Musharraf abanwa ndani na nje arejeshe demokrasia Pakistan. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 06.11.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Musharraf abanwa ndani na nje arejeshe demokrasia Pakistan.

Rais G Bush amemtaka rais Pervez Musharraf aondoe hali ya hatari na arejeshe demokrasia nchini Pakistan. Rais Bush pia amemtaka Musharraf ajiuzulu ukuu wa jeshi.

Jenerali Pervez Musharraf

Jenerali Pervez Musharraf

Licha ya rais Musharraf kuwaambia wawakilishi wa kibalozi kuwa anadhamiria kunga’tuka kama kiongozi wa jeshi hali nchini Pakistan imeendelea kuwa ya mvutano.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia,mapambano yameendelea mjini Islamabad baina ya polisi na mawakili.Habari pia zinasema mawasiliano ya simu yamekatika.

Mawakili na watu kadhaa wa vyombo vya habari wamejeruhiwa katika mapambano na polisi katika miji ya Lahore,Karachi na Rawalpindi.

Hatahivyo rais Musharraf amerudi hatua moja nyuma .Msemaji wake ameeleza kuwa tarehe ya uchaguzi itasogezwa ili ikaribie ratiba ya uchaguzi, katikati ya mwezi januari.

Waziri wa habari Tariq Azeem amesema muda wa hali ya hatari utafupishwa kwa kadri itakavyowezekana.

Hatahivyo bunge la Pakistan linatarajiwa kukutana baadae ili kujadili suala la uchaguzi.Kuna habari, huenda bunge likapiga kura kuchelewesha uchaguzi hadi kwa kipindi cha mwaka mzima.

Wakati huo huo jaji mkuu wa Pakistan Iftikhar Chaudhry aliefukuzwa kazi, ametoa mwito kwa watu wa Pakistan juu ya kusimama na kupigania kurejeshwa katiba ya nchi.

Akizungumza kwa njia ya simu na mawakili mjini Islamabad bwana Chaudhry amemshutumu rais Musharraf alietangaza hali ya hatari jumamosi. Jaji huyo amesema kuwa katiba ya nchi imechanwa vipande vipande na kwamba kinacholazimu sasa ni kujitoa mhanga.

Rais Musharraf amesema ametangaza hali ya hatari kutokana na mgogoro uliosababishwa na ghasia za watu wenye itikadi kali na kutokana na kuvuruguika kwa mahakama.

Lakini wadadisi wamesema bwana Musharraf ametangaza hali ya hatari ili kuzuia uamuzi wa mahakama kuu juu ya iwapo kuchaguliwa kwake tena kuwa rais kulifanyika kwa njia halali mwezi jana.

Wakati huo huo habari ambazo hazijathibishwa zinasema watu zaidi ya 1500 ikiwa pamoja na mawakili wamekamatwa ama wanazuiwa majumbani mwao nchini Pakistan.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com