1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshauri mwingine wa Trump ajiuzulu

Sylvia Mwehozi
7 Machi 2018

Mshauri mwandamizi wa uchumi wa rais Donald Trump, Gary Cohn amejiuzulu wadhifa wake, na kumfanya kuwa afisa wa karibuni katika mfululizo wa maafisa wa ngazi ya juu wanaoachia ngazi katika utawala wa Marekani.

https://p.dw.com/p/2tpFG
USA Gary Cohn in der Lobby des Trump Tower in New York
Picha: picture-alliance/dpa/Pool/CNP/A. Lohr-Jones

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kwamba Cohn, Mdemocrat na anayepigia upatu biashara huria, ameshindwa kukubaliana na uamuzi wa Trump wa kuongeza ushuru katika bidhaa za chuma na alumini zinazoingia nchini humo, akidai kwamba ulipaji kisasi kutoka nchi nyingine utaziadhibu biashara za Marekani nje ya sekta hizo.

Ripoti zinasema kwamba maoni ya Cohn yamekataliwa na wasaidizi wengine waandamizi ambao wanasema ilikuwa ni muhimu zaidi kwa Trump kufuata kampeni kubwa aliyotoa iliyosaidia kuwaleta wafanyakazi wa kawaida katika chama cha Republican.

Mkuu wa utumishi John Kelly amesema Trump amemshukuru Bw. Cohn kwa utumishi wake, na kumuelezea kama mmoja ya watu wachache walio na "vipaji", na kwamba ameitumikia nchi yake kwa utumishi uliotokuka.

Hope Hicks
Hope Hicks aliyekuwa mkurugenzi wa mawasiliano White House naye alijuzulu Picha: Reuters/C. Barria

Cohn, anakuwa afisa wa karibuni katika mfululizo wa washauri waandamizi kujiuzulu au kufutwa kazi. Hope Hicks, pengine ambaye alikuwa ni msiri wa kuaminika zaidi kwa Trump, alitangaza Jumatano iliyopita kwamba anajiuzulu kama mkurugenzi wa mawasiliano.

Hatua yake hiyo ilifuatia kuondoka kwa mkuu wa utumishi Reince Priebus, mshauri wa usalama wa taifa Michael Flynn na wengine.

Kumekuwa na uvumi wa karibuni wa kujizulu kwa Kelly pia, pamoja na mshauri wa usalama wa taifa HR McMaster. Katika taarifa yake Cohn, amesema "imekuwa ni heshima kuitumikia nchi yangu" na kusema kwamba anamshukuru rais kwa kumpatia fursa hiyo.

Trump baadae aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba "atafanya maamuzi hivi karibuni ya kumteua mshauri mpya wa uchumi". Zaidi Trump amesema wapo watu ambao wangependa kufanya kazi Ikulu. "Watu wengi wanataka kuingia. Ninaweza kuchagua yeyote. Ninaweza kuchukua nafasi yoyote White House na nitachagua watu 10 bora wanaohusika na nafasi hiyo. Kila mtu anataka kuja hapa na wanaipenda White House kwasababu tuna nguvu kuliko hapo kabla."

USA Michael Flynn beim Briefing im Weißen Haus in Washington
Michael Flynn, alikuwa mshauri wa usalama naye alijiuzulu Picha: Reuters/C. Barria

Awali Trump alikana ripoti za vyombo vya habari kuwepo na taharuki ndani ya White House lakini akaongeza kwamba kuna watu bado anaotaka wabadilike. Mahusiano baina ya wanaume hao wawili mara kwa mara yameonekana kuwa si thabiti.

Masoko yalihakikishiwa siku ya jumanne kwamba ushuru huo hauwezi kuwa mbaya na vita vya biashara inaweza kuepukika, lakini kuondoka kwa Cohn kunaashiria kuwa masoko siku ya Jumatano yanaweza kuyumba. Mpango wa ushuru uliofutiwa na kitisho ckutoka kwa Trump cha kuweka "kodi sawa" kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nchi zinazotoza kodi kwa bidhaa za Marekani.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Saumu Yusuf