Mswaada wa Bajeti ya Ujerumani ya mwaka 2011 | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.07.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mswaada wa Bajeti ya Ujerumani ya mwaka 2011

Serikali ya Ujerumani imewasilisha mswada wa bajeti yake ya mwaka ujao wa 2011 pamoja na mpango wake wa fedha hadi mwaka 2014.

default

Waziri wa fedha wa Ujerumani Bw.Wolfgang Schäuble

Kilicho kizuri ni kwamba yaonekana Ujerumani itabidi ichukuwe mikopo michache zaidi kuliko vile ilivohofiwa hapo mwanzoni.

Serikali ya mseto ya Ujerumani mnamo siku mbili imeweza kuvivuka vizingiti vikubwa. Jumanne iliopita, wakuu wa serekali hiyo walikubaliana vipi mfumo wa afya utakavogharimiwa siku za mbele hapa nchini. Hiyo ilikuwa mada ambayo zaidi kuliko nyingine yeyote ilioleta mabishano ndani ya serikali hiyo ya muungano, hivyo kusababisha serekali hiyo kuwa na sura ya kusikitisha machoni mwa watu. Na jana baraza la mawaziri liliipitisha bajeti ya mwaka ujao wa 2011 na pia ramani ya matumizi ya fedha za serikali hadi mwaka 2014, yaani kipindi cha kutoka sasa hadi baada ya uchaguzi mkuu ujao. Mpango huo wa kazi ya tarakimu umetilia maanani na kuupa sura ule mkakati uliotokana na hatua kubwa ya kuunusuru uchumi, jambo lilokuwa lazima lifanyike kutokana na mzozo wa mabenki.

Kwa wananchi wengi, marekebisho ya kiuchumi, bila ya hata kuwauliza, ni mada inayowagusa sana, kwa vile wao ndio walipaji katika mfuko wa bima ya afya, wakiwa wagonjwa na pia wafanya kazi katika shughuli za afya. Mada hiyo pia ni ya kusisimua, kisiasa, kama vile serikali ya Ujerumani, kwa masikitiko, ilivotambua punde.

Lakini mada ilio muhimu zaidi ni bajeti ya serikali. Hapo mwanzoni watu waliona ni kutia chumvi pale bajeti ya serikali inapotajwa kwamba ni kitabu kinachoamua hatima ya taifa. Lakini leo hisia hiyo haiko tena.

Majukumu makubwa ya kifedha ambayo Ujerumani, kama vile mataifa mengine pia, yamebeba katika kupambana na mzozo wa mabenki yasingestahiki zaidi kwa waziri wa fedha kujifanya kama vile hayajui, ingekuwa hakuna mzigo mkubwa wa riba za kulipa kutokana na mikopo iliochukuwa serikali katika miongo ya miaka iliopita. Kila mwaka waziri huyo anabidi apate Euro bilioni 40 kulipia riba hizo. Na zaidi ya miaka arobaini sasa, mlima wa madeni ya serikali unazidi kupanda juu. Hata imefika hadi kwamba matokeo yake ni kuwa serikali inabidi ichukuwe mikopo zaidi, ili tu iweze kulipia riba za mikopo ya zamani.

Deutschland Haushalt Regierung Finanzminister Wolfgang Schäuble

Bw.Wolfgang Schäuble akizungumza mkutanoni kuhusu bajeti ya mwaka ujao.

Hali hiyo imekwenda vizuri katika miaka arobaini iliopita. Lakini katika miongo ya miaka ijayo, idadi ya wakaazi hapa Ujerumani itapungua, na hiyo ina maana ya mambo mawili: Mzigo huo wa madeni utagawiwa baina ya mabega machache ya watu, na kwa kila mlipaji kodi mbinyo wa kutakiwa agharamie utazidi. Na ikiwa idadi ya wakaazi nchini itapungua, basi kusitarajiwe kwamba uchumi utapanda zaidi; hivyo kusitarajiwe mapato makubwa ya kodi ambayo yataweza kuziba matundu katika bajeti.

Sasa serikali ya Ujerumani inafanya - chini ya masharti magumu yaliotokana na mzozo wa kifedha ambao haujatanzuliwa bado- kile ambacho zamani sana ingebidi kukidhibiti. Kwamba waziri wa fedha anataka kwa nguvu zaidi kubana matumizi na kupunguza madeni kuliko vile inavotakiwa na katiba ya nchi, ni jambo la kijasiri, lakini, licha ya kuwa ni jambo chungu, hilo ni jambo la lazima. Na hata hivyo, mlima huo wa madeni mwaka hadi mwaka utapanda juu, japokuwa kidogo kidogo. Lini utaanza mlima huo wa madeni kupungua, ni jambo ambalo bado halionekani.

Mwandishi: Stützle, Peter/Othman, Miraji/ZR

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com