1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano mkutano wa Lima

Elizabeth Shoo12 Desemba 2014

Katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu ongezeko la joto duniani unaofanyika Lima, Peru, upo mvutano kati ya nchi tajiri na maskini kuhusu hatua za kuchukua ili kuzuia mabadiliko ya tabia ya nchi.

https://p.dw.com/p/1E36Z
Mkutano wa tabia ya nchi mjini Lima
Picha: Reuters

Ni nani anayepaswa kubeba jukumu la kulinda mazingira na kupunguza utoaji wa gesi ya kaboni katika anga? Hilo ndilo swali wanalojadili wajumbe kutoka nchi 195 katika mkutano wa Umoja wa Mataifa unaondelea mjini Lima. Mataifa yanayoendelea yanazinyooshea kidole nchi tajiri na kusema kwamba zinatakiwa kuwajibika zaidi kwani ndizo zinazochafua mazingira kwa kiasi kikubwa. Lakini nchi tajiri zinakataa na kutaka mataifa yanayoinukia kama vile China na India yadhibiti utoaji wa gesi chafu ya carbon dioxide kutoka kwenye viwanda na magari kwa mfano.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, aliuhudhuria mkutano wa Lima kwa kifupi na kuzihimiza nchi zote kuchukua hatua. Kerry pia alisifu makubaliano ambayo yameweza kufikiwa hadi sasa. "Marekani na China ni nchi mbili ambazo kwa muda mwingi zilionekana kuwa viongozi wa pande mbili zinazopingana katika mjadala huu," alisema Kerry. "Lakini sasa nchi hizo zimekubaliana kwenye masuala kadhaa. Hii ni hatua ya kihistoria na inapaswa kutufundisha kwamba vizuizi tulivyokutana navyo katika miaka iliyopita vinaweza kuondolewa."

Waziri wa mambo ya nje wa Marekanin John Kerry akiwa na rais Ollanta Humala wa Peru
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa na rais Ollanta Humala wa PeruPicha: Reuters/E. Castro-Mendivil

Mkataba kamili kusainiwa Paris 2015

Kerry amezitaka nchi zinazoendelea pia kukubali kufanya na mabadiliko ya sera na kulivalia njuga suala la ulinzi wa mazingira. Alikumbusha kuwa hivi sasa asilimia 50 ya gesi ya kaboni inatoka katika nchi zinazoendelea.

Mpaka sasa mkutano wa Lima haujawa na mafanikio makubwa lakini waziri wa mazingira wa Peru Manuel Pulgar-Vidal ameahidi kwamba mkutano hautomalizika bila wajumbe kuweka misingi ya ahadi watakazotoa katika mkutano wa mazingira utakaofanyika jijini Paris mwakani. Hadi hapo kila nchi inapaswa kuweka bayana utayarifu wake wa kupunguza utoaji wa hewa chafu ya kaboni. Lengo la mkutano wa Paris ni kuwa na mkataba utakaodhibiti uchafuzi wa mazingira na hivyo kufanya kiwango cha joto duniani kisiongezeke kwa zaidi ya nyuzi joto 2 za celcius ifikapo mwaka 2100.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman