1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muda wa kuondoka vikosi vya kigeni nchini Libya wamalizika

Zainab Aziz Mhariri:Tatu Karema
24 Januari 2021

Muda wa mwisho wa kuondoka kwa vikosi vya kigeni kutoka nchini Libya ulimalizika mnamo siku ya Jumamosi lakini hakukuwepo na dalili yoyote kwamba askari hao walikuwa wanajiandaa kuondoka.

https://p.dw.com/p/3oLMn
Libyen Proteste gegen Haftar-Truppen in Tripolis
Picha: Hazem Turkia/AA/picture alliance

Mnamo Oktoba 23, pande hasimu nchini Libya zilifikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye mazungumzo yaliyofanyika mjini Geneva, Uswisi. Makubaliano hayo yalijumuisha tarehe ya mwisho ndani ya miezi mitatu ya kuondolewa vikosi vya askari wa kigeni na mamluki.

Libya imekuwa katika machafuko tangu alipopinduliwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011 na imegeuka kuwa uwanja wa mapambano kati ya makundi yanayopingana ambayo yanaungwa mkono na nchi za kigeni. 

Uturuki inaiunga mkono Serikali ya mjini Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa na imewapeleka wanajeshi na vifaa vya vita kuisaidia serikali hiyo kupambana na majeshi hasimu yaliyoko mashariki mwa Libya na yanayoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Urusi, Misri na Umoja wa nchi za Kiarabu.

Soma zaidi: UN: Libya ina wapiganaji 20,000 wa kigeni na mamluki.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umesema katika taarifa yake kwamba unasisitiza juu ya utekelezaji wa makubaliano ya tarehe 23 Oktoba mwaka uliopita na umewataka viongozi wa Libya kuharakisha utekelezaji wa hatua za kusitisha mapigano, pamoja na kuwarudisha nyumbani askari wote wa kigeni pamoja na mamluki.Katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na juhudi za kila aina za kimataifa zenye lengo la kuumaliza mzozo wa nchini Libya.

Mkutano wa amani ya Libya nchini Tunisia
Mkutano wa amani ya Libya nchini TunisiaPicha: Yassine Gaidi/AA/picture alliance

Wakati huo huo wajumbe kutoka serikali ya umoja wa kitaifa GNA yenye makao yake mjini Tripoli na wawakilishi wa upinzani wa bunge lenye makao yake mashariki mwa Libya wamesema walifikia makubaliano mnamo siku ya Jumamosi juu ya kujaza nafasi muhimu katika serikali hatua iliyofikiwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika nchini Morocco. Nafasi hizo ni pamoja na ya gavana wa benki kuu ya Libya, mkuu wa idara ya kupambana na rushwa na mkuu wa tume ya uchaguzi.

Soma zaidi:Mkutano wa Majadiliano wa Libya washindwa kufikia makubaliano ya serikali

Taarifa ya pamoja ya wawakilishi kutoka kambi hasimu za nchini Libya imesema mchakato huo wa uteuzi wa nafasi hizo muhimu utafunguliwa siku ya Jumanne. Mchakato huo, unatarajiwa kuendelea hadi Februari 2. Libya inakusudia kujaza nafasi hizo ili kuwezesha ushirikiano na uongozi wa muda utakaochochaguliwa wiki ijayo huko Geneva.

Katika mazungumzo tofauti yaliyofanyika mjini Geneva mapema wiki hii, wawakilishi wa Libya walipiga kura kupitisha utaratibu wa kumchagua kiongozi wa muda atakayeshikilia madaraka hadi utakapofanyika uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 24.

Mazungumzo mengine yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yaliyofanyika nchini Misri katikati ya wiki iliyopita, wajumbe hao wa Libya walikubaliana kuandaa kura ya maoni kwa mujibu wa kikatiba kabla ya uchaguzi huo wa Desemba.

Vyanzo:/DPA/AFP