1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni aongoza matokeo ya awali nchini Uganda

15 Januari 2021

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais uliofanyika Alhamisi nchini Uganda yaliyotolewa usiku wa kuamkia leo yanaonesha rais Yoweri Museveni anaongoza dhidi ya mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi.

https://p.dw.com/p/3nwfG
Uganda Wahlen Yoweri Museveni
Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Kulingana na Tume ya Uchaguzi nchini humo matokeo ya awali kutoka vituo visipungua 300 vya kupigia kura, yanaonesha rais Museveni wa tawala cha NRM amepata asilimia 61.3 huku Kyagulanyi maarufu Bobi Wine kutoka chama cha NUP amejikingia asilimia 27.9 ya kura.

Hata hivyo bado ni mapema kueleza bayana mwelekeo wa uchaguzi huo ikizingatiwa kuwa idadi ya vituo 300 ambako zoezi la kuhesabu kura limemalizika ni ndogo ikilinganishwa na zaidi ya vituo 34,000 vilivyotumika katika uchaguzi wa siku ya Alhamisi.

Afrika Uganda Wahlen Bobi Wine, Popstar und Präsidentschaftskandidat der Opposition
Bobi Wine akipiga kura siku ya Alhamisi Picha: Jerome Delay/dpa/AP/picture alliance

Kulingana na Mwandishi Habari wa DW mjini Kampala, Bobi Wine anatazamiwa kupata uungaji mkono mkubwa wa wapigakura wa mji huo mkuu na matokeo ambayo bado hayajajumuishwa kwenye mji huo yanaashiria mwanasiasa huyo atampiku rais Museveni.

Tume ya Uchaguzi ya Uganda itachapisha matokeo mengine katika saa chache zinazokuja huku mshindi wa kiti cha urais anatarajiwa kutangazwa siku ya Jumamosi au Jumapili.

Majimboni mchuano ni mkali kati ya chama tawala na Upinzani

Kinyang´anyiro kingine kwenye uchaguzi huo ni nafasi za ubunge ambakoupinzani unatumai kutoa changamoto kubwa kwa wagombea wa chama tawala NRM.

Katika eneo la magharibi mwa Uganda uliko mji wa Hoima na ziwa Albert, wagombea wasiopungua sita wa upinzani wanaongoza katika kura zilizokwishahesabiwa dhidi ya wale wa chama tawala.

Uganda Kampala | Präsidentschaftswahl: Wahlplakate
Chama tawala cha rais Museveni, NRM, kinakabiliwa na upinzani mkali Picha: Sumy Sadurni/AFP/Getty Images

Kwa miaka mingi, eneo hilo halijawahi kuwa na mbunge kutoka chama cha upinzani isipokuwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016, wanasiasa wawili waliojiengua kutoka chama tawala NRM waliwania nafasi za ubunge kama wagombea binafsi na kuibuka na ushindi.

Kwa sehemu kubwa, matokeo kamili ya nafasi za ubunge yanatarajiwa kutangazwa leo Ijumaa na kutoa picha kamili ya uwakilishi katika Bunge linalokuja.

Duru kutoka miji kadhaa ya nchi hiyo zinasema kumekuwa na hali ya utulivu huku polisi na wanajeshi wakishika doria kwenye mitaa yenye makaazi ya watu.