1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muda unayoyoma kwa vyama vinne Ujerumani kuafikiana

Saumu Mwasimba
16 Novemba 2017

Kila chama kati ya Vinne vilivyoko kwenye mazungumzo kinajitutumua kuonesha nguvu zake na kushikilia msimamo katika masuala muhimu yaliyo kizingiti

https://p.dw.com/p/2nl6t
Deutschland Jamaika-Koalition Sondierungsgespräche | Die Grünen - Özdemir & Göring-Eckardt
Picha: Reuters/A. Schmidt

Kwa kipindi cha wiki kadhaa vyama vinavyotafuta msimamo wa pamoja kuunda serikali ya mseto nchini Ujerumani vimekuwa katika mikutano.Kinachoonekana hadi sasa ni kama mchezo wa kamari ya mashindano  ya kushikilia misimamo na kuoneshana nguvu.Lakini shinikizo la muda siku zote sio msingi mzuri wa mazungumzo anasema mtaalamu wa masuala ya mawasiliano Thorsten Hofmann ambaye amezungumza na DW.

Uchaguzi nchini Ujerumani ulifanyika tarehe 24 ya mwezi Septemba na kimsingi ilitakiwa ifikapo sikukuu ya Krismasi kuwepo tayari na serikali mpya  ya mseto inayofahamika kama serikali ya Jamaika kutokana na uwiano wa rangi za vyama vinne vinavyotarajiwa kuunda serikali Ujerumani.Lakini kufikia wakati huu hakuna chochote kilichoafikia na vyama hivyo katika vikao vyao.Je nikusema kwamba kila jambo muhimu linahitaji kuchukuwa muda mrefu?Thorsten Hofmann anasema kwahakika ni kweli kila jambo muhimu mara nyingi hukawia muda mrefu lakini pamoja na hayo kinachoshuhudiwa nchini Ujerumani ambacho ni kitu kipya ni kwamba kuna vyama vinne vinavyojadiliana kwa pamoja kwa nia ya kufikia mwafaka wa kuelekea kuunda serikali ya mseto pamoja.

Deutschland Jamaika-Koalition Sondierungsgespräche | Merkel & Seehofer, UNION
Kansela Merkel wa CDU na kiongozi wa CSU SeehoferPicha: Reuters/A. Schmidt

Vyama vyote hivyo vinne vilikuwa katika mapambano makali ya kuwania kura katika uchaguzi  uliopita na kila upande ulipigania kwa dhati kupata kura.Ndio sababu  katika mazungumzo hayo yaliyowakutanisha mwanzo kabisa yalikuwa yanakwenda kwa tahadhari,na mtu anaweza kusema kwamba yalikuwa ni mazungumzo ya kujaribu kutafuta maridhiano.

Katika kampeini za uchaguzi  peke yake kuna wengi walioumizwa kwa maneno katika kile kilichoonekana wakati mwingine kuwa kama kwa sehemu yalikuwa mashambulizi ya kibinafsi.Na hapo hapo ni watu haohao waliokwaruzano kwenye kampeini kwa hali zote walitakiwa kukaa pamoja kujadiliana  si tu kuhusu kufikia lengo la pamoja lakini pia kukaa pamoja na kufanya kazi pamoja.Hii inamaanisha palikuwa na umuhimu mkubwa sana kwa watu hawa kwanza kujenga hali ya mjongeleano na kwa maana hiyo sio tu muda ulihitajika a kutosha  kwa ajili ya mazungumzo lakini muda mrefu pia ulihitajika kujenga mahusiano mema na  hali ya kuaminiana.

Deutschland Jamaika-Koalition Sondierungsgespräche | Symbolbild Medien
Picha: Reuters/A. Schmidt

Pamoja na sarakasi,vishindo na mihemko kuongezeka, je kwa kiasi fulani haionekani kama kichekesho wakati mwisho wa siku takriban yale yote muhimu wa kuyaamua ni Kansela? Na kama kweli ni hivyo kwamba muamuzi ni Kansela basi hakuna haja ya mazungumzo kwasababu siku zote mambo ya msingi katika mikutano hiyo huibua migogoro.Kila chama kina maslahi yake tafauti ni mwenzake.

Na hili haswa ndio tatizo linalomuweka njia panda hata Kansela Merkel.Na kinachoshuhudiwa sasa ni kile kinachoitwa  mapambano ya pande tatu katika mkutano mmoja.Kwanza yameanza kujadiliwa yale yanayopendekezwa  halafu ukaanza mchakato,suali ni je wapi mazungumzo hayo yanakoelekea na ikiwa tatu bado kuna haja ya vikao hivyo kufafanuliwa.

Hapa pia ndipo yatakapojitokeza mengi na hasa pale yatakapoanza kufululiza mahojiano na waandishi habari kwa vyama hivyo vilivyoshiriki mazungumzo.   Yote hayo hapana shaka yataanza kuibua minong'ono katika kumbi za majengo ya bunge na hata wakati mwingine miongoni mwa wanachjama wa vyama hivyo hivyo. Pamoja na yote lakini muda ndio utakaoamua mbivu na mbichi katika suala la kupatikana mwafaka na hatimae kuundwa serikali ya mseto katika ya vyama vinne nchini Ujerumani,CDU/CSU,FDP,na Die Grune au walinda mazingira.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/Wagener,Volker

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman

Source:DW-Interview-Haus