Msafara wa mwenge wa Olimpiki - athari kwa michezo? | NRS-Import | DW | 09.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Msafara wa mwenge wa Olimpiki - athari kwa michezo?

Msafara wa mwenge wa Olimpiki ukiwa ni moja kati ya matukio muhimu ya leo, unazingatiwa pia na wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani, hususan baada ya maandamano yaliyofanywa barani Ulaya na pia huko Marekani.

default

Msafara wa mwenge wa Olimpiki unalindwa na polisi

Kwanza ni gazeti la “”Emder Zeitung” ambalo limeandika:


“Dunia nzima ilishangaa vile China ilivyobadilika na kuwa nchi muhimu ya kiuchumi duniani katika muda wa miaka michache tu. Wakiinama na kuomba ushirikiano, wanasiasa na mameneja wa ulimwengu mzima walisafiri hadi China. Lakini wote walifunga macho yao na walikataa kufahamu kwamba, maendeleo haya ya haraka ya kuelekea kwenye ubepari yaliwezekana tu kwa kuwakandamiza wananchi wa China. Sasa, msafara huu wa mwenge wa Olimpiki, ambao juu ya hayo yote ulianzishwa na Wanazi wa Ujerumani mwaka wa 1936, unatoa mwanga juu ya hali ilivyo. Ni kama udikteta huu mkali unafichuliwa kabisa na kuwekwa wazi mwangani.”


Mwenge wa michezo ya Olimpiki unatumiwa kama ishara pia na gazeti la “General-Anzeiger” la hapa mjini Bonn. Limeandika:


“Kwa mtazamano wa Wachina ambao wana uzoefu mkubwa wa kutumia ishara, mwenge huu wa Olimpiki ni ishara ya kuwepo moto kubwa ambao lazima uzimwe haraka. Lakini wao wenyewe wanatupa picha kama wana woga wa kukithiri kuwa watu wengine wanataka wasifanikiwe na wakati huo huo kutoviruhusu vyama vingine vya kisiasa nchini mwao. Hivyo wanatoa ushahidi kwamba bado wako mbali na kuwa na demokrasia. Basi suali ni: jee, wanaopaswa kushtakiwa ni nani? Si ni halmashauri kuu ya Olimpiki ulimwenguni ambayo iliruhusu michezo hii ifanyike China? Basi, lazima kuliangalia suala hili kwa njia tofauti kabisa, kwani bila ya kuichagua China hatungekuwa na mjadala huu. Basi inawapasa wahusika wa michezo hii wajiingize katika mjadala huu! Hiyo ndiyo ingekuwa ishara bora kabisa.”


Tukiendelea na gazeti la “Financial Times Deutschland”, mhariri huyu anajihusisha na suala hilo hilo la michezo na siasa na anaamini kwamba:


“Wanaharakati wa haki za binadamu wataitumia michezo hii ya Olimpiki nchini China hadi siku yake ya mwisho kupigania malengo yao. Basi, matumaini ya halmashauri kuu ya Olimpiki ulimwenguni ya kwamba michezo hii haitaingiliwa na siasa si tu ya kijinga, bali pia kwa kuamini hivyo, inaficha sera kali za ukandamizaji za China. Badala ya kuzungumzia ikiwa msafara wa mwenge wa Olimpiki utafanywa tena, halmashauri kuu ya Olimpiki inapaswa kuweka wazi msimamo wake kuhusu haki za binadamu na kuitaka serikali ya China kuziheshimu haki hizo.”


Na hatimaye tusikie yalivyoandikwa na gazeti la “Tageszeitung” la mjini Berlin:


“Maandamano haya ya Ulaya na San Francisco yanaiathiri michezo ya Olimpiki kwa ujumla ikiwa na lengo la kuwaleta pamoja watu wa dunia nzima katika amani. Ni kosa kubwa kwamba hakuna jukwaa lolote rasmi la kupinga propaganda ya nchi mwenyeji wa michezo hii. Jamii inatakiwa tu kuwashangilia wanamichezo na wanaobeba mwenge. Lakini katika dunia ya kisasa, watu hawakai tena kimya.”

 • Tarehe 09.04.2008
 • Mwandishi Dreyer, Maja
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Dekn
 • Tarehe 09.04.2008
 • Mwandishi Dreyer, Maja
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Dekn
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com