1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muswada tata waanza kujadiliwa Uturuki

17 Mei 2016

Bunge la Uturuki Jumanne (17.05.2016) limeanza kujadili muswada wenye utata mkubwa sana ambao utawavuwa wabunge kadhaa kinga ya kutoshitakiwa na ambao wabunge wa upinzani wanasema unakusudia kuwatimuwa bungeni.

https://p.dw.com/p/1IpPi
Picha: picture-alliance/dpa/Str

Muswada huo tayari umepelekea kuzuka kwa matukio ambayo hayakuwahi kushuhudiwa kabla katika kamati ya kujadili muswada huo ambapo wabunge wametwangana makonde na hata kupigana mateke badala ya kujadili muswada huo.

Mjadala huo umeanza mchana na unatarajiwa kuwa mkali ambapo utaendelea hadi usiku na kupigiwa kura ya mwisho hapo Ijumaa.

Kwa mijibu wa sheria ya sasa ya Uturuki wabunge katika bunge wana haki ya kupatiwa kinga kamili ya kutoshtakiwa. Iwapo muswada huo utapita utawaondolea kinga hiyo wabunge 130 kutoka vyama vyote ambavyo majalada yao yamepelekwa kwa spika wa bunge.

Muswada unakusudia kukikomowa chama cha HDP

Lakini chama kinachouwaunga mkono Wakurdi cha (DHP) kinasema muswada huo unakusudia hasa kuwatimuwa wabunge wake kutoka katika bunge hilo.

Wabunge wa chama cha upinzani cha HDP wakiwa bungeni.
Wabunge wa chama cha upinzani cha HDP wakiwa bungeni.Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Wabunge wa chama hicho ni rahisi kufunguliwa mashtaka kwa madai ya kuwa na uhusiano au hata kuuga mkono kwa maneno chama kilichopigwa marufuku cha Wafanyakazi cha Wakurdi ambacho kinapambana katika uasi waliouanzisha upya dhidi ya serikali.

Viongozi wenza wa chama cha HDP Selahattin Demirtas na Figen Yuksegdag ambao wote wawili yumkini wakafunguliwa mashtaka wamesema katika baruwa iliyotumwa kwa wabunge wa Umoja wa Ulaya kwamba kile inachotafuta muswada huo ni kukiangamiza chama chao cha HDP bungeni.

Iwapo idadi fulani ya wabunge wa chama hicho itabidi wasiwepo bungeni itakuwa rahisi kumfungulia njia Rais Tayyip Erdogan kutimiliza ndoto yake ya kubadili katiba kwa kuanzisha mfumo wa rais mwenye madaraka makubwa ya utendaji nchini Uturuki.

Chama cha HDP kinasema muswada huo utapelekea kufunguliwa mashtaka kwa wabunge wake hamsini kati ya wabunge 59 ilio nao bungeni.

Kupita kwa muswada ni mapinduzi

Viongozi hao wenza wa chama hicho wamesema iwapo muswada huo utafanikiwa mapinduzi hayo yatakuwa hatua muhimu kabisa kwa Erdogan kuondoa demokrasia bungeni nchini Uturuki kwa kuweka utawala kamili wa rais.

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki (kulia)akizungumza na naibu wazirí mkuu Bulent Arinc.
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki (kulia)akizungumza na naibu wazirí mkuu Bulent Arinc.Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Wameongeza kusema iwapo muswada huo utakuwa sheria unaongeza uwezekano wa viongozi kama wao ambao tayari wanalengwa kwa uchunguzi wa jinai kushtakiwa kwa madai ya kufanya propaganda za kigaidi kwa chama cha PKK na hata kutupwa gerezani.

Chama tawala cha Haki na Sheria AKP kinahitaji kupata kura 367 kati ya viti vya bunge 550 ambao ni wingi wa theluthi mbili kuupitisha muswada huo moja kwa moja.

Kura 330 zinatosha kuitisha kura ya maoni juu ya suala hilo.

Chama cha AKP kina viti 317 bungeni na kinataraji kuungwa mkono na chama cha sera za kizalendo cha MHP ambacho kinakichukia chama cha HDP na kina viti 40 bungeni.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef