Mshambuliaji wa London ni mfungwa wa zamani wa ugaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.11.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mshambuliaji wa London ni mfungwa wa zamani wa ugaidi

Mtu aliyekuwa amevaa kizibao bandia cha mabomu amewachoma kisu watu kadhaa mjini London, na kuwauwa wawili katika kile polisi inakichukulia kuwa shambulizi la kigaidi.

Polisi imesema mshambuliaji huyo alikuwa Usman Khan, mwenye umri wa miaka 28 ambaye aliachiliwa huru kutoka jela mwaka jana baada ya kutumikia kifungo cha miaka sita kwa makosa ya ugaidi.

Mkuu wa Polisi ya London Cressida Dick amesema wahanga wawili, waliochomwa kisu walifariki dunia na watu watatu waliojeruhiwa wanatibiwa hospitalini. Polisi imesema Khan alihukumiwa kifungo mwaka wa 2012 kwa makosa ya ugaidi na akaachiwa Desemba 2018.

Inadaiwa kuwa Khan alikuwa akihudhuria hafla ya London iliyoandaliwa na Learning Together - mpango wa Chuo Kikuu cha Cambridge ambao unawapa elimu wafungwa – wakati alipofanya shambulizi hilo, na kumuuwa mwanamme na mwanamke na kuwajeruhi wengine watatu.

England London Bridge Schießerei | Spurensicherung

Mtuhumiwa alipigwa risasi na kuuawa na polisi

Historia ya mshambuliaji huyo itazusha maswali magumu kuhusu serikali na mashirika ya usalama ya Uingereza. Neil Basu, mkuu wa polisi ya London ya kupambana na ugaidi, alisema polisi wanawasaka washukiwa wengine wowote.

Waziri Mkuu Boris Johnson amesema kwa muda mrefu amekuwa akihoji kuwa ni makosa kuwaruhusu wahalifu wa mashitaka mazito kuachiliwa mapema kutoka jela.

Johnson, ambaye aliongoza mkutano wa dharura wa kamati ya COBRA ya serikali jana jioni, alisema polisi zaidi wataweka doria mitaani katika siku zijazo ili kuwahakikishia wananchi usalama.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni chini ya wiki mbili kabla ya Uingereza kuandaa uchaguzi mkuu. Vyama vya kisiasa vilisitisha kwa muda kampeni zao mjini London kama ishara ya heshima.

Viongozi wa kisiasa wameelezea kushtushwa kwao na huzuni kutokana na shambulizi hilo la Ijumaa. ``Hatutanyamazishwa na wale wanaotutishia,'' alisema kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn. ``Lazima na tutasimama pamoja kukataa chuki na mgawanyiko."