1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msichana wa Kijerumani atekwa nyara Kabul

Admin.WagnerD17 Agosti 2015

Mwanamke mmoja wa Kijerumani ambaye ni mfanyakazi wa shirika la maendeleo la Ujerumani GIZ, ameripotiwa kutekwa nyara mjini Kabul, Afghanistan leo hii na watu wawili ambao walikuwa wamejihami kwa silaha

https://p.dw.com/p/1GGpf
Zum Thema Afghanistan - Die deutschen Entwicklungshelfer bleiben
Picha: picture-alliance/dpa

Hili ndiyo tukio la karibu kabisa kutokea, katika mfululuzo wa mashambulizi ya namna hii yanayolenga wafanyakazi wa kigeni katika mji wa Kabul ambao hali yake ya usalama bado inazorota.

"Sina hakika kama hili jambo limetokea kweli ama la. Ninachokijua ni kile ambacho nimekisoma katika vyombo vya habari vya hapa Ujerumani. Siwezi kutoa uthibitisho. Lakini tunafanya uchunguzi wa tuliyoyasikia na tutatoa taarifa rasmi haraka iwezekanavyo," alisema Martin Schafer, msemaji mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani akiwa anazungumza na waandishi habari kuhusiana na ripoti za kutekwa kwa raia huyo.

Halikadhalika bado hakuna hakika kama waliomteka nyara mwanamke huyo ni wanamgambo ama kundi la kihalifu. Mpaka sasa hakuna aliyejitangaza kuhusika na utekaji nyara wa mfanyakazi huyo wa kigeni wa shirika la misaada, ambalo ni tukio la pili kuwahi kutokea katika miezi ya karibuni mjini Kabul.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Najib Danish amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa hadi sasa bado uchunguzi unaendelea.

Duru za usalama zimesema mwanamke huyo ni mfanyakazi wa shirika la maendeleo la Kijerumani la GIZ. Na mapema mwaka huu mtu mwengine ambaye ni mfanyakazi wa shirika hilo hilo alitekwa nyara.

Mwezi wa Juni msichana mwengine wa kigeni ambae ni mfanyakazi wa shirika la lisilo la serikali la kiswisi na mwenye asili ya kidachi, pia alitekwa nyara na bado hajulikani alipo. Kwa mujibu wa ujumbe wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, katika mwaka 2014 pekee wafanyakazi 57 wa mashirika ya misaada ya kigeni waliuliwa nchini humo.

Siku ya Jumamosi, ubalozi wa Marekani mjini Kabul uliwaonya raia wote wa Kimarekani katika ujumbe wa dharura, kuwa wapiganaji nchini humo wana mipango ya kufanya mashambulizi zaidi katika maeneo yanayotembelewa na wageni.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/dpae

Mhariri:Iddi Ssessanga