1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MUNICH: Rais wa Russia, Vladmir Putin ashutumu harakati za kijeshi za Marekani.

10 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCTR

Rais wa Russia, Vladmir Putin, amesema tabia ya Marekani kuendelea kutumia nguvu za kijeshi imesababisha harakati mpya za mataifa kuwania kutengeneza silaha.

Rais Vladmir Putin alikuwa akizungumza katika mkutano wa kila mwaka wa usalama wa kimataifa mjini Munich, Ujerumani.

Rais huyo wa Russia alisema harakati za kijeshi za Marekani zinachochea mataifa madogo kuanzisha miradi ya silaha za kinyuklia.

Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel, amefungua mkutano huo kwa hotuba iliyoashiria kwamba jumuiya ya kimataifa imepania kuizuia Iran kuendelea na mpango wa kutengeza silaha za kinyuklia.

Bibi Angela Merkel alisema Iran inapaswa kutekeleza masharti yote iliyowekewa na Umoja wa Mataifa.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates anahudhuria mkutano huo.

Msuluhishi mkuu wa mradi wa kinyuklia wa Iran, Ali Larijani, ni miongoni mwa wakuu zaidi ya arobaini wa kisiasa wanaohudhuria kikao hicho.

Iran imeshikilia kwamba mradi wake wa nishati ya kinyuklia ni wa amani ingawa mataifa mengine yanayatilia shaka madai hayo yakisema nchi hiyo imepania kutengeneza silaha za kinyuklia.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, na mkuu wa sera wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, wanatarajiwa kuwa na mashauriano yasio rasmi kati yao na Ali Larijani kuhusu mradi wa Iran wa nishati ya kinyuklia.