1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtu mmoja ajeruhiwa katika shambulio la roketi mjini Baghdad

Amina Mjahid
27 Januari 2020

Shambulio la roketi lililotokea usiku wa kuamkia leo katika ubalozi wa Marekani mjini Baghdad limemjeruhi mfanyakazi mmoja wa ubalozi huo hii ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa za ndani ya ubalozi huo.

https://p.dw.com/p/3Wsck
Irak Anti-Regierungs-Proteste in Bagdad
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mizban

Wafanyakazi wawili wa Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad ambao hawakutaka majina yao kutajwa, hawakutoa maelezo kuhusu utaifa wa aliyejeruhiwa au maelezo zaidi juu ya majeraha aliyoyapata.

Vurugu kati ya maafisa wa usalama nchini Iraq na waandamanaji wanaoipinga serikali pia ziliendelea kushuhudiwa usiku kucha huku mtu  mmoja akiuwawa kwa kupigwa risasi katika kamatakamata iliyokuwa na vurugu kusini mwa taifa hilo. Vurugu nyengine pia zilishuhudiwa mjini Baghdad karibu na uwanja wa Khilani.

Ubalozi wa Marekani  umekuwa ukilengwa kufuatia mvutano unaozidi kupanuka kati ya Marekani na Iran uliyoijumuisha pia Iraq katika wiki za hivi karibuni. Wafuasi wa wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq waliuvamia ubalozi wa Marekani Desemba 31, kuvunja mlango na kuliwasha moto eneo la kuingilia ubalozi huo.

Taarifa za jeshi la Marekani zinasema, maroketi matano aina ya katyusha yalivurumishwa katika eneo maalum lenye ulinzi mkali linalojulikana kama Green Zone, kunakopatikana balozi nyingi za kigeni siku ya Jumapili. Roketi la leo asubuhi ni la tatu kulenga ubalozi wa Marekani mwezi huu huku waliotekeleza shambulio hilo bado hawajajulikana. 

Hata hivyo Marekani inawanyooshea kidole cha lawama wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kwa kushambulia kambi zao za kijeshi nchini humo. Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdul-Mahdi amelaani shambulio la leo na kusema kwamba taifa lake linajizatiti kuulinda ujumbe wa kidiplomasia uliopo nchini humo.

Iraq imekumbwa na maandamano ya takriban miezi mine kupinga ufisadi unaodaiwa kufnywa na serikali, ukosefu wa ajira, na ushawishi wa Iran katika siasa zake.

Chamzo/Reuters