1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mustakabali wa Kosovo wajadiliwa Vienna

P.Martin21 Februari 2007

Wajumbe wa Serbia na Kosovo hii leo wamekutana Vienna nchini Austria kujadili mustakabali wa Kosovo.

https://p.dw.com/p/CHJd

Duru hii ya mazungumzo,ni nafasi ya mwisho kwa pande hizo mbili kujadili pendekezo la mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Martti Ahtisaari,kuipa Kosovo uhuru wa kiwango fulani,kabla ya suala hilo kupelekwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Tangu mpatanishi Martti Ahtisaari kutangaza pendekezo la kuipa Kosovo uhuru wa kiwango fulani,jungu limeanza kutokota katika jimbo hilo la kusini mwa Serbia.Wakati ambapo Wakosovo wenye asili ya Kialbania walio wengi zaidi katika jimbo hilo,wanaunga mkono mpango wa Ahtisaari,Waserbia wanaupinga katakata.

Majadiliano yalioanza leo hii yanatazamiwa kuendelea hadi tarehe 10 mwezi wa Machi kutafuta njia ya kuafikiana.Baadae katika mkutano wa kilele uliopangwa kufanywa pamoja na viongozi wa pande hizo mbili,Ahtisaari ndio atatayarisha hati ya mwisho itakayopelekwa kwenye Baraza la Usalama kupigiwa kura,mwishoni mwa mwezi wa Machi. Ahtisaari hii leo alipozungumza mjini Vienna alisema,hana matumani kuwa wajumbe wa Serbia na Kosovo watabadilisha misimamo yao na kukubaliana juu ya hatima ya Kosovo.Akaongezea na tunamnukulu:

“Katika maisha yangu marefu,nimejifunza kuwa watu wanapozungumzia “maafikiano” kuhusika na tatizo fulani,basi humaanisha upande mwingine ndio ukubaliane na msimamo wao.Na hali hiyo inadhihirika pia katika mgogoro huu.”mwisho wa nukulu.

Kwa bahati mbaya,huo ni ukweli wa mambo,kwani juma lililopita,bunge jipya la Serbia liliamua kwenda mkutanoni na jawabu moja tu,yaani kulikataa kabisa pendekezo la Ahtisaari.Hata waziri mkuu wa Serbia anaeondoka madarakani,Vojislav Kostunica alisema,”ukweli wa mambo ni kwamba kuhusika na Kosovo hakuna cha kufidia.Shinikizo zote ni za bure,mapendekezo yote hayana maana sawa na vile vivutio vya kutaka kuifanya Serbia iachilie maadili yake.”

Akaongezea kwamba wanakwenda Vienna “kueleza kuwa Serbia ipo tayari kwa maafikiano yenye maana,ambayo huheshimu maadili ya kimsingi ya utaratibu wa kimataifa.”

Hapo anachomaanisha ni kuheshimu mamlaka ya Serbia ya kujiamulia mambo yake.Katika hati ya Ahtisaari,neno “uhuru” halikutajwa.Lakini kile anachotaka kuipatia Kosovo ni madaraka ya kiwango fulani pamoja na bendera yake,wimbo wa taifa na uwezekano wa kuwa mwanachama katika mashirika ya kimataifa-mambo ambayo kwa maoni ya Serbia huenda mbali mno.Desemba mwaka jana,Serbia katika kura ya maoni iliyopigwa kuhusu katiba yake,iliamua kuwa milele Kosovo yapaswa kubakia sehemu ya Serbia isiyoweza kutengwa.