Mustakbal wa Kosovo,siku ya siku ikiwadia-December 10 ijayo | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 07.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mustakbal wa Kosovo,siku ya siku ikiwadia-December 10 ijayo

Misimamo inatofautiana kati ya umoja wa ulaya,Marekani na Urusi kuhusu jimbo la Kosovo linalodai uhuru

default

Mawaziri wa NATO na wa umoja wa ulaya wajadiliana kuhusu Kosovo

Jumuia ya kimataifa na pande zinazohusika na mozozo wa Kosovo wamejiwekea muda mwengine :December 10 ijayo mkuu wa tume ya pande tatu ya baraza la usalama la umoja wa mataifa anatazamiwa kutoa ripoti kuhusu mustakbal wa jimbo la mizozo la Kosovo.Kiroja hapo ni kwamba misimamo ya serikali za pande zote mbili, mijini Pristina na Belgrade hailingani hata kidogo.Na hata wawakilishi wa tume ya pande tatu ya baraza la usalama-Umoja wa Ulaya,Marekani na Urusi hawazungumzi kwa kauli moja.

Hata muda wa mazungumzo ya wawakilishi wa tume ya pande tatu, ukifutwa December 10 ijayo,bado azimio la umoja wa mataifa nambari 1244 litaendelea kutumika katika jimbo la Kosovo ,azimio linalotambua kisheria Kosovo ni sehemu ya Serbia lakini chini ya usimamizi wa Umoja wa mataifa.

Mpira kwa hivyo umerejeshwa tena katika kambi ya baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Lakini hata huko,walishindwa msumu wa kiangazi uliopita kukubaliana juu ya azimio la umoja wa mataifa kusimamia utaratibu wa kuipatia uhuru wa aina fulani Kosovo.Urusi yenye kura ya turufu katika baraza la usa lama imepinga mswaada wa azimio ulioandaliwa kutokana na kile kijulikanacho kama “mpango wa Ahtisaarri.”

Kimsingi msimamo huo haujabadilika:Urusi inaunga mkono kikamilifu washirika wao wa Serbia.Marekani inatia kishindo Kosovo iwe huru na kutambuliwa haraka,pindi wakosovo wenye asili ya Albania watajitangazia uhuru wao .Umoja wa Ulaya hauna msimamo mmoja panapohusika na suala la uhuru wa Kosovo na kutambuliwa uhuru huo bila ya azimio jipya la Umoja wa mataifa.Kwa maneno mengine tunaweza kuuchambua msimamo wa Umoja wa ulaya kama ifuatavyo:

Miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, angalao 20 zinaunga mkono uhuru utangazwe na kutambuliwa haraka pindi Kosovo ikitangaza kujitenga na Serbia December 10 ijayo.Kundi hilo linazijumuisha pia Ujerumani,Uengereza, Ufaransa , Italy na Poland .

Wanaopinga moja kwa moja kutambulikwa uhuru wa Kosovo ni pamoja na Cyprus,Ugiriki na Slovakia.Hispania na Hungary zinasita sita.Mataifa hayo yanahoji si vyema kuchochea kiu cha uhuru kwa jamii za wachache.Cyprus inahofia,mbali na Uturuki, mataifa mengine pia yasije yakaitambua jamhuri iliyojitangaza wenyewe ya Uturuki katika eneo linalokaliwa na Uturuki,kaskazini mwa kisiwa hicho.

Umoja wa Ulaya unataka lakini kulinda mshikamano na kusaka msimamo wa pamoja kuhusu Kosovo,seuze tena Kosovo ikijitangazia uhuru,Umoja wa ulaya ndio utakaowajibika kuijenga upya sehemu hiyo.Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO ambayo wanachama wake wengi ni wa kutoka Umoja wa ulaya,inataka wanajeshi wake 16 elfu waendelee kuwepo Kos ovo ili kuzuwia pasitokee machafuko.Umoja wa Ulaya unapanga kuzungumza na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon,baada ya mkutano wa kilele wa viongozi wa umoja huo,utakaoitishwa muda mfupi baada ya kumalizika muda uliowekwa -December 10 ijayo.

Pengine kuna masikilizano yaliyofikiwa pamoja na serikali ya Kosovo,muda uliowekwa katika mpango wa Ahtisaari uheshimiwe-yaani May mwaka 2008 iwe tarehe ya kujipatia uhuru Kosovo.Hadi wakati huo Umoja wa ulaya utaibuka na msimamo mmoja na pengine pia baraza la usa lama la umoja wa mataifa litakua limeshakubaliana kuidhinisha azimio jipya.Wanasheria wa Umoja wa ulaya wanachunguza kwa sasa kama azimio nambari 1244 linaweza kutumika kama msingi wa kuendelezwa shughuli zake katika Kosovo.

 • Tarehe 07.12.2007
 • Mwandishi B.Riegert/Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CYel
 • Tarehe 07.12.2007
 • Mwandishi B.Riegert/Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CYel
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com