1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muammar Gaddafi

Abdu Said Mtullya5 Februari 2009

Jee itawezekena kwa nchi za Afrika kuleta muungano wa bara lao?

https://p.dw.com/p/GnhS
Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika-AU Muammar Gaddafi.Picha: AP

Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika,Muammar Gaddafi wa Libya anaupa kipaumbele mradi wa kuundwa muungano wa Afrika .Lakini wadadisi wa masuala ya kimataifa wanasema lengo hilo bado lipo mbali na hali halisi.

Gaddafi aliekuwa kiongozi wa pekee kutoka kaskazini mwa Afrika kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Afrika mjini Addis Ababa, alipokea kijiti kutoka kwa mwenyekiti wa hapo awali rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taratibu za Umoja wa Afrika AU Gaddafi atakuwa mwenyekiti wa Umoja huo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Yumkini kipindi hicho kitakuwa fursa kwa Gaddafi kujaribu kuleta mapinduzi kwenye Umoja wa Afrika.

Wazo la Gaddafi linafahamika- anataka kuundwa kwa serikali moja kwa Afrika nzima, na anataka Afrika iwe na jeshi moja la askari milioni 2. Kiongozi huyo wa Libya pia anataka Afrika iwe na sarafu, na pasipoti moja. Gaddafi amekuwa analea wazo hilo tokea mwaka 2007. Lakini wazo hilo lilipingwa na jirani zake.

Safari hii pia amekuja na pendekezo juu ya kuundwa Umoja wa Afrika-United States of Afrika. Pendekezo hilo lilijadiliwa Addis Ababa lakini halikuleta mabadiliko ya kina kirefu kwenye Umoja wa Afrika.

Hatahivyo nchi za Afrika zimekubaliana kuunda mamlaka mpya ya Umoja wa Afrika itakayochukua nafasi ya kamisheni ya hapo awali.Mamlaka hiyo inapaswa kuwa na jukumu kubwa zaidi,fedha zaidi na kuwa na uhuru mkubwa katika kutekeleza wajibu wake. Gaddafi ametangaza kuwa,katika msingi wa mabadiliko hayo, Muungano wa Afrika utaundwa kwenye kikao kifuatacho cha nchi za Umoja wa Afrika mnamo miezi sita ijayo!

Lakini aliekuwa mkurugenzi wa taasisi ya mjini Hamburg ya mitaala ya kimataifa ya Rolf Hofmeier amesema kuwa lengo hilo bado lipo mbali.

Mkurugenzi huyo pia ametabiri kuwa Umoja wa Afrika utakabiliwa na matukio ya ugeugeu mnamo kipindi cha mwaka mmoja ujao kutokana na uenyeketi wa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.

Hatahivyo mtaalamu wa siasa, Issa Shivji wa Tanzania amesema wazo la kuundwa muungano wa Afrika linastahili kuungwa mkono.