Mripuko wa bei ya mafuta ghafi washtusha | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mripuko wa bei ya mafuta ghafi washtusha

Ongezeko kubwa la bei ya mafuta lililovunja rekodi hivi karibuni,limesababisha wasiwasi katika sekta ya uchumi kote duniani.Mawaziri wa Nishati wa kundi la G-8 wameonya juu ya hatari kwa uchumi kudorora duniani kote.

Wengi walishtushwa,bei ya mafuta ghafi ilipoweka rekodi mpya hapo Ijumaa kwa kufikia Dola 159 kwa pipa.Kwani siku hizi za karibuni,kimsingi hakuna kilichobadilika upande wa mahitaji na uzalishaji wa mafuta.Ukuaji mkubwa katika nchi zinazoinukia kiuchumi hasa China,unaongeza mahitaji ya mafuta duniani wakati uzalishaji wa mafuta ukiongezeka pole pole.

Lakini kwa sababu ya matatizo ya kiufundi,viwanda vya kusafishia mafuta vinashida kutimiza mahitaji yaliyoongozeka.Kwani tangu miaka mingi,shirika la nchi zinazozalisha mafuta OPEC,limedharau kupanua viwanda vyake vya kusafishia mafuta na mahitaji makubwa ya hivi sasa hayawezi kutimizwa kwa haraka.Huo ni ukweli unaojulikana tangu muda mrefu,lakini juma lililopita kwa ghafula bei ya mafuta iliongezeka kwa kiwango kikubwa mno.

Inasemekana aliesababisha mripuko huo wa bei bila ya kutaka ni Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Ulaya,Jean-Claude Trichet.Kwani juma lililopita kwenye mkutano wa Baraza la Benki Kuu,aliyaonya masoko ya fedha kujitayarisha kwa ongezeko la riba.Matamshi hayo yalipandisha thamani ya Euro katika masoko ya fedha na Dola ikaporomoka.Na Dola inayopoteza thamani huchochea ulanguzi wa bei ya mafuta.Kila mmoja anapoamini kuwa bei ya mafuta itaongezeka,basi kweli bei huongezeka;na walanguzi katika masoko ya hisa ndio huitumia nafasi hiyo kuipandisha zaidi.

Lakini bei ya mafuta inapozidi kwenda juu,nishati mbadala ndio huvutia zaidi,hata kama kiuchumi nishati ya aina hiyo kwa hivi sasa haina faida.Wanasayansi ndio wapo mbioni na utafiti wao kutafuta njia za kuzalisha nishati kutoka raslimali isiyomalizika kama vile jua,maji,upepo na ujoto wa ardhi badala ya mafuta ambayo siku moja yatakujamalizika.

Kwa hivyo bei za mafuta na gesi ya ardhini zikizidi kuongezeka,uwekezaji wo wote utakaosaidia kupunguza kutegemea mafuta,utavutia zaidi.Mataifa yaliyoendelea kiviwanda yana nafasi moja tu kujitoa katika janga la mripuko wa bei ya mafuta,bila ya uchumi wake kuporomoka vibaya:- nchi hizo upesi iwezekanavyo,ziache kutegemea mafuta na gesi ya ardhini hata ikiwa utaratibu huo utagharimu fedha nyingi.

 • Tarehe 10.06.2008
 • Mwandishi R.Wenkel.R - (P.Martin)
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EGim
 • Tarehe 10.06.2008
 • Mwandishi R.Wenkel.R - (P.Martin)
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EGim
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com