Mubaraka kufikishwa mahakamani Agosti | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mubaraka kufikishwa mahakamani Agosti

Akipatikana na hatia huenda akapewa adhafu ya kifo !

default

Waliomwangusha Mubarak walipokuwa kwenye uwanja wa Tahrir mjini Cairo.

Aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak anatazamiwa kufikishwa mbele ya mahakama mnamo mwezi wa Agosti kujibu tuhuma za kuwaua waandamanaji. Ikiwa atapatikana na hatia Mubarak anaweza kupewa adhabu ya kifo.

Mubarak alieng'olewa madarakani kutokana na mapinduzi ya umma aliamrishwa jana kusimama kizimbani mnamo mwezi wa agosti ili kujibu tuhuma zinazomkabili juu ya kuwaua waandamanaji. Kiongozi huyo wa zamani alietawala nchini Misri kwa muda wa miaka 30 amehojiwa juu ya jinsi alivyohusika katika kampeni ya kuwazima waandamanaji ambapo mia nane waliuawa. Mubarak pia anakabiliwa na tuhuma za rushwa.

Wanawe wawili pia watasimamishwa kizimbani kujibu tuhuma; Gamal aliekuwa anatayarishwa kuurithi uongozi wa baba yake na mwengine ni Alaa. Hakimu Sayed Abdel Azim,ambae ni Mkuu wa Mahakama ya Rufani amearifu kuwa kesi ya Mubarak na wanawe itaanza tarehe tatu mwezi wa Agosti mjini Cairo.

Adhabu ambayo Mubarak anaweza kupewa ikiwa atapatikana na hatia ya mauaji ya waandamanaji ni ya kifo.

Baadhi ya Wamisri wanasema kuwa Mubarak anastahili adhabu ya kifo. Mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa Dr. Hassan Abu Taleb kutoka chuo cha Al Ahram cha mjini Cairo amesema Mubarak anastahili adhabu ya kifo,na asilani asiruhusiwe kuikwepa adhabu hiyo. Hata hivyo wanaharakati wanaotetea haki za binadamu wanasema kuwa Mubarak pia anastahili kufanyiwa kesi katika msingi wa haki.

Lakini Mwenyekiti wa Baraza la Misri la haki za binadamu Fouad Riad amesema yapo mambo mengine muhimu zaidi kwa sasa. Amesema maadui wakubwa kwa watu wa Misri sasa ni njaa na umasikini. Kwa hiyo ameeleza kuwa mkazo unapaswa kuwekwa katika kuleta mandeleo ya haraka.

Hata hivyo mwendesha mashtaka wa serikali amesema Mubarak hana uzima wa kuweza kupelekwa jela ya hospitali na kwamba kwa sasa ataendelea kuwekwa kwenye kituo maalumu cha afya kilichopo kwenye kitongoji cha burudani cha Sharm el Sheikh.

Mubarak ambaye sasa na umri wa miaka 83 alilazwa hospitali akiwa na matatizo ya moyo,mara tu baada ya kuhojiwa na idara za sheria. Marekani imesema inatumai Mubarak atafanyiwa kesi ya haki.

Pamoja na tuhuma zinazomkabili kiongozi huyo wa zamani wa Misri ni kuua kwa kudhamiria,kutumia mamlaka vibaya, ubadhirifu wa fedha za umma na kujitajirisha kinyume cha kisheria.

Mwandishi/Durm, Martin/ARD/ZDF/

Tafsiri/Mtullya Abdu/

Mhariri/ Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com