Mualjeria Riyad Mahrez mchezaji bora Afrika | Michezo | DW | 06.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Mualjeria Riyad Mahrez mchezaji bora Afrika

Mshambuliaji wa Aljeria Riyad Mahrez ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika wa mwaka baada ya kuiwezesha klabu yake ya Leicester City kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza msimu uliopita.

Mahrez mwenye umri wa miaka 25, alimpiku nahodha wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang, aliyenyakua tuzo hiyo mwaka jana, na nyota wa Senegal Sadio Mane anayechezea Liverpool. Aubameyang ameshika nafasi ya pili, huku Mane anayechezea klabu ya Liverpool akishika nafasi ya tatu.

Mahrez ambaye ni mzaliwa wa Ufaransa amesema kuwa, imekuwa ni heshima kwake kutangazwa kuwa mchezaji bora barani Afrika wa mwaka huu.

"Hii ni heshima kubwa, nimefurahi na nimeridhishwa. Nawashukuru wachezaji wenzangu wa Leicester na Algeria alisema Mahrez wakati alipokuwa akipokea tuzo na kuongeza kuwa " ninaitoa tuzo hii kwa familia yangu na kwa wote ambao wananiunga mkono kila siku"

Klabu ya Leicester city iliushangaza ulimwengu wakati ilipoweza kunyakua ubingwa wa Premier msimu uliopita. Mshambuliaji huyo ambaye kipaji chake kilianza kuchomoza wakati akiwa na klabu yake ya nyumbani aliipatia wafuasi wengi nyumbani klabu ya Leicester, ambayo awali aliidhania kuwa timu ya mchezo wa raga walipowasiliana naye kumtaka ajiunge nao miaka minne iliyopita.

Mahrez ametoa mchango mkubwa katika klab yake ya Leicester City  kwa kuifungia magoli 17, na pia kutoa mchango katika mabao 10 ya timu hiyo katika mechi 37 alizochezea. Mshambuliaji huyo anabaki kuwa mchezaji pekee hadi sasa wa Algeria kushinda kikombe cha ligi kuu ya kandanda ya England.

Fußball Leicester City Spieler Riyad Mahrez (Getty Images/S. Forster)

Mshambuliaji Riyad Mahrez wa Leicester city akiwa na Sebastian Larsson wa Sunderland.

Ushindi wake unahitimisha ukame wa tuzo hizo wa miaka 19 kwa wachezaji wanaotokea Afrika ya Kaskazini tangu  Mustapha Hadji wa Morocco alishinda tuzo hiyo ya mchezaji bora wa Afrika wa mwaka mnamo mwaka 1998.

Wachezaji wengine kuwahi kushinda tuzo hiyo ni Rabah Madjer aliyeshinda tuzo hiyo mnamo mwaka 1987 na Lakhdar Belloumi aliyeshinda taji hilo mwaka 1981.

Wachezaji wote watatu waliokuwa wamependekezwa kuwania tuzo hiyo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika, waliteuliwa pia kuunda kikosi cha wachezaji kumi na moja kinachounda timu kamili ya shirikisho la kandanda barani Afrika CAF, ambayo pia inaundwa na mlinzi wa Cote Di Ivoire Eric Bailly anayeisukuma kabumbu katika klabu ya Manchester United.

Mlindamlango Denis Onyango alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mwaka barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza barani Afrika, akimshinda Khama Billiat wanaecheza pamoja katika klabu ya Mamelod Sundowns na Mzambia Rainford Kalaba.

Onyango alitoa mchango mkubwa wakati mabingwa mara saba nchini Afrika Kusini Mamelod Sundowns walipofanikiwa kushinda ubingwa katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika, na pia akiiwezesha Uganda ambayo imechaguliwa kufuzu fainali za mwaka huu za mataifa barani Afrika.

Ama kwa upande mwingine Asisat Oshoala wa Nigeria alijinyakulia kwa mara ya pili tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika kwa upande wa wanawake.

Oshoala ambaye pia anaichezea timu ya soka ya wanawake ya Arsenal alishinda tuzo hiyo mara ya kwanza wakati alipoiwezesha timu ya wanawake ya Nigeria kuibuka mabingwa wa Afrika kwa wanawake mnamo mwaka 2014.

Kelechi Iheanacho na Alex Iwobi wote kutoka Nigeria walishinda tuzo ya mchezaji bora  kijana anayechipukia wakati mwamuzi Bakary Gassama wa Gambia akishinda kwa mara ya tatu mfululizo kama mwamuzi bora barani Afrika.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com