1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa mkuu wa mauwaji ya wataalamu wa UN akamatwa Congo

Saleh Mwanamilongo
1 Juni 2020

Tresor Mputu Kankonde alikamatwa nje kidogo ya mji wa Kananga, ambao ni mji mkuu wa jimbo hilo la Kasai ya Kati.Kukamatwa huko kumepongezwa na mashirika ya kiraia,mabalozi wa Marekani na Umoja wa Ulaya mjini Kinshasa. 

https://p.dw.com/p/3d6TL
Zaida Catalan mtaalam wa Umoja wa Mataifa alieuliwa na mwenzie Michael Sharp,mwezi Machi 2017 jimboni Kassai ya kati, katikati mwa DRC.
Zaida Catalan mtaalam wa Umoja wa Mataifa alieuliwa na mwenzie Michael Sharp,mwezi Machi 2017 jimboni Kassai ya kati, katikati mwa DRC.Picha: Getty Images/AFP/B. Ericson

Mtuhumiwa mkuu katika mauwaji ya wataalam wawili wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo amekamatwa. Mwendesha mashtaka wa kijeshi kwenye jimbo la Kasai ya Kati, amesema kwamba Tresor Mputu alianguka katika mtego wa idara ya ujasusi baada ya kusakwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Kukamatwa huko kumepongezwa na mabalozi wa Marekani na Umoja wa Ulaya mjini Kinshasa. 

Gavana wa jimbo la Kassai ya Kati, Martin Kabuya ,ameimbia DW kwa njia ya simu kwamba kukamatwa kwa Tresor Mputu Kankonde ni muhimu kwa kuendeleza kesi ya mauaji dhidi ya wataalam hao wa Umoja wa Mataifa. Kankonde ni mmoja wa viongozi wa kundi la wanamgambo la Kamuina Nsapu ambaye alikuwa mafichoni kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kusakwa na viombo vya dola nchini Congo. Kankonde alikamatwa nje kidogo ya mji wa Kananga, ambao ni mji mkuu wa jimbo hilo la Kasai ya Kati. Duru za kiusalama zinaelezea kwamba wakati wa kukamatwa kwake, Kankonde alikuwa akijaribu kupanga tena wanamgambo wa kundi la Kamuina Nsapu kwa lengo la kuushambulia mji wa Kananga kutoka mji wa Kasuyi.

Mputu Kankonde kufikishwa mahakamani hivi karibuni

Mwendesha mashtaka wa kijeshi kutoka Kananga, Jean-Blaise Kuzola, amesema kwamba  mashuhuda wengi wanamuona Kakonde kama sehemu muhimu katika kutafuta ukweli juu ya kuuwawa kwa wataalam wawili wa Umoja wa Mataifa, Zaïdan Catalan na Michael Sharp mwezi Machi 2017, kwenye kijiji cha Bunkonde karibu na mji wa Kananga. Mashirika ya kiraia yamepongeza hatua ya kukamatwa kwa mshukiwa mkuu wa kesi hiyo. Dieudonne Mushagalusa ni mratibu wa mashirika ya Kiraia mjini Kinshasa.

''Tumepongeza sana hatua hiyo. Sisi kama mashirika ya kiraia tumeomba kwamba haki itendeke,pili sheria ichukuwe mkondo wake na tatu ni kwamba adhabu kali itolewe kwa wale haliohusika na mauwaji hayo na vilevile fidia kwa wathiriwa''.

Kongo Kananga Tshimbulu MONUSCO
Picha: Reuters/A. Ross

Balozi wa Marekani mjini Kinshasa, Mike Hammer amesema kwamba kukamatwa huko kwa kiongozi wa kundi la Kamwina Nsapu ni hatua muhimu katika kutekelezwa kwa sheria na Marekani itaunga mkono juhudi za Congo na Umoja wa Mataifa ilikufikia ukweli wa mauwaji hayo.

Kwa upande wake balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Congo, Jean-Marc Châtaigner amepongeza kukatwa kwa mshukiwa huyo akielezea kwamba hatua hiyo itaruhusu kuendelea kwa uchunguzi kamili wa mauwaji ya Zaida Catalan na Michael Sharp.

Jean-Bosco Mukanda, shahidi wa mtuhumiwa ambaye anazuiliwa akihusishwa katika kesi hiyo inayoendelea huko Kananga, awali alitangaza mbele ya majaji kuwa Kankonde ndiye ambaye alichukuwa nywele za Zaïdan Catalan baada ya kuuawa kwake.

Mwendesha mashtaka wa kijeshi huko Kananga amesema kwamba Kankonde atafikishwa mahakamani hivi karibuni. Washtakiwa ishirini na nne bado wako wanazuiliwa jela, watatu wamefariki dunia na wawili wametoroka katika mazingira ya kutatanisha.

Michael Sharp, raia wa Marekani na Zaida Catalan, raia wa Sweden waliuawa Machi 2017 wakati walipokuwa wakifanya uchunguzi kwa ajili ya Umoja wa Mataifa kuhusu makaburi ya pamoja kwenye jimbo la Kasai ya Kati.