Mumbai yagubikwa na milipuko | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 27.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mumbai yagubikwa na milipuko

Maafisa wa kijeshi nchini India wanaendelea na shughuli ya kuondoa maiti za watu waliouawa kwenye hoteli mbili za kifahari zilizoko mjini Mumbai kufuatia mashambulio ya bomu hapo jana usiku.

Hoteli ya Taj iliyoshambuliwa kwa mabomu mjini Mumbai

Hoteli ya Taj iliyoshambuliwa kwa mabomu mjini Mumbai


Taarifa zinaeleza kuwa yapata watu 100 wamepoteza maisha yao na wengine 300 kujeruhiwa.Wakati huohuo nchi jirani ya Pakistan imelaani shambulio hilo na kuahidi kutoa ushirikiano kamili katika vita dhidi ya ugaidi.


Ni saa 15 tangu shambulio hilo kutokea na zaidi ya watu 100 bado wamenasa katika hoteli ya kifahari ya Taj Mahal vilevile hoteli ya Trident Oberoi.Maafisa wa kijeshi na polisi waliojihami kwa silaha wanaripotiwa kuzingira majengo hayo.


Kwa mujibu wa afisa mmoja wa serikali Pradeep Indulkar baadhi ya waliokufa ni pamoja na raia mmoja wa Australia,Japan na Uingereza.Wapiganaji wanane wanaripotiwa kuuawa katia shambulio hilo.Hata hivyo uongozi wa jimbo la Maharashtra umesisitiza kuwa hali ya usalama imeimarishwa kufuatia tukio hilo.Vhushan Gagrani ni msemaji wa jimbo la Maharashtra anaeleza kuwa hali iko shwari.

''Maeneo yote tisa yaliyoshambuliwa yamedhibitiwa kwa sasa.mapigano yaliyoendelea usiku kucha katika hoteli za Taj na Oberoi sasa yamesitishwa.Watu waliofariki ni takriban 84 na yapata 200 wamejeruhiwa''


Wapiganaji hao waliojihami kwa silaha nzito walivamia hoteli mbili za kifahari,mkahawa mmoja maarufu,kituo cha treni pamoja na kituo kimoja cha wafuasi wa Kiyahudi.Mpaka sasa kundi moja la kiislamu Deccan Mujahideen limekiri kuhusika na shambulio hilo .


Itakumbukwa kuwa jengo la Taj Mahal lililojengwa miaka 105 iliyopita ni alama muhimu nchini humo.

Mlipuko mkubwa ulisikika kwenye hoteli iliyo karibu ya Trident-Oberoi muda mfupi baada ya shambulio la hoteli ya Taj Mahal.

Guam Patel mgeni kwenye hoteli hiyo alishuhudia tukio hilo na anasimulia kuwa

''ali kuwa kwenye ghorofa ya 11 nikipiga simu.Punde nilisikia kele na mishindo miwili mikubwa niliyodhani ilitokea humo chumbani !Hapo ndipo nikabaini kuwa jambo baya limetokea.Nilipotazama nje niliuona mkahawa uliokuwa karibu unawake moto.Tulilazimika kuvihama vyumba vyetu ndipo wahudumu wa hoteli wakatuambia tuondoke na kukusanyika kwenye ukumbi maalum.''


Mashambulio hayo yaliyotokea kwenye eneo la kibiashara la Mumbai huenda yakawashtua wawekezaji katika nchi iliyo na uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa barani Asia.Mumbai imeshashambuliwa kwa mabomu awali ila shambulio la jana ni jambo ambalo halijapata kushuhudiwa kwani liliwalenga zaidi raia wa kigeni.


Uongozi nchi humo umeagiza masoko ya hisa kufungwa japo Benki Kuu inaendelea na shuguli zake ili kuhakisha mzunguko wa fedha hauathiriki.Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo washambuliaji hao walikuwa vijana walio na asili ya Asia Kusini waliokuwa na umri wa miaka 20 na kitu na walikuwa wanazungumza kugha za kiHindi au Urdu.


Shambulio hilo limeitia doa sifa ya serikali inayoongozwa na chama tawala cha Congress huku uchaguzi mkuu ukisubiriwa kufanyika mwaka 2009.Chama hicho kwa sasa kinakabiliwa na shutma nyingi za kushindwa kudhibiti usalama nchini humo.

Shule zinaripotiwa kufungwa japo huduma za treni zinaendelea kama kawaida.

Marekani imelaani vikali shambulio hilo pamoja na Umoja wa Ulaya na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.

Rais wa Nchi jirani ya Pakistan Asif Ali Zardari pamoja na Waziri Mkuu Yousaf Raza Gilani wamelaani vikali mashambulio hayo na kuahidi kutoa ushirikiano katika vita dhidi ya ugaidi.


India imekuwa ikiilaumu Pakistan kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa kiislamu wanaopambana na wanajeshi wa India kwenye eneo la Kashmir. • Tarehe 27.11.2008
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/G31Y
 • Tarehe 27.11.2008
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/G31Y
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com