Mubarak ajitetea kwa masikitiko | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mubarak ajitetea kwa masikitiko

Mahakama ya Misri itatangaza hukumu ya kesi dhidi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak mnamo Septemba 27.

Tangazo hilo la Mahakama limekuja baada ya kiongozi huyo wa zamani kusimama kizimbani hii leo na kutoa ushahidi wake wa kujitetea katika kesi hiyo ya mauaji dhidi ya waandamanaji waliokuwa wanaupinga utawala wake.

Hosni Mubarak ameonekana kujitetea kwa hisia ya huruma kabisa akiwa mahamani hii leo akisema ndani ya kipindi cha miaka 30 ya Utawala wake hakuna kibaya alichokifanya zaidi ya kutetea maslahi ya taifa lake.Katika hotuba yake mahakamani alijieleza kwa urefu akitetea rekodi yake madarakani akijisifia tangu alipokuwa afisa wa kijeshi hadi siku zake za mwisho madarakani Februari mwaka 2011.

Aliiingia mahakamani akisukumwa katika kiti cha magurudumu huku akiwa amevalia sare za rangi ya kibuluu kuonyesha ameshastakiwa katika kesi nyingine inayohusiana na masuala ya rushwa mapema wiki hii.Kwa kiasi kikubwa hotuba yake ya kujitetea mahakamani mjini Cairo,ilijikita katika kile alichosema ni mafanikio ya miongo mitatu ya utawala wake akisema kwamba ni utawala ulioleta mafanikio makubwa ya ukuaji wa kiuchumi katika historia ya Misri.

Aidha Mubarak amejitetea dhidi ya kuhusika na rushwa katika kesi nyingine inayomkabili pamoja na watoto wake wawili wa kiume ambao pia hukumu ya kesi dhidi yao itatolewa Septemba 27.Mubaraka ameonekana kuzungumza kwa masikitiko na hisia kali aliposema kwamba, hii huenda ikawa hotuba yangu ya mwisho kwasababu umri wangu unakaribia kufika kikomo hapa duniani,Namshukuru mwenyezimungu nina dhamiri njema na nimeridhika nimeitumia dhamiri hiyo kuitetea Misri.'

'

uwanja wa Rabia-al-Adawiya

uwanja wa Rabia-al-Adawiya

Pamoja na hayo amesema hakuwahi hata mara moja kuagiza waandanaji wauwawe.Wamisri waliowengi waliuoukosoa kwa kiasi kikubwa utawala wa Mubarak pamoja na vikosi vyake vya polisi ambavyo vitendo vyao vya mateso na unyanyasaji dhidi ya raia vilichochea vuguguvu la mwaka 2011 lakini baada ya miaka minne ya vurugu tangu alipoangushwa madarakani wengi sasa wanaukumbuka utawala wake.Itakumbukwa kwamba aliyemrithi madaraka Mohammed Mursi aliangushwa madarakani na jeshi mnamo mwezi Julai mwaka 2013 baada ya utawala wake wa mwaka mmoja kukabiliwa na misukosuko.

Kuondolewa kwake kuliibua wimbi la ghasia na umwagikaji mkubwa wa damu uliosababisha watu 1,400 kuangamia wengi wakiwa ni wafuasi wa udugu wa kiislamu.Tangu wakati huo Vuguvugu ambalo lilipongezwa na kuonekana kama mapinduzi yaliyopata umaarufu kwa kumuondoa Mubarak,yaligeuka na kuendelea kutajwa na maafisa wa serikali pamoja na vyombo vya habari vya ndani ya Misri kama njama zilizohusisha mataifa yenye nguvu pamoja na wanamgambo.Aliyekuwa waziri wa ndani Habib al-Addly akizungumza mahakamani katika hotuba pia ya kujitetea dhidi ya mashtaka ya kuua yanayomkabili alisema kuondolewa kwa Mubarak Madarakani ilikuwa ni njama iliyopangwa na Marekani pamoja na nchi nyingine zenye nguvu.Na zaidi mauaji ya waandamanaji katika vuguguvu la mwaka 2011 yalifanywa na kundi la Hamas la Gaza pamoja na Udugu wa Kiislamu.

Mwandishi: Saumu Yusuf

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com