Musharraf atetea hatua ya kuahirisha uchaguzi wa ubunge | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.01.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Musharraf atetea hatua ya kuahirisha uchaguzi wa ubunge

Wapinzani walalamika kwa shingo upande

default

Rais wa Pakistan -Pervez Musharraf -akionekana kwenye runinga akitetea hatua ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa ubunge kutoka tarehe 8 Januari hadi Febuari 18,2008.

Uchaguzi wa ubunge nchini Pakistan umeahirishwa hadi Febuari 18 badala ya Januari mwaka huu.

Hatua hiyo imepingwa na upande wa upinzani ukidai kuwa ni njama za Rais Perves Musharraf kujipatia wabunge wengi.Hata hivyo rais anatetea hatua hii kama .

Rais Musharraf amenukuliwa kusema kuwa uamuzi wa tume ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi wa ubunge hadi Febuari 18 ni sawa na hatua moja ambayo haikuweza kuepukika.

Kauli ya rais imekaririwa na mjumbe wa chama chake cha PML-Q Tariq Azim.Azim,kwa wakati huo akiwa kama naibu waziri wa habari amevitaka vyama vya upinzani kukubali hatua hii iliotangazwa na mkuu wa tume ya uchaguzi Qazi Mohammed Farooq …nafikiri vyama vyote vya siasa ni lazima vifurahie uamuzi huu.Yaani vyama hivi vyote vinaelewa.Lakini baadhi vinapuuza kimakusudi hali halisi ilivyo kwa hivi sasa.Ofisi nyingi za tume ya uchaguzi zilichomwa na sasa maafisa wengi wa tume hiyo wanakaa nje chini ya mitina katika mazingira hayo ni vigumu kufanyika uchaguzi. Nafikiri hatua hii inavipendelea vyama hivyo na hivyo ni lazima waiunge mkono,amesema Azim.

Chama cha Bhutto na vingine vimelaani kwa shingo upande kuahirishwa huko kutoka januari 8 hadi febuari 18 na kusema hata hivyo vitashiriki.

Uchaguzi wa ubunge ni muhimu kama hatua muhimu kwa Pakistan ya kueleka utawala wa kiraia wa kidemokrasi chini ya Musharraf aliestaafu kama mkuu wa majeshi wiki chache zilizopita.

Chama cha Bhutto cha pakistan Peoples Party-PPP- ambacho ni kikubwa zaidi nchini humo kinadai kuwa kuahirishwa huko ni hatua ya kuwapa wafuasi wa Musharraf mda wa kufanya mizengwe katika kura.

Hata hivyo kitashiriki katika uchaguzi.Wadadisi wa mambo wanasema chama cha Bhutto kimeteseka na mauaji ya kiongozi wake. Lakini mwanachama wa chama cha rais Mushsraarf cha PML-Q hakubaliani na hayo …ikiwa kuna alieumia sana katika vurugu hizi za kuuliwa Benazir Bhutto bila shaka ni serikali.na yeyote aliefaidika kutokana na hali hiyo ni vyama vya siasa.Serikali haiwezi kufaidika na mauaji hayo.Hata sio chama cha PML-Q. Kusema kweli makaratasi yetu pamoja na mabango yamechomwa na mengine yanachanwa na ofisi zetu nyingi zimeshambuliwa na wafuasi wa vyama hivyo.Kwa hivyo ni sisi ambao tumeteseka,amesema Azim.

Wakati rais Musharraf akitetea hatua ya kuahirisha uchaguzi huo pia ameiomba Uingereza kusaidia kufanya uchunguzi wa kifo chake.Tangazo hilo laweza kutuliza hasira za umma kuhusu msimamo wa serikali ukitoa sababu kuwa kiongozi wa upinzani alikufa kwa kujigonga katika paa la gari bada ya kushambuliwa kwa risasi na bomu akitoka katika mkutano wa hadhara.

Lakini wafuasi wa Bhutto wanasisitiza kuwa uchunguzi wa Umoja wa Matifa ndio pekee unaoweza kutoa habari za ukweli wa nini kilichomuua Bi Bhutto.

Wafuasi hao wamepuuza tangazo la serikali la kuwa kikosi cha upelelezi cha Uingereza cha Scotland –yard kisaidie katika uchunguzi huo.

Marekani,mshirika mkuu wa utawala wa Musharraf ,kwa upande wake imepuuza mwito wa umoja wa Matifa kufanya uchunguzi ikisema kikosi cha upelelzi cha Uingereza cha Scotland yards kinasifika na kitatoa majibu sawa wanayotaka wananchi wa Pakistan kuhusu suala hilo.

Na hali ikiwa hivyo wapinzani wa serikali wanaihimiza kuwapa ulinzi wa kutosha hadi siku ya uchaguzi ilioahirishwa kutoka januari nane hadi febuari 18.

 • Tarehe 03.01.2008
 • Mwandishi Siraj Kalyango
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Cjjl
 • Tarehe 03.01.2008
 • Mwandishi Siraj Kalyango
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Cjjl

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com