1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wa ebola katika wilaya tano za Uganda ungali hatari

3 Novemba 2022

Wizara ya afya nchini Uganda imefahamisha kuwa hali ya mripuko wa ebola katika wilaya tano za kati mwa nchi ingali ya hatari

https://p.dw.com/p/4J1bl
Uganda | Ebola Ausbruch | Gesundheitsministerin Ruth Aceng
Picha: Hajarah Nalwadda/Xinhua/picture alliance

Wizara ya Afya ya Uganda imesema kufuatia hali hiyo, hawawezi kufanya maamuzi ya kuondoa zuio kwa shughuli za watu eneo hilo.

Hadi kufikia sasa kati ya watu 131 waliogunduliwa kuwa na ugonjwa huo, 46 wamefariki ikiwemo watatu walioshiriki katika kuzikua maiti ya jamaa yao aliyefariki kutokana na ugonjwa huo. 

Kinyume na matarajio kwamba baada ya siku 21 wilaya ambako wakaazi waliwekwa chini ya karantini zingerejelea shughuli zao, wizara ya afya inasema itakuwa hatari kubwa kufanya hivyo.

WHO: Chanjo za majaribio za ugonjwa wa Ebola kupelekwa Uganda

Hii ni baada ya wizara pamoja na shirika la afya duniani WHO kufanya tathmini na kugundua kwamba idadi ya wanaougua Ebola inaongezeka hasa katika wilaya ya Kasanda.

Watu wote 23 wa wilaya hiyo ambao walishiriki shughuli ya kufukua maiti ya jamaa yao wakitaka kumzika kwa heshima wameambukizwa huku watatu kati yao wakifariki.

Wakaazi wa eneo hilo wamelezea madhila wanayoyapitia katika kipindi hiki cha zuio ambapo shughuli za biashara na uchukuzi hasa zimeathirika.

Ugonjwa wa Ebola wazua taharuki Uganda

Wakati huo huo, pamezuka mabishano kati ya wafadhili na serikali ya Uganda kuhusu matumizi ya fedha zilizotolewa kama msaada wa kupambana na mripuko huo wa Ebola.

Serikali ya Marekani ikisambaza taarifa kuwa imetoa kiasi cha dola milioni 22 na kuonyesha kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo ni kugharamia zoezi la kuwafuatilia walioambukizwa. Lakini serikali ya Uganda inadai kuwa haijapokea fedha zozote kutoka kwa wafadhili.

Hata hivyo, waziri wa afya aliandamana na maafisa wa balozi mbalimbali katika ziara yake eneo ambalo linaelezwa kuwa chimbuko la ugonjwa huo. Waziri amefahamisha kuwa  ujenzi na upanuzi wa vituo zaidi vya kuwashughulikia wagonjwa wa ebola ni hatua ambayo serikali imechukua kuweka mfumo thabiti wa kupambana na janga hilo.

Hadi kufikia sasa kati ya watu 131 waliogunduliwa kuwa na ugonjwa huo, 46 wamefariki ikiwemo watatu walioshiriki katika kuzikua maiti ya jamaa yao aliyefariki kutokana na ugonjwa huo. Lubega Emmanuel DW Kampala.