Msichana wa miaka 19 ahukumiwa kifo Sudan | Masuala ya Jamii | DW | 11.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Msichana wa miaka 19 ahukumiwa kifo Sudan

Msichana mmoja aliye na miaka 19 amehukumuhiwa kifo na Korti moja nchini Sudan baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mumewe wa kulazimishwa, alipojaribu kumbaka.

Msichana huyo Noura Hussein alilazimishwa kuolewa na binamu yake akiwa na miaka 16, aliikataa ndoa hiyo na kukimbilia kwa jamaa yake aliyoishi naye kwa miaka mitatu. Baadaye mwezi Aprili mwaka huu alirejea nyumbani nje kidogo ya mji wa Khartoum  baada ya babake kumwambia ndoa hiyo imefutiliwa mbali. Lakini alikuta kuwa mipango ya harusi yake ilikuwa bado inaendelea.

Baada ya kuolewa, Noura alikataa kufanya tendo la ndoa na mumewe na ilipofika siku ya sita, mumewe alimbaka huku jamaa zake wa kiume wakimshikilia Noura kwa nguvu  ili kurahisisha kitendo hicho. Siku ya pili mumewe alijaribu tena kumbaka. Noura alimchoma kisu na kumuua wakati alipojaribu kuzuwia tendo hilo.

Africa Child Marriage Mosambik (picture alliance/AP Photo/S.Mohamed)

Mikono ya msichana aliye na miaka 18 na mumewe wa miaka 20

Aidha Korti ya Sharia inayofuata sheria za kiislamu ilimkuta msichana huyo na kosa la mauaji mwezi uliyopita na siku ya Alhamisi wiki hii, ikamhukumu kifo kwa kunyongwa.

Hata hivyo mawakili wake kwa sasa wana siku 15 za kukata rufaa huku wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu wamepaza sauti zao juu ya hili kwa kumtolea wito rais Omar al Bashir kumsamehe msichana huyo,wakisema ilikuwa hatua ya kujilinda. 

"Chini ya sheria ya kiislamu familia ya mume inaweza kudai fidia ya fedha au kifo, walichagua kifo na hicho ndicho kilichofuatwa," alisema  Badr Eldin Salah, mwanaharakati kutoka Vuguvugu la vijana wa Afrika waliokuwa Kortini wakati hukumu hiyo ilipotolewa. 

Badr Salah ameongeza kuwa mawakili wa Noura watakataa rufaa dhidi ya hukumu hiyo lakini pia kunahitajika uungwaji mkono kutoka jamii ya Kimataifa na kutoka katika jumuiya kama Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.

Sheria za Sudan zinaruhusu ndoa pindi msichana anapovunja ungo

Sudan imechukua nambari 165 kati ya nchi 188 katika orodha ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya usawa wa kijinsia, inayolinganisha nafasi ya  wanawake na wanaume kuhusu upatikanaji wa huduma  za afya, elimu, ujumuishwaji kisiasa na fursa za ajira.

Sudans Präsident Omar Hassan el Bashir, Porträt (dpa)

Rais wa Sudan Omar el Bashir

Sudan ni mojawapo ya nchi barani Afrika zilizo na sera dhaifu kuwalinda wanawake na wasichana. Kwa mfano Ubakaji katika ndoa pamoja na ndoa za utotoni hazichukuliwi kama kosa. Sheria za taifa hilo zinaruhusu msichana kuolewa pindi anapovunja ungo, na zinakubali pia msichana wa miaka kumi kuolewa na mlezi wake kwa ruhusa ya jaji.

Wakati huo huo Yasmeen Hassan Mkurugenzi wa shirika la Equality Now amesema Noura ni mhanga na anapaswa kushughulikiwa kama muathirika, huku akisistiza kuwa katika mataifa mengi muathirika kama Noura hupata huduma mbali mbali ili kuhakikisha anaondokewa na kiwewe baada ya kukutwa na tukio kama hilo.

Yasmeen anasema kumhukumu tu kwa tukio la uhalifu kutokana na kujilinda na shambulio  ni udhalilishaji wa haki zake chini ya katiba ya Sudan na chini ya sheria za kimataifa.

Mwandishi:  Amina Abubakar/Reuters

Mhariri: Gakuba, Daniel

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com