1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wauwa 50 katika tafrja ya harusi Uturuki

21 Agosti 2016

Takriban watu 50 wameuwawa Jumamosi(20.08.2016) wakati anayetuhumiwa kuwa mripuaji wa kujitowa muhanga alipojiripuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakicheza ngoma mtaani wakati wa sherehe ya harusi kusini mwa Uturuki.

https://p.dw.com/p/1JmTl
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/S. Suna

Takriban watu 50 wameuwawa hapo Jumamosi(20.08.2016) wakati anayetuhumiwa kuwa mripuaji wa kujitowa muhanga aliporipuwa vilipuzi vyake miongoni mwa watu waliokuwa wakicheza ngoma mtaani wakati wa sherehe ya harusi kusini mwa Uturuki.

Rais Tayyip Edogan amesema yumkini wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu wamefanya shambulio hilo wakati wa usiku ambalo ni shambulio lililosababisha maafa makubwa mwaka huu nchini Uturuki nchi inayokabiliwa na vitisho vya wanamgambo ndani ya nchi na kutoka Syria.

Wiki chache tu zilizopita Erdogan na serikali yake walinusurika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa ambalo serikali ya Uturuki inamlaumu Sheikh Fethulah Gulen anayesihi uhamishoni nchini Marekani kuwa na mkono wake lakini mwenyewe amekanusha madai hayo.

Kundi la Dola la Kiislamu limekuwa likilaumiwa kwa kuhusika na mashambulio mengine nchini Uturuki mara nyingi ikilenga mikusanyiko ya Wakurdi ili kupalilia chokochoko za kikabila,shambulio lao baya kabisa likiwa lile la mwezi wa Oktoba mwaka jana wakati wa maandamano ya kuwaunga mkono Wakurdi na wanaharakati wa haki za wafanyakazi mjini Ankara ambapo waripuaji wa kujitowa muhanga wameuwa zaidi ya watu 100.

Sherehe zillikuwa zinamalizika

Tafrija ya harusi ya Jumamosi ilikuwa ikifanyika katika mji wa Gazianstep ulioko kama kilomita 40 kutoka mpaka wa Syria na ilikuwa imamhusu mwanachama wa chama chenye kuwaunga mkono Wakurdi cha Demokasia ya Wananchi (PDP) ambapo inaelezwa kwamba bwanaharusi ni miongoni mwa majeruhi wakati biharusi hakujeruhiwa.

Familia zikiomboleza hosptalini.
Familia zikiomboleza hosptalini.Picha: Getty Images/AFP

Sherehe zilikuwa zikimalizika kwa usiku wa kupaka hina ambapo wageni hujipaka hina kwa nakshi tofauti mikononi na miguuni mwao.Baadhi ya wana familia walikuwa tayari wameondoka wakati bomu hilo liliporipuka ambapo watoto na wanawake ni miongoni mwa waliouwawa.

Damu na alama za kuunguwa zimejitokeza kwenye uchochoro mwembamba ambapo ndiko ulikotokea mripuko huo.Wanawake waliokuwa wamevaa vitambaa vya kichwa yaani hijabu walikuwa wakilia wakati wakiwa wamekuwa wameketi nje ya chumba cha kuhifadhia maiti wakisubiri kupata habari juu ya ndugu zao wasiojulikana walipo.

Veli Can mmojawapo wa shuhuda mwenye umri wa miaka 25 amekaririwa akisema "Sherehe zilikuwa zikimalizika wakati kulipotokea mripuko mkubwa miongoni mwa watu waliokuwa wakicheza ngoma na damu na vipande vya mwili vimetapakaa kila mahala."

Mamia wahuhudhuria mazishi

Mamia wamekusanyika kwa ajili ya mazishi Jumapili (21.08.2016)wengine wakilia kwenye majeneza yaliofunikwa vitaambaa ya kijani ambayo ni rangi ya Uislamu.Lakini maziko mengine itabidi yasubiri kwa sababu wahanga wengi wamekatika vipande vipande na kutahitajika vipimo vya vinasaba kuweza kuwatambuwa.

Watu wakikusanyika kufuatia mripuko.
Watu wakikusanyika kufuatia mripuko.Picha: Getty Images/AFP

Uturuki ilianza mashambulizi ya anga dhidi ya Dola la Kiislamu mwezi wa Julai mwaka jana wiki chache baada ya kusambaratika kwa mchakato wa amani na kundi la Wakurdi la PKK na pia ililenga mashambulizi hayo dhidi ya maeneo ya kundi hilo la PKK yaliyoko kaskazini mwa Iraq.

Hapo Jumamosi wabunge wa chama tawala cha AK halikadhalika Rais Erdogan yeye mwenyewe binafsi amesisitiza kwamba haoni tafauti ya kundi la Dola la Kiislamu na wanaharakati wa Kikurdi wanaotaka kujitenga wa PKK na kundi linaloongozwa na Sheokh Gulen.Serikali imeyaainisha makundi yote hayo kuwa ya mgaidi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Isaac Gamba