1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa NASA watishia kususia uchaguzi

Admin.WagnerD15 Mei 2017

Muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, umetishia kuandamana na kususia uchaguzi ujao ikiwa tume ya uchaguzi nchini humo haitafutilia mbali rufaa iliyowasilisha mahakamani kupinga uamuzi wa mahakama.

https://p.dw.com/p/2czLK
Kenia Oppositionsführer Musalia Mudavadi, Raila Odinga, Isaac Ruto, Kalonzo Musyoka, and Moses Wetangula  in Nairobi
Picha: Reuters/T. Mukoya

Muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA umetishia kufanya maandamano na kususia uchaguzi ujao ikiwa tume ya uchaguzi nchini humo IEBC haitafutilia mbali rufaa iliyowasilisha mahakamani kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama kuruhusu upinzani kuweka kituo chao cha kukusanya matokeo ya uchaguzi. Huku zikiwa zimesalia siku 84 uchaguzi mkuu kufanyika, umekuwa mchezo wa paka na panya kati ya chama kinachotawala cha jubilee na muungano wa upinzani NASA huku lawama zikitoka kila upande kushutumiana.

Upinzani unadai kwamba chama cha Jubilee kinatumia tume ya uchaguzi nchini kubatilisha uamuzi wa mahakama uliotolewa mwezi uliopita ambao uliwaruhusu kuwa na kituo chao cha kuhesabu kura.

Kiongozi wa walio wengi bungeni Adan Duale anadai kwamba upinzani una njama ya kuiba kura kutumia mfumo wa kielektroniki "Tunajua wanaweka kituo cha kukusanya matokeo nchini Tanzania na watakapoweka kituo hicho watavuruga mtandao wa IEBC na wanataka kutumia matokeo ya kugushi kujitangaza washindi”.

Wahlen Wahlurnen in Mombasa Kenia
Picha: REUTERS

Kura zihesabiwe na kutangazwa vituoni

Upinzani unataka kura za urais zihesabiwe na kutangazwa katika vituo vya maeneo ya uwakilishi bungeni jambo ambalo tume ya uchaguzi nchini imepinga.

Tume ya IEBC ilienda mahakama kutaka upinzani usiruhusiwe kuweka kituo cha kukukusanya matokeo ya uchaguzi mkuu.

Mwenyekiti wa tume ye Uchaguzi Wafula Chebukati alifafanua uamuzi huo akisema, "Vyama vya kisiasa na vyombo vya habari vina Uhuru wa kukusanya matokeo ya chaguzi kwa matumizi yao lakini ni wajibu wa tume ya IEBC kutangaza matokeo hayo.

Kiongozi wa chama cha ODM atakayeperusha bendera ya muungano wa NASA, Raila Odinga, aliionya tume ya uchaguzi.

Chama cha Jubilee kinadaiwa kupanga njama ya wizi wa Kura kwenye uchaguzi ujao.

Wakati huo huo upinzani umehusisha mfumko wa bei za vyakula na uchaguzi mkuu ujao uliopangiwa kufanyika tarehe nane mwezi Agosti mwaka huu.

Mwandishi: Alfred Kiti

Mhariri: Iddi Ssessanga