Mugabe atimuliwa kama kiongozi wa ZANU-PF | Matukio ya Afrika | DW | 19.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mugabe atimuliwa kama kiongozi wa ZANU-PF

Rais Robert Mugabe ametimuliwa kama kiongozi wa chama tawala nchini Zimbabwe – ZANU-PF katika hatua ya kulazimisha kufikishwa kikomo miaka yake 37 madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi

Nafasi yake imechukuliwa na Emmerson Mnangagwa, naibu wake ambaye alimfuta kazi mwezi huu. Hayo ni kwa mujibu wa duru katika mkutano maalum wa ZANU-PF ulioandaliwa leo kuamua hatima ya Mugabe. Mke wa Mugabe, Bi Grace Mugabe, ambaye alikuwa na mipango ya kumrithi mumewe, pia ametimuliwa chamani.

Muda wa yeye kujiuzulu ni Jumatatu 20.11.2017 saa sita za mchana, lasivyo chama kitaanzisha mchakato wa kumvua madaraka bungeni. Chama cha ZANU-PF kimesema kuwa Mnangagwa atarejeshwa chamani kama kama kaimu kiongozi. Hoja ya kumuondoa Mugabe ilipokelewa kwa shangwe na vifijo na wajumbe wa mkutano

Akizungumza kabla ya mkutano huo wa leo, kiongozi wa chama cha maveterani wa kivita Chris Mutsvangwa amesema Mugabe ambaye ana umri wa miaka 93,  anaishiwa na muda  wa kufanya mazungumzo ya kuondoka kwake na anapaswa kuondoka nchini humo mapema iwezekanavyo.

Mutsvangwa amefuatisha na kitisho cha kuitisha maandamano kama Mugabe atakataa kuondoka, akiwaambia wanahabari kuwa "tutarejesha waandamanaji na watafanya shughuli yao”. Mnangagwa, kiongozi wa zamani wa usalama wa taifa, anayefahamika kama "mamba”, sasa ndiye anaonekana atakayeongoza serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa baada ya kuondoka Mugabe ambayo itaangazia kujenga upya mahusiano na ulimwengu wan je na kuuokoa uchumi ambao unashuka kwa kasi.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Yusra Buwayhid