″Mtihani mgumu kwa Sarkozy″ | Magazetini | DW | 21.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Mtihani mgumu kwa Sarkozy"

Kwanza kwa udondozi wa magazeti ya Ujerumani hii leo tunaelekea nchi jirani na Ujerumani, Ufaransa, ambako mgomo wa reli unaendelea. Jana pia walimu na wafanyakazi wa serikali walishirika katika mgomo.

Wafaransa wanaandamana

Wafaransa wanaandamana

Gazeti la “Die Welt” linachambua hivi hali ilivyo huko Ufaransa:

“Kile kilichoanza kama mgomo wa wafanyakazi wa reli, kimeelekea sasa kuwa hamu kubwa ya watu wengi kuanzishwa fujo. Si madereva wa treni wanaoandamana barabarani tu bali pia jumuiya nyingine za wafanyakazi. Karibu kila mwananchi anaona kuna haja ya kupinga mageuzi ya serikali. Rais Sarkozy anataka kushinda vita hivi dhidi ya jumuiya za wafanyakazi na walio faidika na mfumo wa malipo ya pensheni.”


Gazeti la “Financial Times Deutschland” linaamini kuwa Sarkozy atashinda katika mgogoro huu. Lakini matokeo yake ni kuongeza imani katika serikali, kama anavyoandika mhariri huyu:


“Kwa Wafaransa wengi serikali ina jukumu la kuhakikisha ustawi wa wananchi. Rais Sarkozy anafanya kila awezalo kuthibitisha wazo hilo. Ikiwa atashinda katika mgogoro huu kuhusu malipo ya uzeeni, imani kwamba serikali ina uwezo wa kudhibiti kila kitu itaimarika zaidi. Hilo lakini ni kosa kubwa, kwani utandawazi utalibadilisha pia taifa hili la Ufaransa.”


Na hatimaye kuhusu mgomo wa Ufaransa tunasikia maoni ya mhariri wa “Frankfurter Rundschau”. Naye ameandika:


“Rais Sarkozy alitaka mtihani mgumu kuonyesha nguvu yake. Huu basi anao sana. Mbinu yake ni kupigana na watu wengi wakati mmoja. Lakini safari hii huenda atashindwa, kwani hata nchini Ufaransa ni vigumu kutekeleza mageuzi na kupunguza mishahara. Ndiyo sababu, wananchi wengi wanawaunga mkono wafanyakazi wa reli na kushirikana nao mabarabarani, ikiwa ni walimu, wanafunzi, wauuguzi au wengine. Bado lakini Sarkozy anaamini katika msemo usemao: adui wengi, heshima nyingi.”


Ni gazeti la “Frankfurter Rundschau”. Mhariri wa “Süddeutsche Zeitung” amezingatia mkutano wa kilele wa nchi za Kusini Mashariki mwa bara la Asia, ASEAN, ambao unaendelea leo mjini Singapur. Ameandika:


“Kwa kweli, jumuiya hiyo ya ASEAN imejiharibia yenyewe. Siku ya kuadhimisha miaka 40 tangu kuasisiwa, imemzuia mgeni wa heshima kutoa hotuba yake mbele ya baraza hilo, yaani Ibrahim Gambari. Mwanadiplomasia huyu wa Umoja wa Mataifa alijitahidi sana kutuliza mambo huko Myanmar. Lakini Myanmar wala China hazikutaka Gambari ahutubie jumuiya hiyo. Nchi majirani na Myanmar, wakati huu wote wa mzozo wa Myanmar zilitumia hoja kwamba kulingana na desturi zao haipaswi kumtuhumu mwingine hadharani, ndiyo maana zilikaa kimya. Lakini kwani nini viongozi hao hao walimnyamazisha sasa Gambari? Kwa kumkatalia mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kutoa hotuba yake, jumuiya ya ASEAN imepoteza imani yake yote."

 • Tarehe 21.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CQ86
 • Tarehe 21.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CQ86
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com