Museveni aapishwa kwa muhula wa tano | Matukio ya Afrika | DW | 12.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Museveni aapishwa kwa muhula wa tano

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameapishwa siku ya Alhamisi kuongoza mhula mwingine wa miaka mitano, huku kiongozi wa mkuu wa upinzani Kiiza Besigye akikamatwa na mitandao ya kijamii kuzimwa.

Rais Museveni mwenye umri wa miaka 71, ambaye ameitalwa Uganda tangu 1986, alichukuwa asilimia 60 ya kura katika uchaguzi mkuu uliyofanyika mwezi Februari. " Waganda wamekuwa wakishiriki uchaguzi wa vyama vingi kwa miaka kadhaa sasa na katika uchaguzi wa mwisho alieshinda ni mgombea Museveni na ndiyo maana anaapishwa hii leo," alisema Badru kiggundu, mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini Uganda.

Chama kikuu cha upinzani cha Forum for Democratic Change FDC, ambacho kinasema matokeo ya uchaguzi huo yalichakachuliwa, siku ya Jumatano kilifanya hafla yake ya siri ya kumuapishwa mgombea wake Kizza Besigye, ambayo ilisambaa kwenye mtandao wa Youtube.

Besigye amkuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu ulipomalizika uchaguzi huo, kulingana na msemaji wa aFDC Ibrahim Semuju Nganda. Polisi inasema uzuwiaji huo unalenga kuhakikisha besigye hatendi makosa. Baada ya vidio ya kuapishwa kwake kutolewa, Besigye aliwapiga chenga walinzi wake na kuingia mitaani, hatua iliyolilaazimu jeshi la polisi kumkamata.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli akiwasili viwanja vya Kololo kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Museveni.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli akiwasili viwanja vya Kololo kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Museveni.

Besigye kushtakiwa kwa kukaidi "amri halali"

"Alikuwa anaongoza kundi la watu kuvuruga amani," alisema Patirick Onyango, msemaji wa jeshi la polisi na kuongeza kuwa, "tutamshitaki kwa kukaidi amri halali." Wanachama wengine wa upinzani pia walikamatwa kuelekea kuapishwa kwa Museveni, kwa mujibu wa duru kutoka upande wa upanzani.

Siku ya Jumatano serikali iliizima mitandao ya kijamii ya Facebook, twitter na WhatsApp, ambapo watumiaji walishindwa kuingia kwenye akaunti zao za mitandao hiyo. Msemaji wa mamlaka ya udhibiti wa mawasiliano ya Uganda, UCC alikamataa kuzungumzia hatua hiyo.

Polisi wa kuzuwia fujo walisambazwa katika maeneo mengi ya mji wa Kampala ambako maduka mengi yalisalia kufungwa, baada ya hapo Jumatano kuwatembezea kichapo wakaazi waliompungia mikono Kizza Besigye.

Miongoni mwa viongozi wa Kiafrika waliohudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Museveni ni pamoja na rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir, anaetafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kwa makosa ya uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur. Museveni amepuuza wito wa kukamatwa kwa al-Bashir, akiitaja ICC kuwa kundi la watu wasio na maana.

Ingawa viongozi wa Afrika awali walikaribisha hatua ya kuanzishwa kwa mahakama ya ICC, walikuja kuigeuka pale ilipoanza kujaribu kuwawajibisha. Wakati Museveni akiitaja ICC kuwa kundi la watu wasio na maana, rais al-Bashir alikuwa akitikisa kichwa katika ishara ya kukubaliana naye.

Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir akiwasili viwanjani kuhuduria sherehe ya kuapishwa Museveni.

Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir akiwasili viwanjani kuhuduria sherehe ya kuapishwa Museveni.

Aishukuru Urusi kwa mauzo ya silaha bila masharti

Museveni pia aliishukuru Urusi kwa utayarifu wake kuiuzia Uganda silaha, "bila masharti na jeuri kama mataifa mengine," na kuahidi kuanzisha vita dhidi ya rushwa. " Ukiniona nimevaa tai unasahau kuwa niliwahi kuwa muasi?" aliuliza.

Viongozi wa mataifa ya Chad, Ethiopia, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Tanzania na Zimbabwe pia walihudhuria sherehe hiyo. Baada ya kuapishwa kwake, Museveni aliendelea kusimama kwenye jukwaa nyumba ya bilauri zisizopitisha risasi, na kukabishiwa zana kadhaa za mamlaka, zikiwemo mhuri wa rais na benedera ya taifa.

Baadae bendi za jeshi zilitumbuiza, na mizinga 21 ilifyatuliwa, wanajeshi wakafanya gwaride na ndege za kivita zilifanya maonesho angani huku makundi ya waliohudhuria yakitazama.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza