1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako wa mtuhumiwa wa Berlin waghadhibisha raia

22 Desemba 2016

Wakati polisi wakiendelea na msako mkali dhidi ya washukiwa wa mashambulizi ya Soko la Krismas mjini Berlin yaliyouwa watu 12, vyombo vya usalama nchini Ujerumani vimekumbwa na ukosoaji mkubwa.

https://p.dw.com/p/2UiHy
Deutschland Berlin Sicherheitsmaßnahmen nach Anschlag
Picha: Getty Images/AFP/C. Bilan

Ukosoaji mkubwa unakuja baada ya kubainika kwamba vyombo vya usalama vilikuwa vikimtambua mtuhumiwa namba moja wa mashambulizi hayo, Mtunisia Anis Amri, ambaye ombi lake la hifadhi nchini Ujerumani lilikataliwa baada ya kutambulikana kuwa alikuwa ni mwanamgambo hatari wa siasa kali.

Mamlaka hizo za usalama zilimuainisha Amri kama kitisho katika miezi kadhaa iliyopita. Msako wa mtuhumiwa huyo muhimu wa shambulizi hilo, umeibua maswali mengi, huku raia wengi wakishangazwa na namna ambavyo Anis Amri alifanikiwa kuepuka kukamatwa na kurejeshwa kwao pamoja na kuwa mtu aliyekuwa akichunguzwa na taasisi za kiintelijensia za Ujerumani.

"Aliwahi kuwa kwenye kambi ya watu wanaorejeshwa makwao, lakini aliachiwa baada ya siku moja", amesema msemaji wa masuala ya ndani kutoka muungano wa vyama vya kihafidhina ndani ya bunge, Stephan Mayer, alipokuwa akizungumza na kituo cha redio cha RBB, Alhamisi hii. Amesema tukio hili linaonesha mapungufu katika sera za hifadhi za Ujerumani na kutoa mwito wa kuwepo kwa muda wa kukaa kwenye vizuizi vya kurejeshwa kwa raia wanaokataliwa hifadhi.

Kaka wa Amri, Abdelkader Amri, amesema wameshtushwa na taarifa hizo, na kuelezea kusikitishwa kwake na raia wengine wa Tunisia kutokana na hatua ya Amri ya kujihusisha na shambulizi hilo.

Deutschland Breitscheidplatz nach dem Anschlag in Berlin
Picha: DW/F. Hofmann

Mwendesha mashtaka wa Ujerumani ametoa notisi ya kusakwa kwa mtuhumiwa huyo na zawadi ya euro laki moja kwa atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwake. Ameonya kwamba raia huyo wa Tunisia anaweza kuwa na silaha na ni hatari.

Gazeti la Suddeutche Zeitung limekosoa mamlaka kwa kupoteza muda zikimlenga mtuhumiwa kutoka Pakistan, na baadaye kutambua kwamba hawakuwa sahihi.

Katika hatua inayoonyesha kuibua hasira ya raia, maafisa wa Ujerumani wamesema walikuwa wakimchunguza Amri na kuhisi kwamba alikuwa akipanga kufanya shambulizi. 

Waziri wa masuala ya ndani wa Jimbo la North Rhine Westphalia, Ralf Jaeger, amesema maafisa wa kukabiliana na ugaidi hivi karibuni walibadilishana taarifa kuhusu Amri, na kuanzisha uchunguzi kuhusu mtuhumiwa huyo aliyekuwa akijiandaa kufanya shambulizi kubwa.

Kushindwa kwa hatua za kiusalama katika shambulizi hili kumeibua ukosoaji mkubwa dhidi ya sera za kiliberali za wakimbizi za Kansela Angela Merkel, zilizoruhusu mamilioni ya watu kuingia Ujerumani mwaka jana. Idadi hiyo kubwa ilikikasirisha chama cha kizalendo cha AfD, kinachopingana na sera za Merkel kwa kusema anahatarisha usalama wa taifa.

Hata baadhi ya wanachama wa chama cha Merkel cha Christian Democratic Union, CDU, wamekosoa kile wanachoona kuwa ni hatari zaidi katika mfumo uliopo sasa. "Kitaifa kuna idadi kubwa ya wakimbizi wasiojulikana wanakotoka ama hata majina yao, na hili ni suala muhimu zaidi la kuangaziwa kwenye usalama wa taifa," amesema Klaus Bouillon wa CDU, ambaye ni waziri wa masuala ya ndani wa Jimbo la Saarland.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP/DW
Mhariri: Mohammed Khelef