiri mkubwa waliochuma wakiwa madarakani. Baba yake rais Ali Bongo, Omar Bongo aliiongoza Gabon tangu 1967 hadi alipofariki mwaka 2009 na hakuna uwezekano kuwa mwanafamilia mwingine anaweza kuchukua madaraka nchi humo.

Na kulingana na mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka nchini jirani ya Cameroon Louis Kemanyou amesema upinzani unaongozwa na Jean Ping aliyeshindwa dhidi ya bongo kwa kura chache wakati wa uchaguzi wa 2016 hautokubali hilo litokee.

Mwandishi: Rashid Chilumba