Msako dhidi ya wamiliki wa mitandao ya kijamii Tanzania | Matukio ya Afrika | DW | 20.09.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Msako dhidi ya wamiliki wa mitandao ya kijamii Tanzania

Wamiliki kadhaa wa mitandao ya kijamii ambayo haijasajiliwa Tanzania, wanashikiliwa na polisi. Baadhi ya wanaoshukiwa kumiliki mitandao hiyo ni msemaji wa Chama cha Demokrasia ba Maendeleo (CHADEMA) Tumaini Makene

Mamlaka nchini Tanzania zinaendelea na msako mkali dhidi ya wamiliki wa mitandao ya kijamii ambayo haikusajiliwa kwa mujibu wa sheria na hadi sasa tayari wamiliki kadhaa wanashikiliwa na polisi wakihojiwa. Kukamatwa kwa wamiliki hao ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ambayo licha ya kulalamikiwa vikali na makundi ya wanaharakati, ilianza kutekelezwa mwanzoni wa mwezi huu. 

Msako huo unaendeshwa nchi nzima na ripoti za hivi sasa zinasema kuwa baadhi ya wamiliki au wanaoshukiwa kuwa wamiliki wa mitandao hiyo, akiwamo msemaji wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Tumaini Makene, wanaendelea kushikiliwa na polisi wakihojiwa, ingawa hadi sasa hakuna taarifa zozote endapo watafikishwa mahakamani au la.

Sheria yalenga kuwadhibiti wapasha habari wenye nia mbaya

Chama chake jana kilithibitisha kukamatwa kwa msemaji wake huyo lakini kikasema hakifahamu kwa nini anaendelea kushikiliwa na polisi kwa vile madai aliyokamatwa nayo hayahusiani na yeye kwa vile mtandao unaodaiwa kuuendesha, Chadema Blog, unamilikiwa na wapenzi wa chama hicho walioko nje ya nchi.

Hii ni mara ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo mpya kwa Mamlaka ya Mawasiliano nchini, TCRA, kuendesha msako dhidi ya wale wasiosajiliwa na kulingana na Mkurugenzi James Kulaba, hivi karibuni sheria hiyo mpya imelenga kuwadhibiti wapasha habari wenye nia mbaya. 

TCRA, yawataka wamiliki wa blogu na mitandao ya kijamii inayotumika kama vyombo vya habari kujisajili la sivyo wakumbwe na mkono wa sheria.

TCRA, yawataka wamiliki wa blogu na mitandao ya kijamii inayotumika kama vyombo vya habari kujisajili la sivyo wakumbwe na mkono wa sheria.

Mbali ya Makene, mtangazaji wa kituo kimoja cha televisheni na mshereheshaji ikiwa ni baadhi ya wale walionaswa na operesheni hiyo ambayo inafanyika miezi michache tangu Mamlaka ya Mawasiliano, TCRA, kuwataka wamiliki wote wa blogu na mitandao ya kijamii inayotumika kama vyombo vya habari kujisajili vyenginevyo wakumbwe na mkono wa sheria.

Sheria hiyo inazima nafasi za ajira na uhuru wa kujieleza?

Pamoja na kwamba sheria hiyo imekuwa ikitajwa miongoni mwa sheria zitakazowabana Watanzania kutumia uhuru wa maoni, baadhi ya wanablogu waliojisajili wamekuwa na maoni tofauti juu ya utekelezaji wake. John Bukuku, anayeendesha mtandao wa Fullshangwe, anasema vijana wanaochipukia fursa ya kupanuka na kukua kwa mitandao ya kijamii hawana chaguo lingine zaidi ya kukubaliana na kile kilicholetwa mezani:

Kuletwa kwa sheria hii kumekuwa pigo kubwa kwa vijana wengi ambao waliona kuwa sasa pengine wangeweza kutumia uwanja wa kupanuka mitandao ya kijamii kujipatia ajira na wakati huohuo kuendelea kufurahia uhuru wa mawasiliano kama asemavyo Denis George, ambaye licha ya kusajili mtandao wake, anaona kiwango cha ada ni kikubwa mno:

Baadhi ya watetezi wa habari na utoaji maoni wamesema watakwenda mahakamani kupinga sheria za aina hiyo.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef