1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Mtambue Sundiata Keita

Sudi Mnette
25 Julai 2018

Sundiata Keita ni mfalme wa Mali aliyeacha muongozo wa utawala wa kukumbukwa katika mataifa ya Mali, Guinea, Senegal na Gambia.

https://p.dw.com/p/2tOk2

Kwa kuziunganisha falme zilizogawika vipande vipande katika karne ya XIII Afrika Magharibi, Sunjata Keita anaeandikwa pia kama Sundiata au Soundiata amebuni enzi za ufalme ambazo mpaka leo waimbaji mashuhuri na waandishi vitabu wanausifu. Simba wa Mandingue Sunjata alikuwa kwa wakati mmoja mpigana vita jabari na kiongozi wa taifa mwenye busara.

Maisha yake: Alizaliwa mlemavu mwaka 1190 huko Niani katika ufalme mdogo wa Mandingo ( Nyanda za juu nchini Guine), alilazimika kukimbilia uhamishoni baada ya kifo cha baba yake, mfalme Naré Maghann Konaté. Aliwika baadae katika vita dhidi ya mfalme wa Sosso, Soumaoro Kanté na kugeuzwa Mansa, mfalme wa wafalme, baada ya mapambano ya Kirina mnamo mwaka 1235. Alifariki dunia mwaka 1255 akiacha nyuma utawala wa ufalme mkubwa kupita kiasi.

Historia ya Sunjata Keita imekuwa ikienezwa kupitia simulizi na imegeuka hadithi ambayo inasimuliwa kwa namna tofauti na hakuna kilichoandikwa.

African Roots Sunjata Keita
Sunjata Keita Picha: Comic Republic

Hekaya zinasema alizaliwa mlemavu, Sunjata, alipomuona siku moja mama yake anadhalilishwa, alinyanyuka mwenyewe na kuanza kwenda moja kwa moja, kwa lengo la kumhami: "hatua zake za mwanzo hazikuwa kubwa", anasimulia Mamadou Kouyaté katika usimulizi wake "Sunjata au ufalme wa Mandingo", usimulizi uliotajwa sana na mwanahistoria Djibril Tamsir Niane katika kitabu chake kilichochapishwa mwaka 1960 cha Shirika la uchapishaji la Présence Africaine.

Mwindaji mkubwa na mpigana vita jabari, Sunjata amefanikiwa kuziunganisha falme za Afrika Magharibi, zilizogawika tangu ulipoanguka ufalme wa Ghana. Ushindi wake mkubwa unasalia kuwa ule wa Kirina mnamo mwaka 1235 dhidi ya mfalme Sosso Soumaoro Kanté ambapo Sunjata alitangazwa kuwa Mansa, Mfalme wa Wafalme.

Mtambue Sunjata Keita

Akiongoza enzi yake ya kifalme Sunjata alijitambulisha kutokana na kiu chake cha kuyaunganisha makabila yote, akibuni jamii zilizojengeka kwa msingi wa koo. Aligawa ardhi, haki na majukumu kwa kila koo moja. Anatajikana pia kuwa mwanzilishi wa "Mwongozo wa Mandén au Mwongozo wa Kouroukan Fouga uliotungwa mwaka 1236 na kuangaliwa na baadhi ya watu kuwa waraka wa kwanza kuhusu haki za binaadam barani Afrika. Mwongozo huo umeingizwa katika turathi ya utamaduni wa binaadam tangu mwaka 2009 katika shirikia la Umoja wa Mataifa la UNESCO.

Kwakua hakuna ushahidi wa kimaandishi,wanahistoria wanafuata usimulizi unaotolewa mara nyingi na watu wa karibu na faamilia ya Keita.


Tamara Wackernagel, Sidiki Doumbia na Philipp Sandner wamechangia katika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.

Tafsiri: Hamidou, Oumilkheir
Mhariri: Yusuf Saumu