1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano Ujerumani watishia kuiangusha serikali

Saumu Mwasimba
2 Julai 2018

Waziri wa mambo ya ndani na kiongozi wa chama cha CSU atishia kujiuzulu na kusababisha kitisho cha kusambaratika kwa serikali ya muungano iliyokaa madarakani miezi mitatu na nusu

https://p.dw.com/p/30f9c
Archivbild: Berlin - Merkel und Seehofer
Picha: picture-alliance/dpa/B. v. Jutrczenka

Muungano wa Kansela Angela Merkel uko katika mkorogano mkubwa baada ya waziri wa mambo ya ndano Horst Seehofer kutishia kujiuzulu. Leo yanasubiriwa mazungumzo kati ya waziri huyo wa mambo ya ndani kutoka chama cha Christian Social Union CSU na chama cha CDU cha  kansela Angela Merkel.Mgogoro huu unaorindima kwa wiki kadhaa sasa unatokana na mvutano kuhusu sera ya wahamiaji.

Mvutano huu unaoendelea umezusha maswali kuhusu hatma ya serikali ya muungano Ujerumani ambayo imekaa madarakani kwa miezi mitatu tu na nusu.Vyama ndugu vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU kutoka Bavaria vinavutana kuhusu suala la wahamiaji.

Horst Seehofer ambaye ni waziri wa mambo ya ndani anataka wakimbizi waliojiandikisha nchi nyingine wanaokuja kuomba hifadhi Ujerumani wafukuzwe wakiwa bado wako mpakani lakini Merkel anashikilia msimamo wake kwamba Ujerumani haipaswi kuchukua hatua kivyake bila kuushirikisha Umoja wa Ulaya.

Berlin - Angela Merkel bei CDU Treffen
Picha: Getty Images/S. Gallup

Seehofer anasema kwamba hatua zilizofikiwa na Umoja wa Ulaya kukabiliana na suala la wahamiaji wiki iliyopita hazitoshi na kwa maana hiyo anatishia kujiuzulu. Hata hivyo leoatafanya mazungumzo na chama cha CDU.

Uongozi wa chama cha Kansela Merkel jana usiku uliidhinisha  azimio linaloweka wazi kwamba hatua ya kuwafukuza wakimbizi bila kuzishirikisha nchi nyingine za Ulaya litakuwa ni dalili mbaya kwa washirika wa Ujerumani. Armin Laschet ambaye ni waziri mkuu wa Jimbo la North Rhine Westphalia kutoka chama hicho cha CDU cha Kansela Merkel amefafanua mbele ya waandishi habari.

Tumeweka wazi msimamo wetu baada ya majadiliano marefu. Na msimamo huo sio kutokana na wananchi,sio kutokana na Seehofer wala Kansela Merkel ni  kwasababu tunataka suluhisho la Ulaya. Tunaona zipo harakati  na tunaamini sio sawa kwa sasa kuonesha dalili kwa washirika wetu wa Ulaya kwamba tunataka kuchukua hatua ya pekeyetu kama taifa''

Asylstreit - Sondersitzung CSU-Vorstand: Horst Seehofer
Picha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Bado haijawa wazi athari zitakazotokea endapo Seehofer atajiuzulu kama waziri wa mambo ya ndani na kiongozi wa chama cha CSU.Tayari lakini waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Soeder ameshasema kwamba jimbo hilo halitaki kuhatarisha uthabiti wa seriakali ya muungano huku akiweka wazi kwamba anataraji kutapatikana mwafaka na Kansela Merkel. Viongozi wa CDU na wabunge Jumatatu (02.07.2018) wametilia mkazo umuhimu wa kuendeleza mshikamano kati ya chama chao na CSU,ambalo ndo kundi kubwa bungeni.Mvutano huu pia umeidhoofisha thamani ya sarafu ya Yuro dhidi ya sarafu nyingine zenye nguvu.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo