Musharraf atashinda tena nafasi ya urais? | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Musharraf atashinda tena nafasi ya urais?

Pamoja na kupingwa kutokana na uongozi wake, serikali ya Pakistan imemwidhinisha Rais wa nchi hiyo Jenerali Perves Musharraf kuingia katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi utakaofanyika tarehe sita mwezi mwezi ujao .

Rais Jenerali Perves Musharraf

Rais Jenerali Perves Musharraf

Waziri Mkuu wa Pakistan Bwana Shaukat Aziz amesema serikali ya nchi hiyo imempitisha Rais General Perves Musharraf kutetea nafasi anayoishikilia katika uchaguzi ujao.

Uteuzi wa Rais huyo wa kijeshi umefanyika wakati ambao mahakamu kuu ya Pakistan ikitarajia kukaa na kujadili iwapo General Musharraf atafaa kuendelea na madaraka akiwa mkuu wa kijeshi. Polisi wa usalama wakiwa na silaha wameonekana kwenye eneo la Mahakamu kuu kabla ya maofisa kuanza mjadala kuhusu tukio hilo.

Waziri Mkuu Bwana Shaukat Aziz amekaririwa akisema kwamba siku hii ni muhimu kwa serikali ya nchi hiyo, na kwamba ana matumaini makubwa kwamba Rais General Musharraf, atashinda nafasi hiyo na kuwa madarakani kwa kipindi kingine.

General Perves Musharraf anatetea wadhifa wake kupitia chama cha Pakistan Muslim League-PML, na yeye mwenyewe anajigamba kwamba nafasi hiyo ni ya kwake.

Ikiwa General Musharraf atashinda nafasi ya urais, atabakia katika madaraka hayo na kuacha ukuu wa majeshi kushikiliwa na mtu mwingine. Na ikiwa atashindwa kupata urais, atabakia na cheo cha ukuu wa majeshi.

Hapo awali, Mwanasheria mkuu wa serikali ya Pakistan Malik Mohammad Qayyum, alisema kwamba haitawezekana tena kwa General Musharraf kuongoza nchi kijeshi.

Pamoja na kutaka kuendelea kuwa mkuu wa Pakistan, Rais General Musharraf amekumbanaa na vikwazo vingi na vikubwa katika kipindi cha uongozi wake, kuanzia vita dhidi ya ugaidi akiiunga mkono Marekani, pamoja na vurugu nyingi zilizosababisha vifo vya mamia ya raia.

Miezi miwili iliyopita watu kadhaa walipoteza maisha baada ya wanamgambo wenye msimamo mkali kuuteka msikiti mwekundu mjini Islamabad, ambapo majeshi ya serikali yalilazimika kutumia nguvu za ziada kurejesha usalama.

Wakiungwa mkono na watu wanaosemekana kuwa na ushirikiano na kikundi cha Taleban cha nchini Afghanistan, wanamgambo hao walitaka kumshinikiza Rais General Musharraf kutumia sheria za kiislamu kuongoza nchi.

Aidha, Marekani inaonekana kuwa karibu na kiongozi huyo wa kijeshi kwa vile pia imeidhinisha pesa nyingi kwa ajili ya kuisaidia Pakistan kukabiliana na vikundi vya kigaidi. Na huenda ikamsaidia General Musharraf kufikia lengo lake.

Lakini raia wengi nchini Pakistan wanajiuliza nini kitatokea ikiwa General Musharraf atashindwa kukamilisha malengo yake ya kutaka kuendelea kuwa Mkuu wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa katiba Rais atachaguliwa na jopo la pamoja la baraza la senate , bunge la ataifa na mabunge aya kimkoa, na baada ya hapo mabunge hayo yatavunjwa tayari kwa uchaguzi mkuu katikati ya mwezi Januari mwaka ujao.

 • Tarehe 27.09.2007
 • Mwandishi Tuma Provian Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH7c
 • Tarehe 27.09.2007
 • Mwandishi Tuma Provian Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH7c

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com